Walivyoanzisha kiwanda cha kuchakata mboga na matunda
FAITH Kwamboka, ni mwekezaji mchanga ambaye ni mmoja wa waanzilishi wa Desiccated Sweetness, kampuni ya kuongeza thamani mboga na matunda iliyoko Kaunti ya Nyamira.
Hamasa yake kuanzisha kiwanda hicho cha kuchakata bidhaa za kilimo, inatokana na mahangaiko aliyoshuhudia wakazi wa eneo analotoka waliyopitia, wakiwemo wazazi wake, mazao mabichi ya shambani kuharibika kwa kukosa soko.
Faith akahisi ana jukumu kuwaokoa, na kufanya kilimo kuwa biashara yenye mapato.
Kulingana na data za Wizara ya Kilimo, Kenya hupoteza karibu asilimia 30 ya mazao ya kilimo kwa kuharibika, hasa kwa sababu ya wakulima kukosa soko na miundomsingi bora kuyahifadhi.
Hali kadhalika, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Kimataifa (FAO), Kenya hupoteza kati ya asilimia 30 hadi 50 ya mazao ya mboga na matunda, kwa kuharibika.

Mwaka wa 2021, Faith na mwanzilishi mwenza, Lucy Amecha, walisajili Dessicated Sweetness ili kuandaa jukwaa la kusaidia kuangazia gapu hiyo.
“Kwa kuongeza mazao ya kilimo thamani, tunafungua mianya ya soko na kupunguza upotevu hivyo kuboresha maisha ya wakulima,” Faith anasema.
“Kiwanda chetu kando na kupunguza upotevu wa mazao, tunalenga kuinua jamii na vilevile kuhakikisha watu na sekta ya chakula ina viungio,” anaongeza.
Kampuni hiyo husindika mboga na matunda, hivyo basi kurefusha muda wa kudumu na kudumisha virutubisho.
Mboga wanazokausha ni pamoja na sukuma wiki, spinachi na za kienyeji kama vile managu, terere, kunde na saga.

Matunda nayo ni mananasi, maembe, na ndizi, ikiwa ni pamoja na malenge.
“Bidhaa zetu zinalenga wateja wanaojali maslahi yao kiafya, ndani na nje ya nchi,” Faith anaelezea.
Mjasirimali huyu ana Shahada ya Uzamili ya Masuala ya Data kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi na Digrii ya Masuala ya Hesabu kutoka Chuo Kikuu cha Moi.
Hali kadhalika, kijana huyu mwenye umri wa miaka 30, ana cheti cha Uanahesabu (CPA).
Kabla kuzamia biashara ya kuongeza mazao ya shambani thamani, aliwahi kuhudumu kwenye nafasi mbalimbali za kazi, zikiwemo Mtafiti, Mhasibu, na Meneja wa Mikakati katika kampuni ya masuala ya kilimo.

Nyadhifa hizo zilimpa tajiriba na motisha kuzamia jukwaa la kusindika mazao ya kilimo.
“Tulichagua mboga na matunda kupunguza upotevu wa mazao, na kuwapa wakulima fursa ya malipo bora kimauzo,” Lucy Amecha, mwasisi mwenza anaelezea.
Kuanzisha kiwanda hicho, Lucy pia anasema walinuwia kuona wateja wanapata bidhaa zenye virutubisho vya kutosha hasa zenye Vitamini.
Iliwagharimu mtaji wa Sh500, 000 ambazo wanafichua zilikuwa akiba, na kiwango kingine kupigwa jeki na familia na marafiki.
Kuboresha biashara yao, pia wamepigwa jeki na Kenya Climate Innovation Center (KCIC) kupitia mradi wa Agribiz ambapo walipewa hela, na baadaye United States African Development Foundation (USADF) ikawasaidia kununua mashine na mitambo.
“Hali kadhalika, tulipata sapoti nyingine kutoka kwa Jamii Femmes mpango wa wakfu wa kampuni ya Coca-Cola uliotusaidia kukua zaidi,” Faith akaambia Akilimali kwenye mahojiano ya kipekee.

Desiccated Sweetness imeimarika na kunawiri kiasi kwamba mwaka uliopita, kampuni hiyo ilishinda zawadi ya AYuTe Africa Challenge Kenya, tuzo inayotolewa na kufadhiliwa na Shirika la Heifer International ambalo hutambua vijana wenye bunifu na teknolojia kuboresha sekta ya kilimo.
Aidha, walikabidhiwa hundi ya Sh1.9 milioni, ambazo wanasema zitasaidia kuboresha biashara yao zaidi.
Kampuni iliyoanza na wafanyakazi wanne pekee, sasa inajivunia kuwa na 20 miaka minne baadaye.
Faith ndiye Afisa Mkuu Mtendaji, naye Lucy akiwa Afisa Mkuu wa Mikakati.
Kampuni hiyo ikiwa ilianza na nafasi kidogo tu ya kukodisha, sasa ina kiwanda cha kisasa Mjini Ekerenyo, Kaunti ya Nyamira, bidhaa zake pia zikiteja wanunuzi kutoka ng’ambo hasa Amerika.

Wateja wao ni wenye maduka ya kuoka vitafunwa, hoteli na kampuni za kuunda peremende.
Bidhaa wanazotengeneza ni vipande vya matunda vilivyokaushwa, unga wa mboga, mboga zilizokaushwa na krispi.
Mazao ya shambani, wana zaidi ya wakulima 1, 000 ambao huwasambazia kutoka Kisii na Nyamira, na pia kaunti jirani kama Siaya na Migori.
Aidha, wana viwango ambavyo wameweka vya mazao wanayopokea na taratibu za kuongeza thamani.
