Walivyounda chama cha ushirika kupitia uchuuzi wa maziwa kuboresha bei
MIAKA 16 iliyopita katika Kaunti ya Nandi, kundi la wakulima liliungana kusaka bei bora ya maziwa.
Hatua hiyo, ilitokana na kuendelea kunyanyaswa na mabroka waliokuwa wakinunua bidhaa hiyo kwa bei wanayotaja ni “ya kutupa”.
Karibu miongo miwili baadaye, kundi hilo la jumla ya wafugaji 12,000 wa ng’ombe wa maziwa sasa wanajivunia kuanzisha chama cha ushirika kinachojulikana kama Lelchego Marketing Cooperative Society Limited.
“Lita moja, awali kabla ya kuwa kwenye kundi ilikuwa ikinunuliwa chini ya Sh20 na mawakala,” anakumbuka Samuel Samoei, meneja wa chama hicho kilichoko eneo la Mosoriot, Kaunti Ndogo ya Chesumei, Nandi.

Kwa sababu ya kughadhabishwa na mabroka waliowafinyilia, Samoei anasema walianza kuuza maziwa kwa njia ya kuchuuza Nandi.
Hilo, walipania kusaka bei bora ya bidhaa hiyo ya ng’ombe.
Samoei, kwenye mahojiano ya kipekee na Akilimali, alidokeza kwamba wakulima wapatao 300 mwaka wa 2009 walishikana mikono na kuanzisha kundi lililowaleta pamoja.
“Tulikubaliana kila memba awe akichanga Sh200 kwa mwezi,” akaelezea.
Ni muungano uliowawezesha kupanua soko kutoka Kaunti ya Nandi, hadi kaunti jirani ya Uasin-Gishu na Kisumu, bei ya maziwa ikiandikisha kuimarika.

Mwaka mmoja baadaye, 2010, kundi hilo lilifungua kituo cha kuchemsha maziwa na kuyapoesha na kuyahifadhi eneo na Mosoriot.
Samoei, anafichua; “Ilitugharimu kima cha Sh2 milioni, kununua mitambo ya shughuli hiyo.”
Mtaji huo ulikuwa mkopo kutoka kwa shirika la kifedha, ambao tayari walishakamilisha kuulipa.
Mbali na kuwa na kituo cha Mosoriot, wanachama wa Lelchego Marketing Cooperative Society Limited ambao tayari wametinga zaidi ya 12,000, pia wana kingine Uasin-Gishu. Kilisajiliwa rasmi 2017 kama chama cha ushirika.

Aidha, hukusanya maziwa kutoka kwa wakulima na kuyatafutia soko lenye ushindani mkuu.
Kulingana na Samoei, meneja, lita moja huinunua Sh45 – kutoka kwa wakulima. “Kisha, tunauzia viwanda vya kusindika na kuongeza thamani kwa Sh51,” akafichua afisa huyo ambaye pia ni mfugaji.
Kampuni wanazosambazia zinatoka Kisii, Limuru, Nyandarua, Eldoret, Nandi, na pia New Kenya Cooperative Creameries (KCC) ni mteja wao mkuu.
Ni muungano unaodhihirisha kauli ‘Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu’, Ruth Chelimo, mwanachama na mkulima kutoka eneo la Kosirai, Nandi akikiri chama hicho cha ushirika kuboresha maisha ya wakulima.

“Kupitia uchuuzaji, broka anakulipa pesa za siku hiyo pekee na soko lake si la kudumu. Ushirik, mfugaji ana imani kupata soko bora linalodumu, na lenye faida,” anaelezea mwanachama huyo ambaye pia ni memba wa bodi ya chama hicho.
Chelimo, anaongeza kuwa uzalishaji umeongezeka kutoka lita 1,800 hadi zaidi ya lita 20,000 kwa siku, ingawa msimu wa kiangazi hupungua hadi lita 8,000.
Mama huyo pia anakiri ushirika huo umeinua wanawake. “Hapo awali wanawake walikuwa chini ya asilimia 10 ya washirika. Sasa ni zaidi ya asilimia 50,” anasema, akiongeza kuwa aliacha kazi ya ofisi ili kujikita katika ufugaji wa ng’ombe wa maziwa.
Chama hicho pia kina Sacco, inayotoa mikopo, pembejeo na mafunzo kwa wanachama.

“Kiasi cha hisa zetu kimefikia zaidi ya Sh12 milioni,” Samoei akaambia Akilimali kwa fahari.
“Isitoshe, tunawapa wanachama mikopo kujiendeleza na tunazalisha chakula cha mifugo kwa bei nafuu na kuwasaidia wakulima kupunguza gharama za lishe.”
Kikiwa kilianza na makarani wawili, sasa kina wafanyikazi 20 bila kusahau wahudumu wa bodaboda wanaokusanya maziwa kutoka kwa wakulima na kulipwa Sh3 kwa kila lita.
Kufikia kilipo, wanachama hao hawajakuwa kwenye safari ya kuimarika wakiwa pekee yao.

Washirika kama serikali kuu, ya kaunti ya Nandi, East Africa Dairy Development (EADD), na Heifer International, kati ya wengineo, wamekuwa wenye mchango mkuu, ikiwemo kusaidiwa kununua trekta.
Nandi huzalisha wastani wa lita milioni 300 za maziwa kila mwaka, kwa mujibu wa serikali ya kaunti hiyo.
“Tumejizatiti kuhakikisha kwamba Nandi inaongoza kwa uzalishaji wa maziwa,” anasema Kiplimo Lagat, Waziri (CECM) wa Kilimo na Maendeleo ya Ushirika.

Kulingana na afisa huyo, Kaunti ya Nandi ina zaidi ya wakazi 150,000 wanaojihusisha moja kwa moja na shughuli za kilimo, ambapo takriban asilimia 43 wanashiriki ufugaji wa ng’ombe wa maziwa.
Anabainisha kuwa kaunti hiyo ina vyama vya ushirika 43, ambavyo vimechangia pakubwa kuimarika kwa sekta ya maziwa nchini.