Makala

WAMALWA: Ipo haja ya kuweka vigezo maalum vya kufuzu kutoka daraja moja hadi jingine

September 12th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

NA STEPHEN WAMALWA

WIZARA ya Elimu nchini inahitaji kulishughulikia kwa dharura suala la kuwepo kwa vigezo vya kutegemewa vya kuwawezesha wanafunzi kufuzu kwenda daraja nyingine ya masomo.

Kila mara pamekuwa na haja ya kuongeza au kushusha viwango vya kufuzu ima kwa wanafunzi wa darasa la nane kwenda shule ya upili, wa shule ya upili kujiunga na vyuo vya kiufundi, vyuo anuwai, vyuo vya mafunzo ya huduma za serikali au hata kujiunga na vyuo vikuu.

Hali hii imezua mizozo ya mara kwa mara miongoni mwa wadau wa elimu kila wakati matokeo ya mtihani wa kitaifa yanapotangazwa.

Mwaka jana na hata mwaka huu, vyama vya kutetea maslahi ya walimu nchini KNUT na KUPPET pamoja na wadau wengine walilitaka baraza la mitihani nchini KNEC kufichua vigezo walivyoweka wakati wa kutahini na kusahihisha mtihani wa kitaifa wa KCSE.

Walitilia shaka mchakato mzima kutokana na idadi ndogo ya wanafunzi kufuzu kwenda vyuo vikuu na hata kutishia kwenda mahakamani kupinga matokeo ya mitihani hiyo. Taswira hii haikuwa nzuri hasa katika jukwaa la kimataifa ambako sekta ya elimu nchini Kenya inaheshimiwa.

Mfano hai wa hivi karibuni ni hatua ya mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya kitaifa inayoshughulikia vigezo vya kufuzu masomoni, KNQA, Dkt. Juma Mukhwana, kutangaza kuwa mamlaka hiyo imeidhinisha kuwa wanafunzi waliopata alama ya D+ katika mtihani wa kitaifa wa KCSE watajiunga na vyuo vya kutoa mafunzo ya walimu wa shule za msingi.

Waliopata alama ya C na C- wataweza kusomea taaluma hiyo kwa kiwango cha stashahada au diploma.

“Mabadiliko haya yatahakikisha kuwa tuna walimu wa kutosha nchini kwa kuwa sasa taaluma hii inatishiwa na mabadiliko mengi yanayoendelea kufanywa katika sekta ya mafunzo ya kiufundi nchini,” akasema Mukhwana.

Tangazo hili lilitolewa wakati ambapo tayari tuna walimu 295,000, kulingana na sajili ya huduma za walimu nchini TSC, waliofuzu kutoka katika vyuo vya mafunzo ya walimu na ambao hawajaajiriwa.

Taaluma ya ualimu ni mfano tu kwani taaluma zingine nchini zinashuhudia hali kama hii, dhihirisho kuwa pana tatizo katika mfumo wa elimu.

Tunahitaji kuchunguza upya utahini na usahihishaji wa mitihani ya kitaifa au hata ya vyuo tukifahamu matakwa ya daraja za baadaye za masomo kwa wale tunaowatahini.

Wadau wa elimu kutoka sekta zote sharti washiriki mazungumzo kuhusu jambo hili, wafanye utafiti wa kina na matokeo ya utafiti huo yajadiliwe na kutekelezwa kikamilifu kwa kubuni sera itakayothibiti mchakato huu la sivyo, kitumbua cha elimu yetu kitaingia mchanga.

Mwandishi ni mhadhiri wa lugha na fasihi ya Kiafrika katika Chuo Kikuu cha Mafunzo ya Kigeni cha Tianjin Uchina

[email protected]