• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 7:02 PM
Wamiliki wa nyumba wapoteza wateja mvua zikiharibu makazi

Wamiliki wa nyumba wapoteza wateja mvua zikiharibu makazi

NA FRIDAH OKACHI

WAMILIKI wa nyumba katika kijiji cha Karide, eneo bunge la Kikuyu, Kaunti ya Kiambu wanaendelea kuhesabu hasara kutokana na mvua inayoendelea kunyesha nchini.

Bw Peter Mbuthia, mmiliki wa nyumba zaidi ya 30, amepoteza wateja 21 ambao walikuwa wamekodisha nyumba na maduka. Bw Mbuthia anasema kufikia sasa amepata hasara ya zaidi ya Sh80,000.

Nje ya maduka yaliyo na kivukio | PICHA| FRIDAH OKACHI

“Nyumba zimebaki bila watu. Kuna nyumba ambazo mimi hupokea kodi Sh4,800 na zingine Sh5,200. Kuna wale wanaondoka na kudai niwape pesa walizoweka kwangu kabla ya kuingia,” asimulia Bw Mbuthia.

Mmiliki huyo, alilalamikia serikali ya Kaunti ya Kiambu na Nairobi, kwa kuelekeza maji machafu kwenye eneo lake baada ya kukosa kukamilisha ujenzi wa barabara iliyoazishwa miaka miwili iliyopita.

“Unaona haya maji yote lazima yapite kwenye nyumba hizi. Serikali ya Kiambu imeshindwa kukamilisha barabara hii kwa kukosa kuunda mabomba ya kupitisha maji taka,” alieleza Bw Mbuthia.

Mmoja wa wakazi Bi Jecinta Wanja aliambia Taifa Leo kuwa hawakuwa na matarajio mvua hiyo kunyesha zaidi. Bi Wanja alisema maji ya mvua hiyo yaliingia kila pande ya nyumba.

“Kwa sasa bidhaa zilizo kwenye duka langu, zimeharibika.  Unga na sukari ya wateja zimepatwa na unyevu. Wakati wa mapishi, mvua inaponyesha inafika hadi jikoni,” alisema Bi Wanja, 42.

Baadhi ya maduka yaliyoachwa na wapangaji | PICHA| FRIDAH OKACHI

Aliongeza kuwa maji yenye uvondo yamekuwa yakisambaa kila chumba, hadi kupoteza hamu ya kula.

“Nikipika sili kwa sababu ya mtaro ambao unaelekeza maji kwenye nyumba zetu. Waliokuwa wakijenga barabara hii, walitengeneza nusu na kuacha nusu ya bomba la kupitisha maji taka likiwa halijakamilika,” alisimulia muuzaji huyo.

Mfanyabiashara mwingine alisema kuamkia asubuhi ya Jumatatu alipata maji yakiwa yamejaa kwenye duka lake.

Bi Tabitha Wanjiku, 34, alisema licha ya kulipa leseni kwa serikali bado wanahangaika.

“Siku ya kwanza nilikuwa nimeacha vitu chini. Vitu vilivyoharibika vipo kwenye fundi na vingine nikatupa. Na hata sikuwa nimetumia. Sasa hivi nasubiri nipewe pesa zangu za deposit nitoke,” alieleza Bi Wanjiku.

Wakazi na wafanyabiashara, sasa wanataka serikali kuu na ile ya kaunti kuwasaidia kurekebisha bomba la kupitisha maji taka.

  • Tags

You can share this post!

Baadhi ya shule zahiari kukaa na wanafunzi waliowasili ili...

Kitanda kidogo ni smaku ya ndoa, mshauri wa masuala ya...

T L