Makala

Wanaharakati wakerwa mtoto mchanga ‘kukamatwa’ kwa sababu ya bunduki, risasi na bangi

May 30th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NA MWANGI MUIRURI

WANAHARAKATI wa kutetea haki za watoto pamoja na baadhi ya wanasiasa wameungana kulaani kisa ambapo mtoto wa umri wa miezi minne katika Kaunti ya Meru ‘alitiwa mbaroni’ na polisi mnamo Mei 26, 2024, kwa sababu ya bunduki, risasi na bangi.

Mkurugenzi wa Kituo cha Haki na Watoto nchini Bi Olive Osoro aliambia Taifa Leo kwamba kuna ubutu wa kiutawala ambao unaangazia wahusika katika baadhi ya utekelezaji sheria kama walio na ukatili katika matendo yao ya kushtua.

Bi Osoro alisema kwamba ripoti ya polisi kuhusu kisa hicho ilikuwa sawa na uhalalishaji wa dhuluma dhidi ya watoto, hasa huyo wa umri wa miezi minne pekee ambaye hata hajui bunduki, risasi na bangi ni nini.

Ripoti hiyo ya polisi wa kituo cha Mutuati iliangazia kisa ambapo maafisa walivamia boma la Bw Geoffrey Thuranira,29, baada ya kupokezwa habari za ujasusi kwamba alikuwa mhalifu.

“Tulifika katika boma hilo lililoko katika kijiji cha Murunya Kabachi na baada ya kupekua chumba chake cha malazi, tulinasa bangi ya thamani ya Sh100,000, bunduki moja aina ya AK-47 pamoja na risasi 20,” ripoti hiyo yasema.

Inaendelea kuelezea jinsi mshukiwa huyo mkuu alihepa kupitia kuruka ua na akatimua mbio kijinusuru akipotelea kwa shamba la ndizi.

“Ni hapo ndipo tulimtia mbaroni mke wake aliye na umri wa miaka 21 pamoja na mtoto wake wa umri wa miezi minne na ambao tuliwakabidhi kwa maafisa wa idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai ili uchunguzi wa kina uendelezwe,” ikasema.

Bi Osoro alisema kwamba katika taarifa hiyo ya polisi–na ambayo Taifa Leo iliona–haiwataji mama huyo na mtoto wake kama washukiwa bali katika kuwarejelea, polisi aliyeiandika aliwatambua wawili hao kama “mke na mtoto kwa mshukiwa”.

“Hiyo ina maana kuwa mwanamke alikamatwa kutokana na kuishi na mshukiwa kama mkewe huku naye mtoto akitiwa mbaroni kwa kuwa ni mbegu ya mshukiwa,” akasema.

Seneta wa Murang’a Bw Joe Nyutu tayari amelaani kisa hicho akimtaka Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki ambaye ni mzawa wa eneo hilo la Meru awahamasishe polisi kuhusu sheria na Katiba.

Aliwataka maafisa hao wajifahamishe na ibara ya 53: 1(f) ambayo inaelezea waziwazi kwamba mtoto hafai kutiwa mbaroni na ikiwa ni lazima (i) iwe ni kwa muda mfupi iwezekanavyo na (ii) asiwekwe kwa seli ambayo iko na mtu mzima huku mazingira yawe ya kuzingatia jinsia ya mtoto pamoja na umri wake huku, (2) masilahi ya mtoto huyo yakiwa ndio ya maana zaidi na ya kuzingatiwa kuliko utafsiri mwingine wowote wa kisheria”.

Bw Nyutu alisema ujumbe anaopata katika hali hiyo ni kwamba mtoto hafai kuwekwa seli iliyo na mtu mzima hata ikiwa huyo mtu mzima ni mama yake.

“Kwa sasa kile tumeshuhudia ni polisi kutozingatia sheria na ninatoa wito wamwachilie mama huyo pamoja na mtoto wake na watie bidii kumnasa yule wanayemwinda kama mshukuwa wao wa uhalifu na ujambazi unaochunguzwa,” akasema Bw Nyutu.

Gavana wa Meru Bi Kawira Mwangaza aliambia Taifa Leo kwamba ashachukua jukumu la kufuatilia hali ya mtoto huyo.

“Kuna suala la kisheria na haki kuhusu watoto… Ni vyema tujue mshukiwa katika madai yanayorejelewa ni nani kwa kuwa hawezi kuwa ni mtoto huyo. Mama mtoto naye hajatambuliwa kama mshukiwa na haieleweki ikawa namna gani ikawa hata mtoto naye wa miezi minne ametiwa mbaroni,” akasema.

Mbunge wa Maragua Bi Mary wa Maua alisema kisa hicho ni cha kushtua na hata hakina nafasi ya kueleweka katika ulimwengu wa sheria na haki.

Alisema kwamba “hata kitendo cha kuambia mama wa umri wa miaka 21 na ambaye ana mtoto wa miezi minne kwamba kwa pamoja wanakamatwa kwa madai kwamba mumewe ni mshukiwa ni hali ambayo inatia wasiwasi sana kuhusu uthabiti wa ukadiriaji hali wa maafisa tulio nao katika ajira”.

Bi Wa Maua alisema kwamba “uhalifu usipewe nafasi katika jamii lakini pia polisi watudhihirishie kwamba huwa na ufahamu wa sheria na haki za binadamu”.