Makala

Wanaume wanyemelea wajane kwa kisingizio cha kujikinga mvua

May 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MWANGI MUIRURI

BAADHI ya wanaume wa mjini Maragua katika Kaunti ya Murang’a wamemulikwa kwa kujikinga mvua katika maboma ya wajane na ya wanawake ambao waume wao wanafanya kazi mbali, wakiwa na lengo la kuwanyemelea kimapenzi.

Watu hao wameonywa dhidi ya tabia hiyo msimu huu wa mvua kubwa.

Mkuu wa tarafa hiyo Bw Joshua Okello, alisema Jumatatu kwamba amepata malalamiko kuhusu wanaume ambao mara tu mawingu ya mvua yanapotanda, wanakimbia kwa nyumba za wajane na pia kwa maboma ambapo mabwana hawako, kwa kisingizio cha kujikinga mvua.

“Nimepata malalamiko kwamba nia ya wanaume wengi sio kujikinga mvua bali ni kuwataka wanawake. Machifu wamechoka kutumwa kuwakanya wanaume walio na tabia hiyo chwara,” akasema Bw Okello.

Alisema kwamba katika kipindi cha wiki mbili sasa, amepokea malalamishi zaidi ya 25 hasa katika mitaa iliyo karibu na miji.

“Wale walioathirika zaidi ni wapangaji katika mitaa ya eneo hili na pia maboma yaliyo karibu na barabara,” akasema afisa huyo.

Wengi wa wanaume hao ni wahudumu wa pikipiki na madalali mijini ambao kazi zao zimewawezesha kutambua maboma yasiyo na ‘wazee’.

Alisema kwamba serikali imewezeshwa na sheria kusaidia ndoa kudumu na pia amani ya wajane katika upweke wao.

“Ni hatia kuvunja ndoa ya mwingine na pia ni makosa kujaribu kutumia ujirani mwema kujinufaisha kwa kumshinikiza mwingine kukuridhisha kimahaba,” akasema.

Bw Okello alisema kwamba wanaume wengi hata sio eti huwa na dharura ya kuhepa mvua bali huwa ni njama wamesuka ya kunyemelea vya wenyewe.

“Wengine huchomoka majumbani mwao na kukimbilia hadi eneo ambalo huwa wamelenga. Kwa kuwa hii mvua inaanza kunyesha mwendo wa saa tisa hivi na kuendelea hadi usiku wa manane, nia ni wahifadhiwe usiku kucha na katika mazingira hayo ya baridi, wahurumiwe na warambishwe asali,” akasema.

Alisema kwamba yeyote atakayetolewa lalama za kuchukulia mvua kama njia ya kunyemelea boma la wenyewe, atakamatwa na awajibishwe kisheria.

“Tukipata ushahidi dhidi ya mshukiwa kwamba alijaribu kutekeleza ubakaji, tutamshtaki kisheria mahakamani. Wale ambao tutapata ni matapeli wa ujirani tutawaandalia vikao vya wazee na tuwatoze fidia,” akasema.