Wanaume wasioweza kutungisha mimba wana wasiwasi mwingi – Utafiti
WANAUME wasiokuwa na uwezo wa kuungisha mimba wanakumbwa na wasiwasi mwingi, utafiti umebaini.
Asilimia 17.5 ya idadi ya watu wote ulimwenguni wanakumbwa na matatizo ya uzazi wanaume na wanawake wakiwa kwenye tapo hili.
Shirika la Afya Duniani (WHO), linasema hali ya wanaume kushindwa kuzalisha huwafanya kupata matatizo ya kisaikolojia, uoga, msongo wa mawazo na pia mara nyingi wao huhangaika kutokana na fikira nyingi kuhusu hali yao.
Tafiti ambazo zimefanywa hapo awali zinasema kuwa wanaume ndio hupatikana na tatizo la mbegu za kiume kukosa kuzalisha kwenye asilimia 50 za ndoa ulimwenguni.
Kulingana na utafiti, wanaume hao hujilaumu, huhisi kuwa hawaridhishi wake wao wakati wa tendo la ndoa na pia hujiona wanaume duni wakilinganisha hali yao na wenzao ambao wamejaaliwa kupata watoto.
Hii ni kwa sababu katika jamii mbalimbali wanaume huthaminiwa na uwezo wao wa kupata watoto na wake wao huku wale waliolemewa wakisawiriwa kama gumegume kitandani.
Mahangaiko hayo ya wanaume wasioweza kuzalisha pia yalichapishwa kwenye jarida la Afya nchini Uingereza (BMC) ambalo lina utafiti uliofanyiwa wanaume wasioweza kuzalisha.
“Utafiti huu ulibaini kuwa wasiwasi mwingi ndio dalili ambayo ilionekana sana kati ya wanaume wasioweza kuwatungisha wapenzi au wake wao mimba. Wasiwasi huo mwingi umechangia afya zao kuwa mbaya na pia wakiugua si rahisi wapone maradhi,” utafiti huo unaeleza.
“Wasiwasi ulipatikana miongoni mwa asilimia 34.9 kwa wanaume wasio na uwezo wa kuzalisha, kiwango ambacho ni cha juu ikilinganishwa na wanaume ambao hali yao ya uzazi haina tatizo lolote.”
Kutokana na hali yao, watafiti walipendekeza wanaume hawa wapokee ushauri nasaha mara kwa mara kwa madaktari na wahudumu wa afya.
Nasaha zinawasaidia kupunguza wasiwasi ili waendelee na maisha yao kama kawaida.