• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 2:03 PM
Wanaume waunguziwa chakula na wake watazamaji wa vipindi

Wanaume waunguziwa chakula na wake watazamaji wa vipindi

NA FRIDAH OKACHI

BAADHI ya wanaume sasa wanalalamika kwamba wake wao wanawapikia na kuwapakulia chakula kilichoungua kwa sababu ya kuzama zaidi kwa vipindi na mitandao ya kijamii. 

Wanaume hao waliambia Taifa Jumapili kwamba majukwaa hayo yamesababisha wanawake kusahau kuwa wana jukumu la kuandalia familia zao chakula kwa njia bora.

Bw Vincent Moturi,38, kutoka mtaa wa Fedha, Embakasi alisema yeye kwa kawaida hukifika nyumbani kabla ya saa moja na nusu jioni lakini mkewe mara nyingine humpakulia chakula kilichoungua.

“Ziko siku ambazo nikiwa hapa nyumbani, hula chakula kilichoungua. Wakati mwingine nalazimika kumkumbusha mke wangu kutoka sebuleni akaangalie iwapo chakula kipo sawa kule jikoni,” akasema Bw Moturi.

Kulingana na baba huyo wa watoto wanne, uraibu wa kutumia mitandao ya kijamii na kutazama vipindi kwenye televisheni, umesababisha migogoro.

“Kila wakati nikimuuliza sababu ya chakula kuungua, husema ni kusahau,” akasema.

Mkewe, Bi Everylene Moturi alikiri mara nyingi hutekwa na kutazama televisheni na kufuatilia maudhui katika mitandao ya kijamii.

Alisema yeye hushtukia muda umesonga mbio mno.

“Wikendi huwa sitatiziki kupika kama siku hizo nyingine. Mitandao ya kijamii huwa na mambo ya kusisimua ambayo huniteka sana. Isitoshe, mimi hupenda kufuatilia na kutaka kufahamu matukio yanayojiri kote nchini,” akasema Bi Moturi.

Lakini alisema kwamba siku hizi ameanza kuwa makini Zaidi wakati akiandaa chakula.

“Kwa kweli kiko kipindi ambapo chakula kiliungua bila ya mimi kujua. Lakini ilikuwa ni mara mbili tu! Mzee wangu alilalamika lakini siku hizi ninajua jinsi ya kujipanga,” akasema.

Bw Moturi alisema hapingi mkewe kufuatilia matini katika mitandao ya kijamii na kutazama vipindi vya runinga, bora tu afahamu umuhimu wa kuipa familia kipaumbele.

Alisema hamshuku mkewe kivyovyote anapokuwa katika mitandao ya kijamii.

“Ana uhuru wa kutazama vipindi vyote na kutumia mitandao ya kijamii jinsi atakavyo. Muhimu kwangu ni awe makini ili kutorejelea kosa,” akasema Bw Moturi.

Katika mtaa wa Satellite jijini Nairobi, Bw Sebastian Mwanza alisema tatizo ni kupakuliwa chakula wakati muda umepita.

Pia anasema mke wake huzamia mitandao ya kijamii kiasi cha kutomjulia chumbani akiwa kwa maktaba yake ndogo pale nyumbani.

Aliambia Taifa Jumapili kwamba huwa na sonona kwa kuhisi mke wake huwa amemsahau.

“Sikumbuki ni siku gani mke wangu alifika kwa maktaba yangu ya nyumbani kunijulia hali,” akasema Bw Mwanza.

“Kila wakati mke wangu akifika nyumbani, sehemu ya sebuleni huigeuza kuwa makao makuu ya kutumia mitandao ya kijamii. Nitamsikia ameingia, kitakachofuata ni sauti za vicheko,” akaongeza.

Alisema yeye na mkewe wamelizungumzia suala hilo na kwamba wako tayari kusuluhisha mgogoro kati yao.

“Huyu mke wangu si yule wa kitambo. Wakati wa kula unafika lakini mapishi bado. Hata watoto wanashikwa na usingizi kabla ya kula,” akasema.

Mfanyabiashara Jecinta Njeri alisema utumiaji wa mtandao wa TikTok umemwezesha kupata wateja wa aina mbalimbali wakati wa kufanya biashara ya moja kwa moja mitandaoni.

Sehemu ya mapishi kwake Bi Jecinta Njeri katika mtaa wa Satellite jijini Nairobi. PICHA | FRIDAH OKACHI

“Ndio, huwa nachelewa kupika chakula cha watoto. Mimi binafsi siitumii mitandao ya kijamii kwa ubaya bali kwa manufaa ya familia yangu,” akasema Bi Njeri.

Mama huyu hata hivyo alikiri kuwa kuna wakati mmoja alisahau kwenda jikoni kuangalia chakula na hivyo akapata kimeungua.

“Tangu wakati huo, mume wangu hunisaidia kupika ili wanangu wale na walale mapema kwa sababu ya shule,” alisema.

Utafiti kutoka Shirika la Pew unaonyesha wanawake wanaongoza kwa asilimia 73 katika matumizi ya mitandao ya kijamii dhidi ya asilimia 65 ya wanaume.

  • Tags

You can share this post!

Muziki unaimarisha ubongo na uwezo wa kukumbuka –...

Hofu kuzaana kuongeza kura kutaangusha Mlima Kenya

T L