Wanavyogeuza sehemu kame kuwa ngome ya kilimo
MWAKA wa 2016, Linda Kamau ambaye ni mwasisi wa Sow Precise Africa, kampuni inayotoa huduma za unyunyiziaji mimea na mashamba maji kwa kutumia nguvu za kawi, aliacha kazi yake kama fundi wa masuala ya Teknolojia ya Habari (IT) katika shirika lisilo la kiserikali (NGO).
Baada ya miaka minane ya ajira, alihisi anataka kibarua kingine kuchangamsha ubongo wake.
Akiwa na ari ya zaraa, aliamua kuingilia shughuli za kilimo katika eneo la Mbeere Kusini, Kaunti ya Embu.
Eneo hilo linaorodheshwa kama eneo kame na nusu-kame (ASAL), ambapo wakazi wanategemea mvua kulima mazao kama mahindi, maharagwe na muguka.

Linda anakuza maharagwe, ambayo huyabadilisha na mahindi.
Hata hivyo, hali ya eneo hilo ilimtatiza wakazi msimu wa kiangazi wakilalamika njaa ilhali wana mashamba.
Ipo mito isiyokauka, na wanaofanya kilimo wakati wa kiangazi hutegemea jenereta zinazotumia mafuta ya petroli ama dizeli ambayo ni ghali.
“Mbeere ni eneo lenye rutuba lakini changamoto kuu ni upatikanaji wa maji kwa bei nafuu,” Linda anasema.
Zaidi ya asilimia 80 ya ardhi ya Kenya ni ASAL, na chini ya asilimia 2 pekee ya ardhi hiyo imekumbatia mifumo ya kunyunyizia mimea na mashamba maji kwa mifereji (irrigation).

Linda anasema aliona gapu kubwa iliyohitaji teknolojia kukabiliana na njaa.
Kwa ushirikiano na wawekezaji wenza; Pius Wambua na Julia Kinuthia, mwaka wa 2022 alianzisha huduma za umwagiliaji mimea na mashamba maji kwa kutumia nguvu za kawi yaani sola.
Hapo ndipo kampuni ya Sow Precise Africa ilipozaliwa, na imekuwa yenye mchango mkubwa Mbeere kusaidia wakazi kushiriki kilimo.
Linda ndiye Mkurugenzi Mkuu, Wambua naye akisimamia mikakati, na Julia ni mhasibu.
Utangulizi, hata ingawa walikuwa na wazo bora ukosefu wa hela kulifanikisha ulikuwa kizingiti.
“Tuliwasilisha pendekezo letu kwa Allan & Gill Gray Philanthropies (AGGP), na tukapata ufadhili (ruzuku) wa Dola 10,000,” Linda anafichua.

AGGP ni wakfu kutoka Afrika Kusini unaolenga kupiga jeki wawekezaji kwenye biashara na maendeleo ya uchumi hasa vijana, Ukanda wa Afrika Mashariki.
Kulingana na Wambua, fedha hizo ziliwawezesha kufanikisha malengo yao.
“Changamoto kuu kwa wawekezaji mara ya kwanza ni kuthibitisha wazo na huduma zao zinaweza kuvutia wateja. Wafadhili wengi huwa makini sana na hilo,” anaelezea.
Walianza kwa kutumia shamba lao la ekari 20 kama mfano, na baada ya kuandikisha mafanikio, wakulima wengine wakajiunga nao.

Kwa sasa, wana mitambo mitano ya umwagiliaji maji kwa kutumia jua waliyoitengenezea nchini, inayojulikana kama Sun Rider.
Mitambo hiyo inajumuisha sola, pampu za maji, kifaa cha kugeuza joto la jua kuwa nguvu za umeme (inverter) kutoa maji kutoka chanzo chake hadi shambani, na bomba.
Vifaa hivyo husafirishwa kwa mkokoteni wa umeme.
Aidha, wajasiriamali hao wabunifu wanalenga wakulima wa kipato cha chini.
Kwa sasa, wanahudumia zaidi ya wakulima 50 na hutoza Sh1,500 kwa kila ekari.

Huduma zao zimewawezesha wakulima wenye kandarasi nao kuzalisha mazao mwaka mzima, hivyo basi kuongeza uzalishaji na kipato.
Mmoja wa walionufaika, Stephen Mutua, kwenye mahojiano na Akilimali alisema alikuwa akitumia zaidi ya Sh4,500 kwa wiki kwa kutumia dizeli, lakini sasa anatumia gharama ya chini kupitia mfumo wa sola.
“Mbali na kulima mahindi na maharagwe, pia hukuza muguka na kwa kutumia dizeli ni bei ghali mno. Kupitia sola, gharama imepungua zaidi ya mara dufu,” alikiri.

“Umwagiliaji maji mimea na mashamba kwa sola ni nafuu na bora zaidi,” akaongeza mkulima mwingine Janet Munguti.
Mwaka uliopita, Sow Precise Africa ilishinda tuzo ya Sh750,000 kutoka kwa Heifer International kupitia mpango wa shirika hilo wa AYuTe 2024, unaotambua vijana wenye bunifu mbalimbali kutoa sulumu kwa sekta ya kilimo.
Fedha hizo, Linda anasema ziliwasaidia kuboresha huduma.