Wanawake bomba Wakenya walioandikisha historia 2024
MWAKA huu 2024 unaokaribia tamati, wanawake wa Kenya waliendelea kukiuka vikwazo na kubobea katika nyanja mbalimbali.
Kuanzia vyumba vya mikutano hadi viwanja vya michezo, mahakama hadi majukwaa ya kimataifa na siasa, wanawake wameweka historia na kuwatia moyo wanawake vijana kuwa na ndoto kubwa na kulenga makuu.
Hawa hapa ni wanawake 10 ambao wamevunja rekodi na kuweka historia katika nyanja mbalimbali.
Dkt Jacqueline Kitulu
Jacqueline ndiye rais wa kwanza kutoka Kenya kuchaguliwa wa Chama cha Madaktari Ulimwenguni.
Safari yake kutoka kuwa daktari wa familia aliyejitolea huko Nairobi hadi kuwa mwanamke wa kwanza Mkenya na Mwafrika wa pili kuchaguliwa kuwa rais wa Chama cha Madaktari Ulimwenguni, ni thibitisho la kujitolea kwake bila kuyumbayumba katika afya.
Alichaguliwa Oktoba kuongoza chama, ambacho kinawakilisha madaktari katika nchi 115.
Huldah Momanyi Hiltsley
Huldah ndiye mzaliwa wa kwanza wa Kenya kuchaguliwa kuwa mwakilishi wa serikali nchini Amerika.
Novemba 6, 2024 akiwa na umri wa miaka 39, alishinda kiti cha Wilaya 38 (sawa na eneobunge) katika Seneti ya Jimbo la Minnesota.
Ushindi wake katika uchaguzi unaashiria mafanikio ya ajabu kwa Wakenya wanaoishi nje ya nchi na kuangazia ushawishi unaoongezeka wa wahamiaji Waafrika katika siasa za Amerika.
Lilian Seenoi-Bar
Lilian ndiye meya wa kwanza mweusi wa Ireland Kaskazini.
Mnamo Juni, aliweka historia kwa kushinda kiti hicho.
Lilian, anayetoka Kaunti ya Narok nchini Kenya, alipigiwa kura kuwakilisha eneo la Foyleside la Derry, Wilaya ya Strabane.
Mwanasiasa huyo amejitolea maisha kutetea haki za kijamii na haki za binadamu na akiwa na umri wa miaka 42, sio mgeni katika kuvuka visiki; mwaka jana, alitawala vichwa vya habari kwa mafanikio ya ajabu ya kuwa mwanamke wa kwanza mweusi kuchaguliwa kuwa mwanachama wa ofisi ya umma katika Ireland Kaskazini kama diwani.
Dorcas Oduor
Agosti 2024, aliapishwa kama Mwanasheria Mkuu wa kwanza wa kike nchini Kenya, kuashiria hatua muhimu katika historia ya sheria ya nchi.
Akiwa na zaidi ya miaka 30 ya tajriba ya kisheria, ikiwa ni pamoja na majukumu kama Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma na kuhusika katika tume mbalimbali, uteuzi wake unaonyesha ustadi wake mkubwa na kujitolea kwake kwa haki.
Mojawapo ya mafanikio yake ni pamoja na kushughulikia kesi ya ulaghai dhidi ya Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu na kesi ya mauaji dhidi ya afisa wa polisi Edward Kirui kuhusu ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007-08 huko Kisumu.
Dorcas, aliweka historia kuwa mwanamke wa kwanza kuteuliwa Mwanasheria Mkuu nchini Kenya na hivyo basi kuwa mshauri mkuu wa kisheria wa serikali, akiwakilisha serikali ya kitaifa, mahakamani na katika kesi nyingine za kisheria.
Katika hotuba yake ya kwanza baada ya kuapishwa, Dorcas alielezea mipango ya mageuzi inayolenga kuifanya idara ya sheria kuwa ya kisasa.
Meja Jenerali Fatuma Gaiti Ahmed
Mei, Meja Jenerali Fatuma Gaiti Ahmed aliweka historia alipoteuliwa kuwa kamanda wa kwanza wa kike kuongoza Jeshi la Wanahewa la Kenya.
Alijiunga na jeshi 1983, akihudumu chini ya Kikosi cha Huduma ya Wanawake.
Aidha, ndiye mwanamke wa kwanza kuteuliwa kuwa Brigedia mwaka wa 2015 na Meja Jenerali mwaka wa 2018.
Kupanda cheo kwake kunaonyesha uongozi wake wa kipekee na kujitolea.
Jackline Juma
Jackline ndiye mwanamke wa kwanza kuwahi kufundisha timu ya wanaume katika Ligi Kuu ya FKF.
Mnamo Agosti, alikuwa mwanamke wa kwanza kusimamia klabu katika Ligi Kuu ya Kenya (KPL) kufuatia kuteuliwa kwake kama mkufunzi wa FC Talanta.
Uteuzi wake ulikaribishwa na wadau wengi ambao waliutaja kuwa hatua ya kwanza ya kuwatambua wanawake katika soka.
Asiya Mohammed
Aliwakilisha taifa kwenye Michezo ya Olimpiki ya Walemavu ya Paris ya 2024, akionyesha maendeleo ya ajabu katika utendaji wake.
Yeye ni mlemavu wa miguu mara mbili ambaye hucheza michezo kadhaa, ikiwa ni pamoja na tenisi ya kiti cha magurudumu, makasia, voliboli ya kukaa, chess na kurusha mkuki.
Sally Njeri
Novemba 2, 2024 Sally mwenye umri wa miaka 64 alitimiza kile ambacho hakuna mtu mwingine yeyote nchini Kenya alithubutu kukiota: kuogelea kwa muda wa saa sita bila kusimama kwa muda wa kilomita saba katika kidimbwi cha kuogelea.
Alikaidi umri katika kuogelea kwa ushindani.
Faith Kipyegon
Mnamo Julai, Faith aliimarisha hadhi yake kama mmoja wa wakimbiaji wakuu wa mbio za kati kwa kushinda dhahabu katika mita 1,500 kwenye Olimpiki ya Paris.
Hii ilikuwa dhahabu yake ya tatu mfululizo katika Olimpiki katika mbio hizo.
Faith anashikilia rekodi za dunia katika mita 1,500 na ni mshikilizi wa zamani wa rekodi ya dunia katika mbio za mita 5,000.
Luteni Kanali Faith Mwagandi
Oktoba 20, Faith aliongoza gwaride la Jeshi la Ulinzi la Kenya kutoka Jeshi la Kenya, Jeshi la Anga la Kenya na Jeshi la Wanamaji la Kenya, ambalo lilikaguliwa na Rais William Ruto.
Aliweka historia kama afisa wa kwanza wa kike wa Jeshi la Wanamaji la Kenya kuongoza gwaride la heshima.
Alijiunga na KDF mwaka 2007, na baadaye kuwa Kamanda wa kwanza wa Kivita katika Afrika Mashariki kutoka 2019 hadi 2022.