Makala

Wanawake Uswahilini wataka mbinu kale za kuandaa vyakula zirejeshwe

Na KALUME KAZUNGU December 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

UVUMBUZI wa teknolojia mbalimbali katika kusuluhisha masuala ya kila siku ya kimaisha yamesukuma jamii nyingi kuzitupilia mbali mila zao.

Hii ni kutokana na kurahisishwa kutekelezwa kwa shughuli hizo kupitia matumizi ya mashine.

Miongoni mwa jamii zilizolazimika kuacha baadhi ya tamaduni zao kutokana na ujio wa teknolojia ni Waswahili, hasa wale wa jamii ya Wabajuni.

Ukanda wa Pwani, Wabajuni hupatikana kwa wingi kwenye kaunti za Lamu, Kilifi na Mombasa.

Wanawake Waswahili wa asili ya Kibajuni waliohojiwa na Taifa Leo walishinikiza haja ya mila za jadi kuenziwa na kushikiliwa zisipotee.

Bi Mwanaisha Mohamed Bunu (kulia) akipepeta mahindi kwa kutumia uteo huku Bi Nana Mote akitazama. Wanawake wa jamii ya Waswahili wa asili ya Wabajuni wanasisitiza haja ya mbinu za zamani za kuandaa chakula kuendelezwa na kuenziwa. PICHA | KALUME KAZUNGU

Miongoni mwa mila hizo ni mbinu za jadi za maandalizi ya chakula.

Wanataja matumizi ya kinu cha kutwangia nafaka, jiwe la kusaga nafaka kupata unga kitamaduni, uteo au ungo wa kupepetea nafaka kuwa miongoni mwa mambo yanayosambaratishwa na usasa.

Bi Nana Mote, mkazi wa Lamu, anazisisitizia jamii za Pwani kuzifurahia na kuziendeleza mbinu zao za kale za kuandaa mlo, akisema ni zenye umuhimu mkubwa, hasa kiafya.

Anasema kuwa matumizi ya teknolojia kwa wingi katika ulimwengu wa leo yameacha wengi, hasa akina mama wakiwa wavivu.

Anashikilia kuwa kukosa kutumia mbinu za jadi kutayarisha mapishi pia kumesababisha vyakula vya kileo kukosa ladha asilia.

Bi Mote anaelezea wasiwasi kwamba mila nyingi za jamii, wakiwemo Waswahili Wabajuni zimeishia kusahaulika, hivyo kuacha kizazi cha sasa, wakiwemo Gen Z kukosa kujua asili yao.

“Tunasisitiza mbinu za kale za kuandaa chakula ziendelee kutumiwa ili mila zetu zisisahaulike. Tunapotumia jiwe la kusaga unga au kinu leo hii tutasaidia hata hawa Gen Z kujua chimbuko lao ni wapi. Mwacha mila ni mtumwa,” akasema Bi Mote.

Bi Mwanasiti Said asema kuinua mchi kutwanga mahindi kwenye kinu au kuviringisha jiwe kusaga unga kienyeji ilikuwa ni mbinu mojawapo ya wanawake Waswahili na wale wa jamii nyingine kufanyisha mwili au viungo mazoezi, hivyo kuepuka kuandamwa na maradhi.

Anasikitika kuwa leo hii hilo halifanyiki kwani kila kitu kimekuwa kinaundwa kupitia mashine.

Alisema itakuwa busara jamii zikiendeleza tamaduni hizo kwa manufaa yao, ikiwemo kiafya.

Anaipa ushauri jamii kwamba hata kama kuna mitambo au mashine za kisasa za kusaga, pia wahakikishe vinu na mawe ya kusagia hayakosekani majumbani mwao.

Bi Said anatoa hoja kwamba wanawake, hasa wale wa Uswahilini huwa na shughuli nyingi za kuiandaa nyumba kiasi cha kukosa nafasi ya kuenda jimu.

“Hivyo tukiwa na jiwe la kusagia, kinu, mchi na ungo kwenye nyumba zetu ninaamini hiyo ni jimu tosha. Tutatwanga, kusaga, kupepeta na kupika, hivyo kutoa jasho na kuipa misuli mazoezi ya kuiimarisha,” asema Bi Said.

Bi Rukia Alwy anaeleza wasiwasi kwamba kupitia matumizi ya teknolojia au mbinu za kisasa kwa wingi, vyakula vya jadi ambavyo vilikuwa vikiandaliwa kienyeji kama vile mikate ya mofa na mingineyo imeanza kupotea.

Mofa ni mkate mgumu wa duara unaotengenezwa kwa unga wa nafaka kama vile mtama, uwele au mahindi.

“Ukiuliza kizazi cha leo jinsi mkate wa mofa au ule wa sinia, wa kumimina na chapati inavyotengenezwa kitakushangaa. Wamezoea mofa unaotengenezwa kupitia mashine. Hata kama vyakula hivyo vipo leo, ladha yake si ile ya kiasilia. Na ndiyo sababu tunasisitiza haja ya watu kuendelea kutumia vinu, mawe ya kusaga, ungo na mbinu nyingine za zamani,” akasema Bi Alwy.

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Wabajuni Lamu, Bw Mohamed Shee Mbwana, anasifu mbinu za kienyeji za maandalizi ya mapochopocho kwa kile anachokitaja kuwa ni kuleta upendo, umoja na ushirikiano kwa jamii.

Bi Somoye Farouk (kusoto) akipepeta nafaka kwa kutumia uteo ilhali Bi Fatuma Walid akisaga mahindi kwa kutumia jiwe la kusaga la kitamafuni. Wote ni akina mama Waswahili wa asili ya Wabajuni. Wanasisitiza mila za kale kuenziwa na kuendelezwa katika utayarishaji wa chakula. PICHA|KALUME KAZUNGU

Bw Mbwana asema katika enzi za utotoni ameshuhudia akina mama kutoka vijiji au familia tofauti tofauti wakikusanyika boma fulani (la mmoja wao) kushirikiana kuponda, kuanika na kusaga mahindi au mtama wakitumia vinu na mawe.

“Ninatamani enzi za kinu na mawe kutumika kwa wingi zijirudie. Watu walidumisha ukarimu na ushirikiano wa hali ya juu, almuradi watayarishe, uwe ni unga wa kupika ugali au chenga za kutayarishia mikate wakiwa pamoja,” akasema Bw Mbwana.

Mtaalamu wa lishe kaunti ya Lamu, Bi Zainab Ahmed asema unga unaosagwa na mashine mara nyingi hupitishwa katika awamu tofauti tofauti zinazoaminika kuondoa au kuchuja madini muhimu kwenye chakula.

“Ila huku kusaga unga kienyeji utapata kunaacha nyuzinyuzi muhimu kwa usagaji wa chakula mwilini. Mashine za kisasa zinapoandaa unga huchuja nyuzinyuzi hizo,” akasema Bi Ahmed.

Ikumbukwe kuwa si Pwani pekee ambapo jamii hutumia vinu, uteo na mawe ya kusagia bali pia sehemu nyingine za Kenya na bara zima la Afrika.

Jamii za Kenya kama vile Wamijikenda, wakiwemo Wagiriama, Waduruma, Wadigo na jamii kama Orma, Wasanye, Wapokomo, Wabaluhya na wengineo pia wamekuwa wakitumia mbinu hizo zamani kabla ya usasa kutwaa hatamu.