Wanawake waliosoma, walioolewa waongoza kwa kuavya mimba – utafiti
WANAWAKE walioko kwenye ndoa, walioelimika na ambao wamewahi kupata watoto, sasa wanaongoza kwa viwango vya juu vya utoaji mimba kwa hiari nchini Kenya, kwa mujibu wa utafiti mpya.
Matokeo yaliyotolewa jana yanaonyesha kuwa karibu wanawake 800,000 walitoa mimba mwaka 2023.
Kati ya wanawake 2,022 walihojiwa, asilimia 58 walikuwa wameolewa, ambapo asilimia 32 walikuwa na watoto wawili au watatu.
Wanawake wa kati ya miaka 25-34 waliongoza, wakikanusha dhana kwamba utoaji mimba ni suala la wasichana wachanga wasioolewa pekee.
Utafiti huo ulibaini kuwa wengi wa wanawake waliopokea huduma za baada ya utoaji mimba walikuwa na umri wa kati ya miaka 25-34 (asilimia 41.8), walio kwenye ndoa au wanaishi na wapenzi (asilimia 78.6), waliosoma hadi sekondari (asilimia37%) na Wakristo (asilimia 91).
Takriban asilimia 66 walikuwa wamewahi kuzaa hapo awali, huku asilimia 29 wakiwa wamewahi kupata zaidi ya mimba nne maishani.
Takriban asilimia 89.4 walitumia mbinu moja tu, huku dawa zikiongoza (asilimia 61.8). Mbinu za jadi zilitumiwa na asilimia 27 huku asilimia 12.2 wakitumia mbinu nyinginezo.
Utafiti huu uliofanywa kati ya Aprili 2023 na Mei 2024 na APHRC, NADC, na Guttmacher Institute ulionyesha kuwa jumla ya mimba zilizotolewa zilikuwa 792,694, sawa na utoaji mimba 57.3 kwa kila wanawake 1,000 walio na umri wa kuzaa (15-49).
Mkurugenzi Mkuu wa Afya, Dkt Patrick Amoth, alikiri kuwa utoaji mimba usio salama bado ni changamoto kubwa, huku akisema kuwa kuna uhaba wa takwimu za kitaifa kuhusu suala hili.
Alisisitiza uwekezaji wa serikali katika upangaji uzazi, mafunzo ya watoa huduma, na huduma bora za baada ya utoaji mimba.
Baada ya kujumlisha mimba zote zilizoavywa mimba wa hiari, kujifungua, na mimba zilizoharibika, utafiti ulikadiria kuwa jumla ya mimba 2,850,346 zilirekodiwa nchini Kenya mwaka 2023.