Makala

Wanawake wanavyojituma kuzimbua riziki kwenye matimbo hatari 

March 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA CHARLES ONGADI

UCHUMI ukiendelea kupanda kila uchao, Wakenya wengi wamejipata wakilemewa kukithi familia zao mahitaji muhimu ya kimsingi.

Katika kijiji cha Kashani wadi ya Bamburi katika eneoubunge la Kisauni, Mombasa, baadhi ya akina mama wameamua kujitosa katika kazi ngumu ya uchimbaji saruji.

Gange ya matimbo ikichukuliwa kama ya jinsia ya kiume pekee, wanawake hao wameamua kuzika dhana hiyo na kujituma kuzimbulia familia.

Bi Kadzo Kalama, mama wa watoto sita ambaye ni mkazi wa kijiji cha Guu Ng’ombe ni kati ya akina mama wanaorauka kila asubuhi kuchimba saruji katika timbo la Kashani kujipatia mkate wake wa kila siku.

“Bwanangu alikuwa akifanya kazi hotelini lakini alifutwa mwishoni mwa 2023 na vibarua vidogo vidogo anavyofanya kwa sasa haviwezi kukithi mahitaji ya familia yetu,” anasema Bi Kalama aliyeanza kazi ya uchimbaji saruji mapema mwaka huu, 2023.

Anaambia Taifa Leo Dijitali kwamba kwa siku hutia kibindoni kati ya Sh600 hadi Sh1, 200, kulingana na bidii.

Anaongeza kuwa wanalazimika kushirikiana kuchimba na kisha kubeba kutoka kwenye mahandaki hadi maeneo ambayo ya kupakia kwenye lori zinazosubiri nje.

Naye Sidi Charo, 56, mkazi wa Kashani anasema mshahara wa bwanake ambaye ni bawabu katika kampuni moja ya kutengeneza barabara ya Mombasa/Malindi hauwezi kukithi mahitaji yao kifamilia.

Kutokana na hali ngumu, Bi Charo anasema amelazimika kufanya kazi ya uchimbaji wa saruji ili kukimu familia riziki kutokana na hali ngumu ya maisha kwa sasa.

“Maisha ilivyo sasa huwezi kumtegemea bwana ni lazima ujikakamue kama mwanamke kwa kufanya kazi. Kazi hizi zinafanywa na wanaume pekee, lakini lisilo na budi hufanywa,” akasema Bi Charo.

Aidha, kulingana na Bi Racheal Mumba alilaziika kufunga biashara yake ya kuuza mboga na matunda kutokana na biashara kudorora.

Bi Mumbai ambaye ni mjane, anasema biashara yake ilianza kudorora mwaka jana, 2023, baada ya baadhi ya wateja wake kupoteza ajira hivyo kuishia kumkopa jambo lililomlazimisha kufunga biashara hiyo.

Kulingana na Cosmas Kalama ambaye ni mzee wa mtaa wa kijiji cha Kashani, hali ngumu ya maisha imewalazimisha kina mama kujitosa katika kazi ngumu ya uchimbaji saruji ambayo kwa muda mrefu imeishi kufanywa na wanaume.

“Baadhi ya akina mama ni hawana bwana wala pa kutegemea, ila kazi hiyo ya kuchimba saruji kujipatia mkate wao wa kila siku,” akasema Bw Kalama.

Bw Kalama anasema kwamba majukumu magumu ya ulezi na hali ngumu ya kiuchumi imelazimisha kina mama hao kujitosa katika uchimbaji wa saruji.

Khadija Omar, 43, aliyeingilia kazi hiyo mwaka mmoja uliopita anasema aliamua kuwacha biashara ya uchangudoa eneo la Mtwapa, Kaunti ya Kilifi kutokana na hatari iliyopo kazini na hali ngumu ya kimaisha.

“Niliolewa, ila ndoa haikufanikiwa nikajiingiza katika biashara ya mahaba eneo la Mtwapa ili kulea wana wangu. Lakini baada ya kutafakari kwa kina kuhusu hatua hiyo, niliamua kufanya kazi halali,” akasema Bi Khadija.

Oktoba 2023 vijana wanne waliokuwa wakichimba saruji katika timbo la Kashani walipoteza maisha yao, kufuatia maporomoko.

Gavana wa Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir aliamuru kufungwa mara moja kwa timbo hilo hatari.

Lakini kulingana na Kalama Kadenge, limekuwa kitega uchumi kwa wengi eneo hilo baada ya hoteli nyingi za kitalii na kampuni kaunti za Mombasa na Kilifi kupunguza wafanyikazi wao.

Uamuzi huo ulichochewa na kuendelea kupanda kwa uchumi.