Wanawake wasiojua kuendesha baiskeli hatarini kukosa waume
NA KALUME KAZUNGU
MPEKETONI ni miongoni mwa miji muhimu ipatikanayo katika eneobunge la Lamu Magharibi.
Mji huo ni ngome kuu ya jamii ya Wakikuyu na unatambulika kwa kuzalisha chakula kupitia ukulima, hivyo kulisha na kutosheleza kaunti nzima ya Lamu.
Endapo wewe ni mwanamke na unaishi mjini Mpeketoni, utalazimika kujifunza kuendesha baiskeli mapema na kubobea kwani ujuzi huo ni muhimu sana.
Hata baadhi ya wanajamii waliozungumza na Taifa Leo walisema mwanamke anayejua kuendesha baiskeli katika eneo hilo, huwa rahisi yeye kupata mume wa kumuoa kwa sababu ya tija zinazokuja na ujuzi wa aina hiyo.
Kwa mujibu wa wazee wa jamii ya Mpeketoni, wanaume wengi wa eneo hilo miaka ya sasa wamekuwa waking’ang’ania kuwachumbia na hata kuwaoa wanawake wenye ujuzi wa kuendesha baiskeli.
Mzee wa Mpeketoni, Bw Alexander Mutua, anataja eneo hilo kuwa la maendeleo na kwamba lazima kila mtu ajitume vilivyo, ima awe ni mwanamume au mwanamke.
Alikiri kwamba wanaume wa Mpeketoni wamekuwa wakiwachuza akina dada wasiowajibika, hasa wale ambao kamwe hawana ufahamu wowote kuhusu jinsi baiskeli inavyoendeshwa.
Bw Mutua anafafanua kuwa jamii ya Mpeketoni imeipokea mia fil mia sifa ya wanawake kujua kuendesha baiskeli.
“Ndio sababu ukifika hapa utapata wasichana kwa akina mama, wadogo kwa wakubwa, wakiendesha baiskeli bila kujali. Hata sisi wanaume hapa huwa tuko mbio kabisa kuoa mke mwenye ujuzi wa kuendesha baiskeli. Hilo linamtambulisha mwanamke husika kuwa mtu wa kujituma, asiye mvivu na mwajibikaji. Ina maana mke ukiwa hujui kuendesha baiskeli, basi kupata wa kukuoa hapa inakuwa ngumu,” akasema Bw Mutua.
Naye Bw Emmanuel Kimwa, mmoja wa wazee na viongozi wa jamii ya Mpeketoni, alisema wanaume wengi mara nyingi hupenda kuingia kwenye mahusiano na wanawake ambao sio wenye kumtegemea mwanamume husika katika kila jambo.
Kulingana na Bw Kimwa, wanawake wenye ujuzi wa kuendesha baiskeli wanadhihirisha wazi kuwa watu wa bidi, wenye maono ya mbali na wanaoweza kuishi kwenye mazingira yoyote yale kwa kujitegemea.
Anasema imekuwa mtindo kwa wanaume wengi mjini Mpeketoni kuwakimbilia hao akina dada wenye ujuzi wa kuendesha baiskeli, pikipiki na hata magari kwani hilo litamaanisha sio lazima huyo mwanamume awe nyumbani ndipo vyombo hivyo vya usafiri vitumike.
“Kama bibi yako anajua kuendesha baiskeli, pikipiki au gari, wewe tunakuhesabu kuwa mwanamume mwenye bahati ya mtende hapa Mpeketoni. Akina dada wenye ujuzi huo twawaona kuwa watu wa maono ambao wanaweza kuendeleza boma vyema. Ina maanisha mama anaweza kujituma huku na bwana upande ule mwingine na mwisho wa siku mnaleta kitu kikubwa kwa meza na maisha yaendelee,” akasema Bw Kimwa.
Bi Nancy Wairimu,40, ambaye ni mama wa watoto watano, anasema yeye binafsi alijifunza kuendesha baiskeli akiwa na umri mdogo.
Bi Wairimu, ambaye bado huendesha baiskeli, anakubaliana na madai hayo ya wanaume wa Mpeketoni ya kuwakimbilia wanawake wenye ujuzi kupeleka baiskeli.
“Nakumbuka wakati nilipokuwa nikichumbiwa mume wangu, kwa wakati huo akiwa mchumba wangu, alifikia mahali akaniuliza ikiwa nilijua kuendesha baiskeli? Nilipoitikia ‘ndiyo’ hata alinipa baiskeli yake nijaribu na nikamdhihirishia hilo. Nilimuona amefurahia ajabu na hilo lilimfanya kuharakisha kunilipia mahari na kunichukua niwe wake wa milele,” akasema Bi Wairimu.
Bi Beatrice Kamau, kwa upande wake, anasema pia alishawahi kuulizwa swali hilo wakati akichumbiwa.
“Wakati huo nilijihisi kukwazika lakini baadaye nikagundua umuhimu wa kujua kuiendesha hii baiskeli. Leo hii mume wangu anaweza kuwa mgonjwa tukiwa mashambani na mimi humbeba kwa baiskeli kumpeleka hospitalini. Isitoshe, hizi baiskeli ndizo zinatusaidia sisi akina mama kuwapeleka watoto wetu wachanga kliniki bila kumsubiri mwanamume atoke kazini ndipo atubebe kwa baiskeli kutupeleka hospitalini au kliniki,” akasema Bi Kamau.
Kwa akina dada, ama kwa kweli, itakulazimu uifahamu ndani na nje hii baiskeli, hasa kuiendesha, endapo ungetaka kuolewa haraka Mpeketoni.
Kwa wale wanaozaliwa na kukulia mjini humo, huu ndio wakati wa kujitambua na kuchanika mpinini mapema kuijua baiskeli kuanzia udogoni kabisa ili ufikapo umri wa utu uzima na kutaka kufunga nikaha, hawa madume wasiwe na vijisababu vya kukutelekeza au kukutema wanapotafuta wake wa kuoa.