Makala

WANDERI: Maovu yanayozuia Kenya kupiga hatua kimaendeleo

October 29th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

KWA wakati wote atakapoishi duniani, itakuwa vigumu sana kwa mwanadamu kusahau mchango aliotoa mwanaharakati Mahatma Ghandhi katika kusisitiza haja ya uwepo wa amani duniani.

Ghandhi alitoa kauli hiyo kwa kurejelea dhambi saba kuu ambazo jamii nyingi hujipata kama mateka wake.

Dhambi hizo alizitaja kuwa: Utajiri bila jasho, furaha bila uangalifu, ujuzi wa sayansi usiozingatia uanadamu, werevu bila maadili, siasa bila maadili, biashara isiyozingatia maadili na dini isiyozingatia kujitolea.

Cha kushangaza ni kuwa, Kenya ni ‘mateka’ wa dhambi hizo. Ni baadhi ya maovu ambayo yametufanya kutostawi kimaendeleo, kijamii na kimaadili. Tunaishi katika jamii ambapo kila mmoja anapigania nafasi yake bila kujali athari za vitendo vyake kwa mwenzake. Je, ‘dhambi’ hizo kuu zimetuathiri vipi?

Utajiri bila jasho: Tangu uhuru, Kenya iliegemea mfumo wa utawala wa kibepari, ambao ulitoa nafasi kwa viongozi kujitajirisha kwa kutumia njia wawezayo.

Katika enzi ya marais Mzee Jomo Kenyatta na marehemu Daniel Moi, mawaziri waliripotiwa kutumia kampuni zao kufanya biashara na idara mbalimbali za serikali, hali iliyowafanya watu wachache kuwa matajiri kupindukia. Mamilioni ya wananchi walibaki kama wakimbizi katika nchi yao wenyewe, licha ya kushiriki kwenye vita vya kupigania uhuru. Hali hiyo ni laana ambayo bado inatuandama hadi sasa.

Furaha bila uangalifu: Baada ya kupora mali ya umma, wengi huamua kuitumia watakavyo. Huwa hawajali hata kidogo. Ni kutokana na hali hii ya kutojali ambapo huwa tunasikia visa vya maafisa wa serikali kuu ama kaunti wakienda katika nchi za nje bila sababu yoyote. Wengine hata huripotiwa kuwaoa wanawake wengi, kusudi kuu likiwa ‘kutumia’ fedha hizo.

Ujuzi wa kisayansi usiojali ubinadamu: Visa hivi vimekuwa vikishuhudiwa katika hospitali mbalimbali. Katika karne hii, kuna moja ya kizazi ambacho kina ujuzi mkubwa za kisayansi kote duniani. Ujuzi wa kisayansi uliopo kwa sasa haujawahi kushuhudiwa hata kidogo katika nyakati zilizopita.

Licha ya maendeleo hayo, hali ya ukosefu wa maadili katika hospitali zetu ni ya kusikitisha. Migomo ya wauguzi na madaktari inashuhudiwa karibu kila siku, huku wakiwatelekeza wagonjwa. Wengine hata wamefariki wakiwa mikononi mwao!

Visa vya wizi wa mitihani vimejaa kila mahali—si katika shule za msingi, upili au hata vyuo vikuu. Ni kama saratani isiyoisha. Visa vya watu waliopata digrii feki vimekuwa kama sehemu ya maisha yetu!

Siasa bila maadili: Hii ndiyo saratani kuu inayotuandama nchini. Ni gonjwa ambalo limekosa tiba. Hapa nchini, siasa mbaya zimekuwa chemichemi ya karibu kila maovu yanayotukumba. Wanasiasa hufanya lolote kutimiza malengo yao: hata kuua!

Bila shaka, lazima tuondoe ‘dhambi’ hizi ili kuwa jamii inayojua mwelekeo wake. Tusipofanya hivyo, tutabaki kama mateka; mateka waliopofuka na wanaoyumba nyikani wasiojua waelekeako.

Lazima tujitakaze ili kubuni mazingira bora kwa vizazi vijavyo.

[email protected]