WANGARI: Huduma nyumbani suluhu kwa maambukizi ya corona
Na MARY WANGARI
HIVI majuzi, serikali ilidokeza kwamba itaanza kuwaruhusu baadhi ya wale walioambukizwa virusi vya corona kuhudumiwa makwao.
Tangazo hilo lilipokelewa kwa hisia tofauti huku baadhi wakiunga mkono hatua hiyo lakini wengi wakaipinga kwa sababu zao kadhaa.
Hata hivyo, hatua hiyo huenda ikawa ndiyo suluhu pekee lililosalia, huku idadi ya maambukizi ikiongezeka kwa kasi katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita na kukaribia 7,000
Kulingana na takwimu za Wizara ya Afya, virusi vya corona kufikia sasa vimesambaa katika kaunti zaidi ya 40, huku Nairobi ikiongoza kwa idadi ya maambukizi na kufuatiwa na Kaunti za Mombasa na Busia mtawalia.
Aidha, vituo vya umma vya kutengea wagonjwa ni 113 vikiwa na nafasi ya vitanda 3,800 pekee vya wahasiriwa wa Covid-19.
Ikizingatiwa kuwa si kaunti zote zilizo na vituo vya kutengea wagonjwa, inamaanisha wagonjwa watalazimika kuhamishwa katika kaunti zilizo na vituo hivyo muhimu, katika juhudi za kudhibiti maambukizi zaidi.
Hali hii imesababisha misongamano mikubwa ya wagonjwa katika vituo vichache vilivyopo nchini kama vile kituo cha kutengea wagonjwa cha Hospitali Kuu ya Kenyatta (KNH), cha Mbagathi pamoja na Hospitali ya Rufaa na Utafiti ya Chuo Kikuu cha Kenyatta.
Bila shaka, huku idadi ya maambukizi ikizidi kuongezeka kila uchao, vituo hivyo vimefurika wagonjwa na ni dhahiri kuwa, havitaweza tena kumudu wahasiriwa wengine na kuwapa huduma bora inayohitajika.
Ingawa serikali za kaunti zinajikakamua kutekeleza agizo la Rais Uhuru Kenyatta ambapo aliamrisha kila kaunti kuwa na angalau vitanda 300 vya kutengea wagonjwa, ni bayana vitanda hivyo bado havitoshi kukabiliana na idadi ya wagonjwa wa Covid-19 nchini.
Hivyo basi, Maelezo kuhusu Huduma ya Kutengea wagonjwa Nyumbani yaliyozinduliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), Wizara ya Afya pamoja na wadau wengineo wa afya nchini, yamejiri wakati ufaao. Maelekezo hayo yatasaidia pakubwa kukabiliana na idadi ya maambukizi ya virusi hivyo.
Isitoshe, kanuni hizo zilizoorodheshwa zitawezesha wagonjwa kuhudumiwa nyumbani na jamaa na wapendwa wao mradi maagizo hayo yanafuatwa ipasavyo.
Muhimu ni kwamba, utekelezaji wa huduma hiyo utafanywa chini ya uangalizi wa maafisa wa afya huku serikali ikitenga vituo maalumu vya kuwatunzia wagonjwa katika maeneo ya vitongoji duni.
Utafiti umedihirisha kwamba, asilimia 80 ya walioambukizwa virusi vya corona huwa hawaonyeshi dalili zozote au wanaonyesha dalili chache tu.
Kwa kuzingatia hayo, ni bayana kuwa wakati umewadia kwa Wakenya kukumbatia huduma ya nyumbani kwa wagonjwa wa Covid-19.
Wasiliana na mwandishi kupitia: [email protected]