WANGARI: Idara ya Mahakama ifanikishe miradi ya Maraga akistaafu
Na MARY WANGARI
MWISHONI mwa wiki iliyopita, Jaji Mkuu David Maraga alitoa hotuba yake ya mwisho kuhusu Ripoti ya Hali ya Idara ya Mahakama na Usimamizi wa Haki, huku akijiandaa kustaafu mnamo Januari 12, 2021.
Katika ripoti hiyo, Bw Maraga alielezea kuhusu kibarua kigumu alichokabiliwa nacho cha kuhakikisha kwamba Idara ya Mahakama inasalia kitengo huru kinachoweza kutegemewa kulinda na kuhifadhi haki.
Aidha, alitaja miradi kadhaa aliyofanikisha ikiwemo kupunguza mrundikano wa kesi upesi, kuanzisha miradi 61 ya ujenzi wa mahakama katika sehemu mbalimbali nchini, kufanikisha upeo mpana wa mahakama na hata kubuniwa kwa miundomsingi imara wa teknolojia ya habari na mawasiliano katika utendakazi wa Idara ya Mahakama.
Ukweli ni kwamba, Wakenya watamkumbuka Bw Maraga kwa muda mrefu hasa kama jaji aliyeingia katika vitabu vya kihistoria nchini kwa kufutilia mbali uchaguzi wa urais mnamo 2017, na kusababisha uchaguzi huo kurudiwa tena.
Hali kwamba jaji huyo alifanikiwa kurejesha imani ya umma kwa Idara ya Mahakama ni ya kutia moyo sana ikizingatiwa kuwa alichukua usukani wakati ambapo idara hiyo ilionekana kama kibaraka wa serikali.
Ukakamavu wake katika kulinda sheria kwa dhati utasalia katika kumbukumbu za wengi hasa alipomkashifu Rais Uhuru Kenyatta kuhusiana na uteuzi wa majaji 41 na bila kusahau hivi majuzi alipoibua hisia kali kwa kupendekeza kuvunjwa kwa Bunge la Kitaifa kuhusiana na sheria ya usawa wa kijinsia.
Ni dhahiri kwamba msimamo wake imara kuhusiana na udumishaji wa haki na sheria umeifanya Idara ya Mahakama kupiga hatua katika mweleko chanya na kuboresha taswira ya idara hiyo nchini.
Hata hivyo, uhalisia ambao huwezi ukapuuzwa ni kuwa safari ya uhuru wa Idara ya Mahakama bado ni ndefu na yenye misukosuko chungu nzima hali ambayo bila shaka ilionekana kumtamausha Bw Maraga kiasi cha kumfanya kulalama kila alipopata fursa.
Kuanzia kutatizwa na kuingiliwa kwa uhuru wa Idara ya Mahakama, idara hiyo kukosa kuruhusiwa kujisimamia kifedha, hadi ukiukaji wa amri za mahakama kutoka kwa vyombo vya dola, ni baadhi ya vizingiti vikuu vinavyotishia kulemaza tawi hilo muhimu la serikali.
Huku Bw Maraga akielekea kustaafu na kuacha pengo kabla ya jaji mpya kuchukua usukani, ni sharti Idara ya Mahakama ifanikishe mageuzi muhimu ili kulinda nafasi yake kama nguzo ya haki.
Nyanja mojawapo ni kwa kujumuisha kikamilifu teknolojia katika utoaji huduma wa Idara ya Mahakama ili kuboresha utendakazi wake.
Litakuwa ni jambo la kusikitisha mno endapo idara hiyo italegeza kamba na kuhujumu hatua zilizopigwa hadi kufikia sasa kuhusiana na uhuru wa mfumo wa haki nchini.