WANGARI: Kenya isiwe na pupa ya mkataba na Amerika
Na MARY WANGARI
MAPEMA Julai, Kenya na Amerika zilizindua rasmi mazungumzo kuhusu Mkataba Huru wa Biashara (FTA).
Mkataba huo ambao utakuwa wa kwanza wa aina yake barani Afrika, unafuatia jopokazi lililobuniwa mwaka jana mnamo Agosti, kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya mataifa haya mawili.
Kenya na bara la Afrika kwa jumla inatazamiwa kunufaika pakubwa kutokana na FTA, kwani Kenya ikitumai kupenya kirahisi katika soko la Amerika, huku mataifa mengine ya Afrika yakipata jukwaa thabiti la biashara kimataifa.
Mkataba huo pia utawezesha kubuniwa kwa sera zitakazofanikisha usafirishaji huru wa bidhaa na huduma, hivyo kupiga jeki shughuli za kibiashara kati ya mataifa wanachama.
Hii ni ishara tosha kuhusu ukuaji wa soko la Kenya kimataifa hali inayotarajiwa kubuni nafasi tele za ajira, maendeleo kiuchumi, kiteknolojia na ubunifu.
Chini ya mkataba huo, Kenya haitakuwa na budi ila kuimarisha viwango vya ubora vya bidhaa zake na wakati huo huo, kutoa nafasi kwa wawekezaji wapya humu nchini.
Hatua hii imejiri wakati ufaao huku takwimu zikionyesha kuwa Kenya inaongoza barani Afrika kwa uuzaji wa bidhaa za mavazi Amerika.
Ni bayana kuwa, kwa kutilia maanani sekta ya nguo, Kenya inaweza kubuni nafasi zaidi za ajira.
Hata hivyo, japo manufaa ya mkataba huo ni tele, ni muhimu kwa Kenya kumakinika kuhusu athari zinazoambatana na FTA.
Suala la soko huru kati ya Kenya na Amerika linazua changamoto nyingi hasa ikizingatiwa aina ya bidhaa, viwango, uwezo, na gharama ya uzalishaji kati ya mataifa hayo mawili.
Kenya, sawa na mataifa jirani, inategemea pakubwa bidhaa za kilimo inazouza katika soko la Amerika.
Hii ni tofauti na Amerika iliyo na upeo mpana wa bidhaa ambazo kupitia FTA zitauzwa nchini na katika soko la Afrika Mashariki, hivyo kumaanisha taifa hilo litanufaika zaidi.
Pia kuna tishio la mkataba mpya kati ya Kenya na Amerika kuhujumu uhusiano wa kibiashara kati ya Kenya na mataifa mengine Afrika, ikikumbukwa kuwa Kenya tayari ni mwanachama wa Mkataba wa Soko Huru Barani Afrika.
Hatuwezi kupuuza suala la ushindani usio wa haki kati ya wakulima wenye uwezo mkubwa kifedha na raslimali kutoka Amerika na wakulima wanaotaabika humu nchini.
Kwa vyovyote vile, huku Kenya ikijiandaa kujiunga na Amerika katika mkataba huo muhimu, ni sharti iwe makini kwa kuwa FTA huenda ikajenga au kubomoa kulingana na itakavyotumika.