• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
WANGARI: Mikakati ibuniwe kuimarisha huduma za bodaboda

WANGARI: Mikakati ibuniwe kuimarisha huduma za bodaboda

Na MARY WANGARI

HIVI majuzi, waendeshaji bodaboda kutoka eneobunge la Lari, Kaunti ya Kiambu, waliandaa ibada ya maombi kuhusiana na ongezeko la vifo vya waendeshaji bodaboda eneo hilo.

Haya yalijiri huku uchukuzi kwa kutumia pikipiki ukizidi kupata umaarufu nchini kutokana na ufaafu wake katika mazingira na hali mbalimbali.

Kando na kurahisisha usafirishaji, tasnia hiyo imegeuka kitega uchumi kwa mamia ya familia ambazo sasa zinaweza kupata mkate wa kila siku.

Idadi ya bodaboda imeongezeka kwa kasi nchini hadi zaidi ya milioni mbili kufikia Mei mwaka huu kulingana na takwimu, hali ambayo imechangiwa na hatua ya serikali ya kufutilia mbali ushuru kwa pikipiki zote zenye kiwango cha chini ya 250cc, katika juhudi za kuvutia vijana kusaka ajira.

Licha ya ufanisi huo kiuchumi, inatatiza mno kuwa sekta hiyo inazidi kuendelezwa bila sheria na sera thabiti huku wasimamizi waliotwikwa jukumu la kuiangazia wakizidi kuwa walegevu.

Hali imezidi kuvurugika ikizingatiwa kuwa idadi kubwa ya wanaojihusisha na biashara hiyo ni vijana machachari wengi wao wakiwa na kiwango cha chini cha elimu au hata mahafala wa vyuo vikuu waliokata tamaa baada ya kukosa ajira.

Matokeo yake ni vifo na ulemavu ambao kutokana na uendeshaji bodaboda kiholela hali ambazo zinaweza kuepukika.

Waendeshaji bodaboda pia wamefahamika kukiuka kimaksudi sheria za trafiki, kupuuza mikondo iliyotengewa abiria barabarani na hata kuchukua sheria mikononi mwao kwa kuzua ghasia ambazo aghalabu zimesababisha vifo vya raia wasio na hatia.

Katika juhudi za kupata pesa haraka, waendeshaji bodaboda wameishia kujifunza wao kwa wao huku baadhi wakidiriki kusafirisha bidhaa na mizigo hata kabla ya kuelewa vyema sheria za kimsingi kuhusu usalama wa barabarani.

Isitoshe, huku taifa likipambana na janga la Covid-19, inahofisha kuwa waendeshaji bodaboda ni miongoni mwa wanaopuuza sheria kuhusu Afya ya Umma ikiwemo kubeba abiria mmoja kwa wakati mmoja ili kudumisha umbali wa mita moja, kuvalia barakoa, kunawa mikono miongoni mwa mengine.

Bila shaka, sekta hiyo muhimu kama mbinu mbadala ya usafirishaji wa abiria na bidhaa, inakabiliwa na changamoto tele ambazo zinahitajika kusuluhishwa kwa dharura.

Mikakati madhubuti inahitajika kukomesha maovu yaliyokithiri katika sekta hiyo yanayotishia kuhujumu uchumi na usalama wa umma kwa jumla.

Mamlaka husika ni sharti itoe mafunzo kwa waendeshaji bodaboda ikiwemo uhamasishaji na vifaa vya kujikinga, ili kupunguza ajali na athari zake.

Ni muhimu kanuni kali na sera zibuniwe ili kukomesha ufisadi, uhuni matumizi ya mihadarati na uhalifu katika juhudi za kusafisha sekta hiyo ikiwemo bima ya afya kwa waendeshaji bodaboda na abiria wao.

You can share this post!

TAHARIRI: Takwimu zitumiwe kukomesha ajali

RIZIKI: Uyatima, hali ngumu ya maisha haikuzima ndoto yake...