WANGARI: Mzozo wa FKF, vyombo vya habari usuluhishwe upesi
Na MARY WANGARI
MNAMO Jumamosi iliyopita, wanahabari kadhaa walipigwa na butwaa walipofurushwa nje na polisi walipofika kuangazia mechi kati ya vilabu viwili maarufu vya kandanda nchini.
Hali kwamba kisa hicho kilitokea katika Sikukuu ya Jamhuri iliyoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta ilikuwa ni kinaya kikuu kilichovutia hisia kali kote nchini na kimataifa.
Ingawa kanuni za kudhibiti Covid-19 zilitumika kama kisingizio, kitendo hicho ni ithbati tosha kwamba uhasama kati ya Shirika la Kandanda Kenya (FKF) na vyombo vya habari nchini haukaribii kufika kikomo hivi karibuni.
Kitendo hicho cha kudhalilisha ambapo baadhi ya wanahabari walirushwa nje na maafisa wa polisi wakati wa mchuano kati ya Gor Mahia na Ulinzi Stars, kilisababisha vyombo vya habari anuai nchini kuafikiana kutoangazia mechi zozote za FKF.
Ikizingatiwa kwamba hii si mara ya kwanza shirika hilo linakwaruzana na vyombo vya habari nchini ikiwemo kuwanyima wanahabari vibali vya kuangazia shughuli zake mbalimbali, ni bayana kwamba uhasama huo ni sharti utatuliwe kwa dharura la sivyo utazua madhara zaidi.
Ni vyema ifahamike kwamba haijalishi iwapo FKF ina uhasama wa kibinafsi na baadhi ya wanahabari kwa sababu kilicho muhimu ni kwamba vyombo vya habari vina wajibu wa kufahamisha, kuangazia michuano mbalimbali, usimamizi na chaguzi za FKF na mengineyo kwa niaba ya umma.
Hii hasa ni kwa sababu timu za kitaifa pamoja na FKF hufadhiliwa na pesa za walipa ushuru hivyo basi wananchi wana kila haki ya kujua jinsi shirika hilo linavyoendesha shughuli zake, kwa niaba ya Wakenya.
Isitoshe, umma una haki ya kufurahia na kujiburudisha kwa kutazama ama kusoma kuhusu mechi kati ya vilabu wanavyounga mkono.
Ili kufanikisha haya yote, vyombo vya habari ni sharti viruhusiwe kutekeleza kikamilifu jukumu lake la kufahamisha, kuburudisha, kuangazia maovu katika jamii na kadhalika bila ubaguzi wala mapendeleo yoyote.
Hatua ya FKF kujitwika mamlaka ya kuamua ni wanahabari wapi wanaofaa au wasiofaa kuangazia michuano ya kandanda nchini pamoja na shughuli zake anuai ni sawa na kuingilia uhuru wa vyombo vya habari.
Mgogoro kati ya FKF na wanahabari nchini ni sharti ukomeshwe kwa dharura.
Badala ya kujipiga kifua na kupimana nguvu, wadau husika kutoka pande zote wanapaswa kuketi pamoja na kusuluhisha masuala yanayozua uhasama kati yao.