WANGARI: Serikali ichukue hatua kunusuru shule za kibinafsi
Na MARY WANGARI
KATIKA siku za hivi majuzi, kumekuwa na ripoti kuhusu shule nyingi za kibinafsi ambazo zimo katika hatari ya kufungwa huku sekta ya elimu ikigubikwa na wingu la sintofahamu.
Baadhi ya wazazi hata wameanza kupokea notisi za kuwataka kuwahamisha shule watoto wao.Wafanyikakazi katika taasisi za elimu za kibinafsi ndio walioathrika mno huku wakilazimika kukatwa mishahara yao, kwenda likizo bila malipo au hata kupoteza kazi zao.
Huku wakiachwa bila namna ya kujipatia riziki, walimu na waajiriwa wengine katika taasisi hizo wamejipata katika mashaka yasioambilika ikiwemo kufurushwa katika nyumba wanazopangisha kwa kukosa kodi na pia kukosa chakula.
Si ajabu kwamba, walimu wengi sasa wamegeukia vibarua vyovyote vile iwe ni kuchuuza barabarani au kutumia vipaji vyao, huku wanaokosa namna kabisa wakizama katika matatizo ya kisaikolojia.
Japo sekta nyinginezo zimeathirika vilevile, ni bayana kuwa walimu katika shule za kibinafsi wamehangaika pakubwa wakati huu.
Ripoti tayari zinaashiria uhalisia wa kutamausha kuhusiana na sekta hiyo ambapo shule za kibinafsi huenda zikafungwa kabisa hata baada ya shule kufunguliwa tena mwaka ujao.
Habari hizo ni za kuibua wasiwasi kwa kuwa inamaanisha hatima ya mamilioni ya wanafunzi katika taasisi hizo, inaning’inia hatarini.
Shule za kibinafsi zinatekeleza wajibu muhimu katika sekta ya elimu nchini ikizingatiwa kuna shule za kibinafsi zaidi ya 30,000 nchini.
Aidha, taasisi hizo kuanzia chekechea, shule za msingi na sekondari zimewaajiri wafanyakazi zaidi ya 200,000 kama walimu na wahudumu wengineo.
Inavunja moyo sana hivyo basi, kuona taasisi hizo zikifungwa baada ya kushindwa kumudu shughuli zake kwa kukosa mapato ya kujistawisha.
Ni dhahiri kuwa kusambaratika kwa taasisi hizo hakutaathiri tu maafisa wake bali pia sekta ya elimu kwa jumla.
Isitoshe, hali hiyo italemaza juhudi za serikali kuhakikisha watoto wote wanapata elimu kwa sababu wanafunzi wengi watakosa nafasi za shule, huku shule chache za kibinafsi zitakazosalia pamoja na shule za umma zikisakamwa na msongamano wa wanafunzi.
Ndiposa ninahimiza serikali na Wizara ya Elimu kufanya kila iwezalo kunusuru jahazi la shule za kibinafsi lisizame.
Ikiwa taasisi hizo za kibinafsi zitaendelea kufungwa, Serikali kupitia Wizara ya Elimu itakuwa imefeli na na bila shaka itajuta baadaye.
Huu ndio wakati mwafaka kwa serikali na wadau husika kutumia kila raslimali kuokoa hatima ya shule za kibinafsi.