WANGARI: Serikali itie bidii katika azimio lake jipya la kuokoa SMEs
Na MARY WANGARI
LICHA ya janga la Covid-19 linaloendelea kuzua balaa nchini na kimataifa, kuna mwanga wa matumaini kwa wamiliki biashara ndogondogo na zile za wastani (SMEs).
Hatua ya Rais Uhuru Kenyatta kuzindua mradi wa Sh3 bilioni ili kuwezesha SMEs kupata mtaji na mikopo ya kibiashara, ikifuatiwa na kuidhinishwa kwa mradi huo katika bajeti ya mwaka huu wa kifedha, ni afueni kuu kwa wawekezaji katika sekta hiyo.
Aidha, mashirika anuwai ya kifedha pia yamejitokeza kufadhili mradi huo unaolenga kunusuru SMEs zisizame wakati huu ambapo mifumo ya kiuchumi nchini inakabiliwa na wakati mgumu.
Tayari kitengo cha uwekezaji cha Shirika la Fedha Duniani (IMF) kimeongoza kwa kumimina kiasi cha Sh535 milioni katika Benki ya Afrika (BoA) tawi la Kenya, kwa madhumuni ya kutoa mikopo kwa SMEs.
Kubuniwa kwa mradi wa hakikisho la mikopo kumewaondolea wamiliki wa SMEs kikwazo kikubwa ambacho aghalabu hutumiwa na mashirika ya kifedha kuwanyima mikopo waendeshaji biashara.
Hizi ni habari njema kwa sekta hiyo ambayo kwa hakika imeathirika zaidi kutokana na kupungua pakubwa kwa mapato hivyo kukosa uwezo wa kuendeleza shughuli zake.
Si ajabu kuwa Benki Kuu ya Kenya (CBK) ilikuwa imeashiria kwamba asilimia 75 ya SMEs, ambayo ni sawa na biashara nane kwa kila 10, zinakabiliwa na tishio la kufungwa mwishoni mwa Juni.
Hata hivyo, mradi huo utafanikiwa tu kusadia SME ikiwemo sekta ya Jua Kali, iwapo serikali itaharakisha utekelezaji wake hasa kuhusiana na mashirika ya kifedha
Kutokana na mifumo dhaifu ya kifedha, SMEs zimeathirika zaidi ikilinganishwa na mashirika makubwa kutokana na upungufu wa mapato.
Licha ya serikali kuzindua miradi hiyo, ni dhahiri kuwa mikakati ya kifedha pekee haitoshi kunusuru SME.
Wamiliki wengi wa MSME wamelazimika kufunga biashara zao huku wengine wakielekea kufunga baada ya kulemewa na majukumu ya mishahara ya waajiriwa wao pamoja na malipo ya kodi kwa majengo yao ya kibiashara.
Mchakato mrefu unaohitajika ili kupata mikopo hiyo pia haufanyi hali kuwa rahisi kwa wafanyabiashara hao.
Hii ni kwa sababu wanahitajika kuandikia benki na mashirika ya kifedha wakifafanua ni kwa nini wanahitaji mikopo hiyo na hata baada ya kufanya hivyo, wanalazimika kusubiri kwa kipindi fulani huku ombi lao likitathminiwa.
Bila shaka, masharti hayo ni changamoto kuu ikizingatiwa kuwa idadi kubwa ya waendeshaji SMEs wana kiwango kidogo cha elimu au hata hawana kisomo kabisa.
Ni sharti serikali na wadau husika wamaanishe katika nia yao ya kuimarisha sekta ya SME nchini kwa kuhakikisha utekelezaji bora wa sera zilizobuniwa.