WANGARI: Utunzi wa miundomsingi utapiga jeki maendeleo
NA MARY WANGARI
HIVI majuzi, Mamlaka ya Utoaji Huduma jijini Nairobi (NMS) ilizindua mradi wa kurembesha jiji kuu la Nairobi huku ikiwaataka wamiliki majengo jijini kuyapaka rangi.
Mchakato huo wa kuboresha miundomsingi unaashiria nyakati njema zijazo katika ustawishaji na ukuaji wa uchumi, ikizingatiwa kuwa Nairobi ni kituo muhimu sio nchini tu bali barani Afrika kwa jumla.
Kwa muda mrefu, suala la uzoaji taka na majitaka limekuwa kero kuu ambalo limewahangaisha wakazi, licha ya Kipengele cha Nne katika Katiba kuorodhesha maji na usafi kama jukumu la serikali ya kaunti.
Kitendo ya kuimarisha miundo msingi muhimu jijini imejiri wakati ufaao hasa ikizingatiwa nafasi ya jiji la Nairobi katika ustawishaji wa maendeleo, utawala na hata usalama nchini.
Miundomsingi inajumuisha mambo kadhaa kama vile huduma za maji, hospitali, shule, barabara kuu, madaraja, viwanda vya kuzalisha na kusambaza umeme, mitandao ya mawasiliano, viwanja vya ndege, bandari, majengo ya serikali na kadhalika.
Kwa jumla, miundomsingi hiyo pia inaweza kufafanuliwa kama raslimali ya kitaifa ambayo inaweza kutatiza utoaji huduma wa kawaida katika taifa, endapo itaharibiwa au kukumbwa na hitilafu.
Ni kwa sababu hii, ambapo kila serikali ina jukumu la kulinda na kuhifadhi raslimali muhimu kutokana na uharibifu unaosababishwa na majanga ya kimaumbile kama vile mabadiliko ya hali ya anga, mitetemeko na maporomoko ya ardhi.
Miundomsingi ambayo ni viambajengo muhimu katika maendeleo nchini pia inaweza kuathiriwa na vitendo vya binadamu kwa mfano kupitia wizi, uharibifu, vita, vurugu na mengineyo.
Kando na hayo, miundomsingi vilevile inaweza kuchakaa kutokana na mpito wa wakati na matumizi, na ndiposa inapaswa kufanyiwa marekebisho na kuboreshwa mara kwa mara ikiwemo kubadilishiwa usimamizi wake.
Kitendo cha uboreshaji na uhifadhi wa miundomsingi si muhimu tu katika kiwango cha kitaifa bali mchakato huo pia unatambuliwa kimataifa.Taasisi ya Ulinzi wa Miundomsingi Muhimu (CIP) hujishughulisha na kuangazia mikakati iliyobuniwa na taifa husika kwa madhumuni ya kulinda raslimali muhimu.
Huku takwimu zikionyesha kuwa Kenya hupoteza kiasi cha zaidi ya Sh2 bilioni kila mwaka kutokana na uharibifu na kudorora kwa miundomsingi muhimu, ni dhahiri kuwa wakati umewadia kwa serikali kutilia maanani zaidi suala la kuboresha, kuhifadhi na kustawisha miundomsingi.