Makala

Wanne jela miaka 135 kwa kuua wanawake wakongwe kwa tuhuma za uchawi

Na WYCLIFFE NYABERI January 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WANAUME wanne, miongoni mwao baba na mwanawe wamehukumiwa kifungo cha jumla cha miaka 135 jela baada ya kupatikana na hatia ya kuwaua ajuza wanne katika eneo la Marani kaunti ya Kisii kwa tuhuma za uchawi.

Amos Nyakundi Ondieki almaarufu Sonko, Evans Ogeto Okari na Hesborn Ong’ondi Gichana sasa watatumikia kifungo cha miaka 40 kila mmoja huku Chrispine Makworo- mwanawe Bw Ondieki, akitumikia kifungo cha miaka 15.

Akitoa hukumu kwa njia ya mtandao mnamo Jumatano, Januari 22,2025, Hakimu Waweru Kiarie alisema Bw Makworo alipokea adhabu ndogo kwa kuwa hakuwa amehitimisha umri wa miaka 18 akitekeleza kosa hilo.

“Mshtakiwa wa pili (Chrispine Makworo) anahukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 15 jela kwa kuwa ilibainika kuwa alikuwa hajafikisha umri wa miaka 18 alipotenda kosa hilo,” Hakimu Kiarie alisema.

Wanne hao walipatikana na hatia ya kuwaua Jemima Miranga, 60,

, 57, Sigara Onkware, 62, na Sindege Mayaka, 85 mnamo Oktoba 2021. Kina nyanya hao walishukiwa kumroga mwanafunzi wa kidato cha nne kwa kumfanya bubu.

Walichukuliwa kutoka kwenye nyumba zao na umati ambao ulivamia nyumba zao moja baada ya nyingine.

Wakiwa wamejihami na mapanga, majembe, mashoka na marungu, wavamizi waliokuwa na hasira kali waliwaburuta hadi uwanjani ambapo waliwateketezea kijijini Nyagonyi.

Wahasiriwa na watu wa familia zao walijaribu kuwasihi wanaume hao wasiwaue wanawake hao lakini washambuliaji hao wawakusikiza chochote.

Mmoja wa kina nyanya hao, Sindege Mayaka alijaribu hata kuwapa washambuliaji pesa taslimu ili wamsamehe lakini juhudi zake zote ziliambulia patupu.

Kulingana na watoto wake, washambuliaji hao walichukua pesa hizo, ambazo nyanya huyo alikuwa amezipata baada ya kuuza ng’ombe wake ili zimsaidie kuenda hospitalini na wakazigawa miongoni mwao.

Walimpiga sana, wakamunyunyuzia petroli na kisha wakamwasha moto mkubwa uliomwangamiza.

Alipowapata wanne hao na hatia mwezi Disemba mwaka jana, Hakimu Kiarie alitaja shambulio dhidi ya ajuza hao kama la kinyama na kuongeza kuwa hakuna binadamu yeyote anayestahili kutendewa ukatili huo.

Jaji Kiarie alisema alishawishika pasipo shaka kuwa wanne hao walihusika katika mauaji hayo kulingana na ushahidi uliotolewa mahakamani.

“Wakati watu wawili au zaidi wanapokuwa na nia ya pamoja ya kufanya kusudi lisilo halali kwa kushirikiana, kila mmoja wao anachukuliwa kuwa anatenda kosa hilo,” Jaji Kiarie alisema alipokuwa akirejelea kifungu cha 21 cha Kanuni ya Adhabu.

Washukiwa 16 walifikishwa mahakamani kuhusiana na mauaji hayo lakini 12 hawakupatikana na hatia.

Uamuzi wa mahakama unapatia familia zilizoathiriwa matumaini kwamba haki hatimaye imepatikana kufuatia mauaji ya kutisha ya wapendwa wao.

Christopher Mayaka, mmoja wa watoto wa marehemu Sindege Mayaka, alikaribisha hukumu ya Jaji Kiarie na kusema hatimaye roho ya mama yake itapumzika kwa amani.

“Tumeridhika na hukumu hiyo na tutafuata yale ambayo mahakama imetuambia. Nafsi ya mama yangu sasa inaweza kupumzika kwa amani,” Bw Mayaka alisema.