• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Wapangaji nyumba za Martha wafutiwa kodi ya Januari

Wapangaji nyumba za Martha wafutiwa kodi ya Januari

NA FRIDAH OKACHI

BAADHI ya wapangaji katika eneo la Ongata Rongai katika Kaunti ya Kajiado wameshusha pumzi baada ya mmliki wa nyumba kuwaondolea kodi ya Januari 2024, akiwataka kutumia pesa hizo kwa mahitaji ya wana wao.

Hiyo ni zawadi muhimu kutoka kwa landiledi Martha Wanjiru.

Wapangaji hao walio na kazi za kudumu, wasio na kazi kwa maana ya wanaotegemea vibarua, na wanafunzi, walifurahishwa na hatua ya mmliki wa nyumba hizo ambaye hii si mara ya kwanza kufanya hivyo.

Wapangaji wengi kutoka Kaunti ya Kajiado huwa na wakati mgumu kulipa kodi ya nyumba mwanzoni mwa mwaka baada ya kutumia pesa kwenye matumizi mbalimbali yanayoambatana na msimu wa sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya.

Bi Wanjiru aliwaondolea kodi ya mwezi mmoja akisisitia kuwa kwa kipindi cha miezi kumi na mmoja, amekuwa akichukua kodi hiyo kwa wapangaji wake ambao walikuwa wakilipa bila kususia.

Mama huyo wa mtoto mmoja aliambia Taifa Jumapili kwamba hatua hii yake ni sawa na wema wa mwaka 2022 alipowafanyia wapangaji hao karamu ndipo akatambua changamoto ambazo wengi hupitia mwezi wa Januari.

“Baada ya kutoka ngambo, nilifungua biashara. Ujenzi ulikamilika miaka minane iliyopita lakini mpangaji mkongwe ni yule ameishi hapa miaka saba. Na sijawahi kupata ugumu ninapochukua kodi,” alisema Bi Wanjiru.

Mmiliki huyo alisema hatua hiyo ni kutokana na msaada kutoka kwa familia yake ambayo inaamini si lazima kuweka zingatio kwa kuvuna pesa tu bila kuwa na moyo wa huruma.

“Nimelelewa katika mazingira ya kufahamishwa kila mara kuhusu umuhimu wa kuwa na moyo wa huruma. Nataka kuondoa ile dhana kuwa wapangaji na wamiliki hawana uhusiano mwema,” akaeleza.

Mpangaji Naomi Oyieko alifurahia kuwa sasa hatalipa kodi ya nyumba mwezi Januari.

Mpangaji wa nyumba Bi Naomi Oyieko ambaye alimshukuru Bi Martha Wanjiru kwa moyo wa huruma kufuta kodi ya Januari 2024. PICHA | FRIDAH OKACHI

Alishukuru rafiki aliyemfahamisha kutafuta nyumba katika mtaa huo na haswa kwa landiledi huyo.

“Nimeishi hapa miaka minne sasa. Sijawahi kumuona mmiliki wa nyumba aliye na uta kama huyu. Wakati alitutolea kodi ya mwezi Januari, binafsi nilifurahi ajabu,” akasema Bi Oyieko.

Katika nyumba hizo za kumiliki huyo, kunaye mwanafunzi wa chuo kikuu, ambaye aliambia Taifa Jumapili kwamba alianza kuishi mtaa wa Tumaini katika nyumba ya chumba kimoja.

Lakini hali ni tofauti tangu alipohamia kwa nyumba zinazomilikiwa na Bi Wanjiru.

Wenzake wanampa shinikizo aandae sherehe kwa pesa ambazo angetumia kulipa kodi ya nyumba mwezi Januari.

“Nilihamia hapa Desemba na nilikuwa nimeishi siku 16 pekee. Marafiki wa karibu wanasema nina pesa. Wanataka tufanye sherehe kwa zile pesa ila nilitumia kwa shughuli fulani,” akasema mwanafunzi huyo aliyesema tu kwamba anaitwa Ruth.

Landiledi Martha Wanjiru (kushoto) akiwa na mmoja wa wapangaji. PICHA | FRIDAH OKACHI

Mwekezaji huyo amewataka wamiliki wengine Kaunti ya Kajiado na Nairobi kuwaelewa wapangaji wao licha ya kuchukua mkopo na kujenga nyumba hizo.

Mwaka 2022, mmiliki huyo wa nyumba aliwafanyia sherehe wapangaji hao, ila mwaka 2024 amepiga hatua moja mbele katika kutenda wema, akiwatolea kodi ya kila mwezi Januari pamoja na kuwapa bahasha za zawadi ya pesa kiasi fulani.

“Naomba muweze kutumia pesa hizi kwa shughuli na mahitaji ya watoto ila mfahamu hizi pesa si za pombe. Wale ambao hamna watoto mtafute watoto,” aliwatania wapangaji wake kwa video moja iliyopakiwa kwenye mtandao wa kijamii.

Kulingana na sensa ya mwaka 2019, Kaunti ya Nairobi ina wamiliki wa nyumba 1,354,882 na Kaunti ya Kajiado ikiwa na wamiliki wa nyumba 185,863.

Baadhi ya nyumba zinazomilikiwa na Bi Martha Wanjiru katika eneo la Ongata Rongai. PICHA | FRIDAH OKACHI
  • Tags

You can share this post!

Ukuzaji avokado wageuka hatari kwa sababu ya donge nono

Wakazi Mombasa kufaidi kupitia mradi wa treni

T L