• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 9:50 AM
Wapata riziki tosha kwa kusaga lishe za mifugo

Wapata riziki tosha kwa kusaga lishe za mifugo

Na PETER CHANGTOEK

NI siku ya Jumanne katika kitongoji cha Kithoka, katika Kaunti ya Meru, na sauti ya mashine ya kusaga lishe za mifugo yahanikiza kijijini.

Kundi la vijana linalojulikana kwa jina ‘Dairy Ventures Self Help Group’ ndilo linaloendesha shughuli pevu ya kutengeneza lishe kwa kusaga mabua ya mihindi mibichi katika eneo hilo.

Kundi lilo hilo, ambalo lilipewa mafunzo kuhusu shughuli hiyo na shirika moja kutoka Uholanzi, lilibuniwa mnamo mwaka 2014, na limekuwa la manufaa mno kwa wafugaji wa mifugo.

Ili kufanikisha shughuli hiyo, wanachama wa kundi hilo waliinunua mashine spesheli ya kusaga lishe kwa Sh340,000 mnamo mwaka 2018.

Walipolianzisha kundi hilo, kila mwanachama alitakiwa kutoa Sh1,000 kila mwezi, huku fedha hizo zikihifadhiwa katika shirika moja la mikopo nchini.

Baada ya kuinunua mashine hiyo, kundi hilo limekuwa likitembea kutoka kwa kaunti moja hadi nyingine, kwa madhumuni ya kutengeneza lishe kwa kusaga, huku wakilipwa kwa kazi hiyo, na hivyo kupata riziki kutokana na shughuli yenyewe.

Kwa kuitumia mashine iyo hiyo, vijana hao hutengeneza tani tatu za lishe kwa muda wa saa moja, na tani kumi za lishe kwa muda wa saa tatu.

Kwa kawaida, katika maeneo mengi, wakulima wamekuwa wakilipa Sh2,000 kwa wamiliki wa mashine hiyo, na Sh1,000 za ziada kwa kila kibarua anayepewa kazi hiyo kuitekeleza.

Kwa mwezi mmoja, vijana hao hupata takriban Sh250,000 kwa shughuli hiyo ya kutengeneza lishe za mifugo.

Mashine hiyo ni rahisi kutumia, na hutumia dizeli ili kutekeleza shughuli inayofaa kuitekeleza. Aidha, si nzito na hivyo kuibeba kutoka eneo moja hadi jingine ni rahisi.

MMOJA wa wanachama wa kundi la ‘Dairy Ventures Self Help Group’, akionyesha lishe walizozisaga kwa mashine spesheli. PICHA/ PETER CHANGTOEK

Kwa mujibu wa katibu wa kundi hilo, Stanley Murithi, ni kuwa mashine hiyo husaga sehemu zote za mimea ya foda, na hivyo basi ng’ombe hupata lishe ambazo zina virutubisho mwafaka, na hivyo kuboresha uzalishaji.

“Baada ya kusagwa kwa lishe, mkulima hubeba tu lori moja la lishe hizo, badala ya malori mawili hadi matatu ya foda ambazo hazijasagwa, na hivyo kupunguza gharama ya kusafirisha kwa Sh10,000 hadi Sh12,000 kwa safari moja,” aeleza Murithi.

Ili kuongeza fedha wanazozipata, vijana hao wamelikodi shamba ekari mbili, ambalo hulitumia kuikuza mihindi ambayo huitumia kutengeneza lishe na kuwauzia wakulima kwa Sh20,000-Sh30,000, kwa kutegemea misimu. Shughuli hiyo ya kuzitengeneza lishe imekuwa ikiwapa vijana hao riziki ya kutegemewa kila wakati.

Kundi hilo, kwa wakati huu, linaendeleza shughuli katika kaunti za Kirinyaga, Kajiado, Meru, Nakuru, Tharaka Nithi, Embu na Laikipia, huku likitoa huduma tofauti tofauti, kama vile; kuvuna mimea ya foda,

kukatakata foda, kuzitengeneza lishe aina ya silage, kuuza foda za mihindi kwa wakulima, na kuwajengea wakulima mabanda ya ng’ombe.

You can share this post!

Wakulima 1,000 waungana kutumia viazi vitamu kuoka mikate

Ashtakiwa kunyang’anya polisi simu