WARUI: Mtaala wa CBC bado kizungumkuti kwa walimu wengi
Na WANTO WARUI
Licha ya Wizara ya Elimu kutoa mwelekeo na mafunzo kuhusu mtaala mpya wa CBC kwa walimu, wengi wao wangali wanatatizika jinsi ya kuendeleza mafunzo hayo kwa wanafunzi.
Unapozuru shule nyingi katika madarasa ya gredi ya kwanza hadi ya nne, utagundua kuwa walimu wengi hawajui jinsi ya kukabiliana na mahitaji ya mtaala huo.
Kwa mfano, mtaala wa CBC unawahitaji wanafunzi watumie asilimia kubwa ya muda uliotengewa somo wakijifunza kwa vitendo wakiwa pamoja.
Hili linatatiza walimu pakubwa na wanatumia muda mwingi zaidi wakifafanua maswala ubaoni.
Changamoto nyingine ni ile ya kutathmini kazi ya kila mwanafunzi katika kila kipindi. Walimu wanashindwa kutekeleza hilo kwani muda ulioratibiwa kwa somo unaonekana mfupi kuliko mafunzo yanayohitajika kukamilishwa.
Masomo kama vile Muziki, Sanaa ya uchoraji, Somo la Kilimo ni mengine ambayo yanatoa changamoto nyingi kwa walimu kwani hawajazoea kuyafunza.
Aidha, mbinu ambazo zinapendekezwa kuyafunzia ni ngeni na walimu hawana uzoefu wa kutosha.
Isitoshe, mtaala huu ni ghali mno na unaegemea sana vifaa halisi vya kufunzia.
Walimu wanatatizika sana kupata vifaa vile halisi. Wazazi nao wanaona kama usumbufu kuambiwa wagharimie vifaa hivyo kila mara. Hili linawaacha walimu bila jingine la kufanya ila kutoa mafunzo yasiyoafiki kiwango kinachotarajiwa na mtaala.
Shule za mijini ambako hakuna mashamba zinakabiliwa na shida ya ufunzaji wa somo la Kilimo. Ingawa inamhitaji mwalimu kuwa mbunifu atengeneze vijishamba kupitia magunia au vifaa vingine, hili halitoshi kuwapa wanafunzi ule uzoefu wa kulimudu somo vizuri.
Silabasi ya Gredi ya Nne inawahitaji wanafunzi wafunzwe masomo kumi na matatu.
Wanafunzi hawa ni wadogo sana kiumri hivi kwambahawana uwezo wa kukabiliana na masomo haya yote kwa ghafla.
Inachukua walimu muda mwingi kuweza kuwasaidia wanafunzi kukabiliana na hali hii.
Isitoshe, kuna mzigo mkubwa sana kwa watoto hawa.
Pamoja na vitabu vingi ambavyo wanafunzi wanatakiwa kuwa navyo, kuna vifaa mbalimbali ambavyo pia huitishwa na walimu na inabidi wavibebe.
Walimu nao hawana budi kutafuta baadhi ya vifaa hivyo ili kufaulisha masomo darasani.
Ingawa mfumo huu wa elimu hauegemei sana mitihani, kuna shule, hasa za kibinafsi, ambazo zinajipata zikilazimishwa na wazazi kutoa matokeo ya mitihani, hasa ya mwisho wa muhula.
Walimu wanajipata wamechanganyikiwa pale ambapo wenye shule hizi wananunua mitihani hiyo ambayo haizingatii masomo haya.