Makala

Wasanii wacheshi wakwama mitandaoni kujikimu kimaisha

September 17th, 2020 3 min read

NA BENSON MATHEKA

Ni wazi kuwa wasanii aghalabu hupata pesa kwa kuwaburudisha watu. Lakini je, umewahi kuwaza ni vipi wasanii wacheshi (comedians) wanayakimu mahitaji yao wakati huu wa janga la Corona?  

Kutana na wacheshi wabunifu waliounda klabu ya ucheshi iitwayo 254 Quarantine Comedy Club ambao wanabobea katika kuwatumbuiza mashabiki wao mtandaoni.

Tangu kutolewa sheria kuzuia watu kukusanyika na kufungwa kwa maeneo ya burudani, wasanii hawa walianza kufanya shoo zao majumbani mwao na kuwatumbuiza mashabiki wao ndani na nje ya Kenya kupitia mtandao. Baada ya kundi lao kuvuma, walibadili na kuelekea hoteli ya Hill Park, ambapo huwa wanafanya shoo Live kila Ijumaa kuanzia saa nne usiku.

“Tuna wasanii zaidi ya thelathini, lakini kila Ijumaa huwa tunakutana saa saba hivi kufanya shoo ili kila mmoja aweze kupata fursa yake kwani hatuwezi kukongamana tukiwa wengi,” mwakilishi wa kundi hilo, msanii Obidan Daniel, alisema.

“Kati ya  wasanii watajika ambao wamewatumbuiza mashabiki hapo ni kama Sleepy David, Omwami, Captain Otoyo, Smart Joker, Jb Masandaku, Rib Crackers, Nasra, Adhis Jojo, Nyakundi, Mulamwa, Dj Kris Darlin, Doughty family, na Akuku Danger na wengine wengi. Isitoshe, pia tuna kundi shupavu la wasimamizi watajika wanaoandaa shoo zenyewe ikiwemo Victor Ber,” Obidan alisema.

Walipoanza, walikuwa na mashabiki wengi na wakaanza kufanya shoo zao kila siku kwa muda wa saa tano, lakini kutokana na gharama kubwa ya kuandaa shoo kila siku, walilazimika kufanya kwa siku moja kwa wiki. Wasanii hawa wamekuza tajriba zao sana mitandaoni sana ambapo kwa muda wa miezi miwili tu, wamepata zaidi ya wafuasi 14,000 kwa Facebook pekee.

Baada ya shoo zao, video zenyewe zinapatikana kwenye mtandao wa Facebook, na kuwawezesha mashabiki kufurahia hata ikiwa hawakupata fursa ya kuwatazama moja kwa moja mtandaoni.

Mwanzilishi wa kundi hili, Dorothy, ambaye huwa Marekani, pamoja na wahisani wengine ya mashirika ya TeleAfya na Twatwa ndio huwasimamia wasanii hawa kifedha ili kuwawezesha kufanya shoo zao. Mashabiki wao pia huwa wana fursa ya kutumia M-Pesa kuwafadhili wasanii hao.

“Baada ya shoo yenyewe, malipo hutoka Marekani. Mara yangu ya kwanza kulipwa na pesa za kigeni, nilipata furaha isiyo na kifani, karibu nichukue likizo ya kujistarehesha Mombasa.” Obidan anaelezea.

Wasanii hawa wana imani kuwa shoo yao itaendelea kunoga kutokana na Wakenya kukumbatia mifumo ya kidijitali kufanya mambo yao ya ila siku.

“Tunatumai kuwa shoo hii itaendelea hata baada ya janga la COVID-19. Kwa sasa, tayari imeanza kuonyeshwa katika stesheni ya EduTV, na hio ni hatua kubwa ya kutambulika kwetu, tangu tulipoanza kupitia mtandao wa Facebook Live miezi michache iliyopita na tunamshukuru Mungu.”

Kwa sasa, kundi hili halina ushindani kutoka kundi lingine lolote wakati huu. Pamoja na wacheshi, wasanii wengine wanaoshirikishwa katika shoo yenyewe ni waimbaji, maDJ, mashairi, maemcee na wengineo.

Kulingana na kundi hili, ni changamoto ambazo hufanya maisha yawe ya kuvutia, na ni katika kupambana  kushinda changamoto hizo ndipo maisha hupata maana. Kwao, changamoto kuu imekuwa ni sheria ya kudhibiti mkusanyiko wa watu, kwani ni vigumu kuwachekesha watu usiowaona.

Kwa sasa, hakuna usaidizi wa moja kwa moja wanaopata kutoka kwa serikali, lakini wangependa sana serikali kushughulikia swala la kuwasaidia wasanii ikiwemo kufadhili shoo zao, kutoa uhamasishaji na kuwapa kazi ili waweze kupata chakula cha kila siku wakati huu mgumu wa janga la Corona.

Kwa wale chipukizi ama wanaonuia kuingia fani hii, Obidan anawashauri wawe wabunifu, na watafiti ili waibuke na mambo ya kipekee.

“Buni mbinu   yako ya kujitambulisha, uwe thabiti na utumie mitandao ya kijamii na kuweka kazi yako hapo mara kwa mara. Utapata hisia tofauti, lakini kumbuka kuwa kitu muhimu ni kuwa washindi ni wale wasiokata tamaa maishani,” Obidan anashauri.

Obidan ni DJ mzoefu ambaye hapo awali alikuwa mwakilishi wa wanafunzi anayesimamia maswala ya burudani na michezo katika chuo kikuu cha Egerton. Baadaye, alianza kufanya ucheshi katika kundi ya Churchill, na kwa sasa ni mcheshi na mtaalamu wa mtandao.