Wasanii wahamasisha Wakenya wajikinge dhidi ya janga la Covid-19
Na ABDULRAHMAN SHERIFF
BAADHI ya waimbaji ni miongoni mwa Wakenya waliojitolea kueneza mawaidha ya kuwasihi wananchi wajikinge na janga la corona.
Wasanii wengine wanaendelea kutunga nyimbo za kuwapa pole wale waliopoteza jamaa zao na wale ambao wameambukizwa na ugonjwa wa Covid-19.
Kutoka eneo la Pwani, msanii wa Injili, Doris Owino amesema kuwa yuko karibu kuimba wimbo unaohusiana na maradhi hayo ya corona lakini anasubiri kuukamilisha ili aupe jina litakalolingana na wakati huo atakapokuwa anauzindua.
“Kwetu sisi waimbaji tuna umuhimu mkubwa wa kuhakikisha tuanajitosa kuimba nyimbo za kuwasihi Wakenya wajilinde na janga hili ambalo ni la kitaifa. Tunaimba kuwahamasisha wananchi wajichunge na kujiepusha yasiyotakikana kuyafanya wakati huu,” akasema Doris.
Naye mwanamuziki Dianah Dinah anasema wana wajibu mkubwa kuimba nyimbo za mada za ugonjwa wa Covid-19 kwa njia zote kuanzia kwa athari zake pamoja na kujikinga kuepuka maambukizi hasa kwa kuwa bado unazidi kusambaa hapa nchini.
“Tunawajibika kutuma jumbe kwa Wakenya wajihadhari na wafuate yale yanayohitajika kuzingatiwa wakati huu ugonjwa huu unazidi kutambaa na kuathiri familia kadhaa,” akasema Dinah.
Kwa mwimbaji Nassir Mohamed Abdalla almaarufu Brother Nassir, pengine tunaweza kusema ndiye msanii aliyekuwa mwepesi na wa kwanza kutoa kibao kilichozungumzia janga hilo la corona.
Kibao hicho kwa jina la ‘Corona’ na ambacho amekiimba kwa mahadhi yanayoiga wimbo wa Kihindi wa ‘Tere Naam’, Brother Nassir anawasihi watu wafuate maagizo yanayotolewa ya kuwaokoa wasikumbwe na janga hilo.
“Nyimbo yangu hii imeshabikiwa mno na wapenda muziki wa kihindi na ninamshukuru Mungu kwa kuiwezesha kuwavutia watu zaidi ya 42,000 katika YouTube, kiwango ambacho kinalingana na nyimbo zingine maarufu barani Afrika,” amesema Brother Nassir.
Kwake Brother Nassir, alifahamisha kuwa katika kibao chake hicho cha ‘Corona’, ameeleza kuwa corona imeanzia China na sasa iko dunia nzima hivyo akamuomba Mungu awaepushe na janga hilo lisiendelee kuwaadhibu.
“Nimemuomba Mungu atusamehe kwa maovu tunayotenda ya kumuasi yeye na kutuepushia janga hili la corona ambalo limeshapoteza maisha ya wengi. Nimemuomba Mungu atuhifadhi na kutuokoa lisiendelee kutuadhibu,” akasema.
Nassir kati ya wasia aliotoa katika nyimbo hiyo yake ni kuwaomba watu wawe wakiosha mikono kila mara na kutosahau kutumia sabuni.
Pia ubeti mmoja wa shairi la wimbo huo unasema: “Tusitoke tubaki karantini, tuswali Ilahi tumuogopeni, ya Mannani Rahamani, tusaidie ya Rabana!”.
Mwimbaji huyo anaamini kuwa amefikisha ujumbe huo muhimu kwa wale wanaopenda muziki na amefurahi kwa kuwa ujumbe wake umeanza kuenezwa kwenye magari ya matatu, tuktuk na majumbani.
“Tuko katika hatari ya janga la corona hivyo nimeona nina wajibu mkubwa wa kutuma ujumbe ambao nina hakika umewafikia wengi na utazidi kuwafikia wengine ili uweze kukabilika ipasavyo na utoweke na maisha yarudi kama yalivyokuwa hapo awali,” akasema Nassir.
Waimbaji wa Mombasa na sehemu nyingine za mwambao wa Pwani wamekuwa wakijiandaa kuimba nyimbo zinazohusiana na corona na wengi wao wamesema watakuwa wakitoa jumbe za kuwasihi wajikinge na kujiepusha na yale yasiyotakikana kufanywa wakati huu.
Waimbaji wengine wanaojitayarisha kuimba nyimbo zinazohusiana na corona ni pamoja na wale wa maeneo ya Kaunti za Kilifi, Taita Taveta na Kwale.
“Ninafanya mipango tukutane waimbaji kutoka sehemu mbalimbali za jimbo letu la Pwani, tutoe kibao kimoja kitakachozungumzia juu ya janga la corona, ugonjwa ulipofika hapa nchini, ulivyoathiri baadhi ya watu na nini twahitajika kufanya kuudhibiti,” amesema msanii ambaye hakutaka kutajwa jina.
Waimbaji wengine wamesema hawataki kutajwa mpaka pale watakapokamilisha nyimbo zao kuhusiana na janga hilo lililoathiri walimwengu wengi.