• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 9:55 AM
Washukiwa wa ulanguzi wa bangi wakamatwa

Washukiwa wa ulanguzi wa bangi wakamatwa

NA MWANGI MUIRURI 

MAAFISA wa polisi katika Kaunti ya Migori walilazimika kufyatua risasi juu ili kusimamisha gari lililokuwa na washukiwa wa ulanguzi wa dawa za kulevya.

Walilazimika kufanya hivyo baada ya dereva wa gari hilo kukaidi amri kusimama.

Badala yake, alitishia kukanyaga afisa aliyeamuru wasimame.

Katika kizazaa kilichozuka mwendo wa saa tatu asubuhi, Jumapili, Machi 17, 2024 washukiwa wawili walinaswa huku bangi inayokadiriwa kuwa na thamani ya Sh9 milioni ikitwaliwa.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi kutoka kwa kamati ya kiusalama ya Kaunti ya Migori, kituo cha polisi cha Isebania ndicho kinashughulikia washukiwa hao pamoja na shehena hiyo ya bangi.

Tukio hilo lilirekodiwa kama kisa nambari 08/17/03/2024 katika kitabu cha matukio cha stesheni ya Isebania.

Ripoti hiyo ilieleza kwamba gari lenye nambari za usajili KCL 532E, lenye muundo wa Toyota Prado lilishukiwa kwamba lilikuwa likiingiza bangi nchini Kenya kutoka Taifa jirani la Tanzania kupitia njia ya mkato ya Nyametaburo kupitia Isebania kuelekea Migori.

Maafisa wa kiusalama waliweka kizuizi katika daraja la Karamu, ambapo muda mfupi baadaye lilionekana likiwasongea likiwa kwa mwendo wa kasi.

“Badala ya kusimamisha gari kama alivyoagizwa, dereva wa gari hilo aliongeza mwendo akilielekeza kwa afisa wa polisi aliyekuwa kwenye kizuizi kwa nia wazi ya kutaka kumuua. Afisa mwingine alifyatua risasi tatu juu ili kuwatia kiwewe washukiwa hao,” ripoti hiyo inasema.

Ripoti hiyo inaongeza kwamba katika drama hiyo mshukiwa mmoja alitoroka kupitia dirisha la gari “lakini Daniel Okoth, dereva, na Erick Ombima akiwa abiria walitiwa mbaroni”.

“Baada ya upekuzi ndani ya gari hilo kulipatikana magunia sita ya bangi yakiwa na kilo 300 kwa ujumla, thamani ikiwa ni Sh9 milioni,” ripoti inaeleza.

Washukiwa hao watafikishwa kortini mnamo Jumatatu, Machi 18, 2024.

 

  • Tags

You can share this post!

Matapeli wanavyotumia watoto na walemavu kuvuna pesa

Tanzia mamake Askofu JJ Gitahi akiaga

T L