Makala

WASIA: Hakuna taaluma bora, ni mwanataaluma ndiye huwa bora au duni

October 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na HENRY MOKUA

KILA binadamu anapokumbwa na hali ngeni, hasa asiyoitarajia, hatua yake ya kwanza kwa kawaida huwa kukataa kwamba jambo hilo halikutukia.

Mathalani, mwanariadha ambaye amefanya mazoezi siku zote kwa kusudi la kushinda mbio fulani hukosa kuamini ameshinda hata baada ya kupewa tuzo aliyoitazamia.

Miongoni mwa masuala yanayoweza kuchangia hali hii ni ushindani mkubwa unaokuwepo.

Katika mashindano kuna wakati unawazia hata kumwachia mwenzio taji kabla ya mashindano yenyewe kwa kuona alivyojiandaa kukupiku.

Hata hivyo, unapomwomba Mungu wako ukajitosa uwanjani na kukabiliana na mtu yule yule uliyemhofia hadi ukamshinda, inakuchukua muda kuamini kwamba umemshinda kweli.

Matokeo ya mitihani hayawi tofauti sana na mashindano mengine kwa jumla isipokuwa kimsingi kwamba kwayo, aghalabu huwakatiza tamaa watahiniwa kuliko kuwaridhisha.

Isitoshe, watahiniwa hawaamini mara moja kwamba watafanya kozi zinazochukuana na matokeo hayo yasiyowaridhisha.

Wengine hushikilia kuwa watafanya kozi zile zile za ndoto zao. Hufanya kosa jingine la kutuma maombi ya kusajiliwa katika kozi wasizofuzu kujiunga nazo hivyo kuachwa nje. Inapofanyika hivi, husalia na nafasi ya kujaribu kuibadilisha anapojiunga na chuo ambapo pia kuna ushindani mkubwa.

Awamu ya kujaribu kuzibadilisha au kuzibadilisha hasa imefikia tamati angalau kwa wanagenzi wa mwaka wa kwanza chuoni; yaani, mwaka wa kiakademia wa 2019/2020.

Je, baada ya awamu ya kuhama kufikia hatima, umeridhishwa na kozi uliyosalia nayo?

Iwapo jawabu lako ni ndio, makala haya ni kwa ajili yako sawa na yule ambaye jawabu lake ni la kwani yapo mambo muhimu mnayopaswa kuyaangazia mnapopiga hatua.

Taaluma na mwanataaluma

Jambo la kwanza la kukumbuka ni kwamba hakuna taaluma bora bali mwanataaluma bora.

Mtoa nasaha mwenzangu alipotoa kauli hii kwa mara ya kwanza nilifikiri alikuwa amekosea na nia yake ilikuwa labda kuhamasisha tu, lakini baada ya kuiwazia kwa muda, nilikubaliana naye.

Ni mazoea ya wengi wetu kuzitukuza kozi fulani na kuzidhalilisha nyingine katika soko letu la ajira. Umewahi kujiuliza; nikifeli katika kozi ithaminiwayo yaweza kuwa ya manufaa gani kwangu?

Hili ndilo swali muhimu wanalokosa kujiuliza wanagenzi wengi wa vyuo vikuu na vya kadri.

Kwa jinsi hiyo, hutumia muda wao mwingi kufanya mzaha wakijua wanasomea kozi muhimu na kwa vyovyote vile lazima wapate namna ya kujikimu kwazo; wakifuzu wasifuzu.

Kwa upande mwingine, sijui iwapo umemwona mtaalamu bora wa taaluma ziepukwazo na wanagenzi wengi wa vyuo vikuu akihangaika.

Naona karibu unaniuliza: unakusudia nini ‘mtaalamu bora?’ Ninalokusudia ni kwanza, mtu ambaye anaithamini taaluma yake. Kuithamini hapa kuna maana kwamba anaiona kuwa wenzo wa kuyaboresha mazingira yake na ya wengine. Maisha yake ni taaluma yake na taaluma yake ni maisha yake hivi kwamba ukijaribu kuyatenganisha haya mawili huwezi.

Ikiwa ni mwanahabari, kila tukio jipya analolishuhudia linampa changamoto ya kutumia uwezo na maarifa yake kubatilisha yasiyofaa.

Mwanataaluma bora ni aliyefuzu vizuri katika taaluma yake; yaani, ametimiza matakwa yote ya kozi anayoisomea na kuwaridhisha wengi wanaomtathmini au hata wote ikiwezekana.

Yeye hufanya bidii katika taaluma yake na kubuni mbinu za kuitumia kubadilisha maisha yake na ya watu wengine kwa njia chanya kupitia kwayo. Jambo la busara kwako kufanya hivyo basi ni kujizamisha katika kozi yako ukijua ndiyo ya msingi kuubaini mustakabali wako.

Nawe uliye katika ngazi za chini masomoni, ifanye bidii, nidhamu na mashauriano kuwa mazoea yako kwani ndivyo vitakuvukisha hadi ngazi za juu na hatimaye kukufanikisha katika taaluma yako.

Jifunze kutenda daima kama mwanataaluma utakaye kuwa katika siku za halafu. Ukichukua mkondo huo, mambo yataanza kukutengenea; na mapema.