Makala

Wasimulia kuhusu maisha yao sasa baada ya uwaziri

Na JUSTUS OCHIENG January 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

KUTOKA kuwa na mamlaka makubwa na ulinzi wa kisiasa, mawaziri waliofutwa kazi na Rais William Ruto kufuatia maandamano yaliyoongozwa na vijana dhidi ya serikali Julai mwaka jana sasa wanaishi katika baridi, mbali na majukumu yao ya zamani.

Watu hao waliokuwa mashuhuri katika utawala wa Kenya Kwanza, wakifurahia mamlaka ya mawaziri sasa wako mbali na mamlaka, ushawishi wao ukipungua hadi minong’ono tu ya zama zilizopita.

Wakiwa wamevuliwa nyadhifa zao kufuatia maandamano makubwa dhidi ya utawala wa Ruto yaliyofikia kilele mwezi wa Juni na Julai 2024, wamejipata wakitengwa na kukabiliana na ukweli wa kisiasa baada ya kuporomoka.

Baadhi yao waliporejea katika baraza la mawaziri na wengine kupatiwa majukumu mapya serikalini, bahati haikutabasamu kwa Simon Chelugui (Ushirika), Aisha Jumwa (Jinsia, Utamaduni, Sanaa na Urithi), Ezekiel Machogu (Elimu), Zachariah Njeru (Maji), Mithika Linturi (Kilimo na Maendeleo ya Mifugo).

Aliyekuwa Waziri wa Afya, Susan Nakhumicha. Picha|Hisani

Wengine ni pamoja na Susan Nakhumicha (Afya), Peninah Malonza (Jumuiya ya Afrika Mashariki), Florence Bore (Kazi na Jamii) na Njuguna Ndung’u (Hazina ya Kitaifa).

Bw Machogu anasema mtindo wake wa maisha umebadilika, kwani sasa anaweza kufurahia uhuru wa kuzima simu zake na kulala kwa raha – mbali na dharura za mara kwa mara na shinikizo kubwa alizokabiliana nazo akihudumu katika Baraza la Mawaziri.

“Lazima nikiri kwamba kazi ilikuwa ngumu sana. Nilikuwa naamka mapema sana kufika ofisini saa kumi na mbili asubuhi na kuondoka nikiwa nimechelewa, nikifika nyumbani saa tisa alasiri,” aliambia Taifa Leo.

“Sasa, ninaweza kuamka saa kumi na mbili asubuhi, kufanya mazoezi yangu ya asubuhi vizuri na kufika kwenye biashara yangu ya kibinafsi saa mbili asubuhi,” aliongeza.

Bw Machogu ambaye ni mtumishi wa umma na aliyekuwa mbunge wa Nyaribari Masaba ambaye alihudumu katika ngazi tofauti serikalini, anasema kufuatia kufukuzwa kwake, anatulia na biashara yake ya kibinafsi na kubuni nafasi za ajira kwa Wakenya wengine.

“Namshukuru Mwenyezi Mungu na rais kwa kunipa nafasi ya kuhudumu kama waziri serikalini. Sidhani nahitaji kazi yoyote sasa. Ninaweza kutumikia nchi katika nafasi tofauti, kutengeneza ajira kwa vijana katika sekta ya kibinafsi,” alisema.

 

Aliyekiwa Waziri wa Ushirika na MSMEs. Picha|Maktaba

Kwa Bw Chelugui, ambaye alikuwa waziri pekee wa zamani kutoka utawala wa Uhuru Kenyatta wa Jubilee katika baraza la mawaziri la kwanza la Rais Ruto baada ya ushindi wake katika uchaguzi wa 2022, maisha yake sasa yako katika sekta ya kibinafsi..

Bw Chelugui anasema kwamba alilazimika kurudi kwenye sekta ya kibinafsi ili kutafuta riziki baada ya Baraza la Mawaziri kuvunjwa Julai 2024.

“Nilirejea katika sekta binafsi katika sekta ya maji, nishati na madini. Pia ninaongeza thamani ufugaji wa ng’ombe,’ aliambia Taifa Leo katika mahojiano ya kipekee.

Bi Jumwa anashukuru hatua ya Rais Ruto kumfanya waziri wa kwanza mwanamke kutoka kabila la Mijikenda.

“Namshukuru Mungu na ninamshukuru sana Rais William Samoei Ruto kwa kufanya lisilowezekana kwa kuniteua kuwa mwanamke wa kwanza wa Mijikenda katika Baraza lake la Mawaziri,” aliambia Taifa Leo.

“Nimejitolea wakati wangu katika uwezeshaji wa jamii kupitia mipango kama Aisha Jumwa Foundation, ambayo inalenga kusaidia vikundi vilivyo hatarini, haswa kina mama vijana. Pia ninajihusisha na mashirika ya msingi ili kushughulikia masuala muhimu kama vile ukosefu wa ajira kwa vijana, elimu, na mabadiliko ya hali ya hewa,” anasema.

Aliyekuwa Waziri wa Jinsia, Utamaduni, Sanaa na Turathi, Bi Aisha Jumwa. Picha|Maktaba

Bi Jumwa anaongeza kuwa kupitia hili, ameweza ‘kuungana tena kwa kina na jamii na kutetea maendeleo endelevu mashinani.’

“Kama nitaitwa kuhudumu tena, nitakubali fursa hiyo kwa kujitolea na unyenyekevu. Shauku yangu ya kuleta mabadiliko katika uongozi na maendeleo ya jamii bado haijayumba, na ninaamini uzoefu wangu unanipa nafasi ya kuchangia ipasavyo katika wadhifa wowote,” akasema Bi Jumwa.

Bw Njeru, ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Ardhi na baadaye Waziri wa Maji, Usafi wa Mazingira na Unyunyuzaji kabla ya kuondolewa kazini Julai, anasema hivi majuzi ameanza kilimo.

“Tangu kuondoka madarakani, nimeendelea kujishughulisha sana. Nimekubali sura hii mpya kwa matumaini, nikizingatia kutoa michango ya maana kwa jamii yangu na ulimwengu wa biashara,” anasema.

Aliyekuwa Waziri wa Kilimo Mithika Linturi. Picha|Maktaba

Bw Linturi, ambaye alihudumu kama Waziri wa Kilimo, alikataa kufichua anachofanya ili kujikimu kimaisha.

“Tunaweza kupanga ziara ya mahali ninapofanyia kazi,” Bw Linturi aliambia Taifa Leo, huku Bi Nakhumicha akisema akiwa Waziri wa Afya alifanya vyema kabla ya kuondolewa afisini.

“Unajua mafanikio yangu. Yanajieleza yenyewe,” aliambia Taifa Leo.

Kwa upande wao, Bi Malonza na Bi Bore hawakujibu mara moja maswali kutoka Taifa Leo.

Huku wakiteseka pembezoni, baadhi ya wenzao walibahatika kurejea kwenye baraza la mawaziri baada ya kufutwa kazi kwa muda.

Waliorejeshwa ni; aliyekuwa waziri Kithure Kindiki ambaye alipandishwa cheo hadi Naibu Rais baada ya kutimuliwa kwa Rigathi Gachagua; Kipchumba Murkomen aliyehamishwa kutoka Barabara na Uchukuzi hadi Michezo na sasa Masuala ya Ndani; Aden Duale (aliyehamishwa kutoka Ulinzi hadi Mazingira); Alice Wahome (Ardhi), Alfred Mutua (aliyehamishwa kutoka Utalii na Wanyamapori hadi Kazi); Rebecca Miano (kutoka Uwekezaji, Biashara na Viwanda hadi Utalii); Soipan Tuya (kutoka Mazingira hadi Ulinzi),

Wengine ni; Davis Chirchir (aliyehamishwa kutoka Waziri wa Kawi na Petroli na kupelekwa Barabara na Uchukuzi), Salim Mvurya (alihamishwa kutoka Madini hadi Michezo); na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Justin Muturi (sasa waziri la Utumishi wa Umma).

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA