Makala

Wasiwasi watoto wakihusishwa kwenye uhalifu na majangili wakomavu

Na OSCAR KAKAI September 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

HUKU Kero la ujangili na wizi wa mifugo likiendelea kusababisha maafa kwenye maeneo mengi yenye utata Kaskazini mwa Bonde la Ufa, washikadau wa amani wamelalamikia kuhusika kwa watoto kwenye suala la ujangili.

Kwa mfano, kesi saba za watoto ambao walihusika kwenye ujangili na wizi wa mifugo ziliripotiwa katika mahakama ya Kapenguria Kaunti ya Pokot Magharibi ndani ya miaka miwili iliyopita.

Kulingana na  hakimu mwandamizi katika mahakama ya Kapenguria, Stella Nekesa Telewa, watoto wengi wanakabiliwa na mkono wa sheria kwa kufanya makosa hayo.

“Masuala ya watoto yanafaa kushughulikiwa kwa makini sababu wengi wako na changamoto nyingi. Wengi wanahusika kwenye ujangili na wizi wa mifugo. Watoto hupata shida wakati kesi zinaendelea na wanafaa kuwa na korti yao maalumu ambayo inafaa kwa mazingira ya watoto. Tunabuni korti ya kukabiliana na kesi kama hizo,” alisema.

Taifa Leo imebaini kuwa watoto wengi chini ya miaka 18 katika eneo hilo huchunga mifugo na kwenye mchakato huo huanza kufanya mashambulizi na kuiba mifugo.

Mwaka jana, shule ya upili ya Turkwel Gorge ilifungwa kwa muda fulani baada ya wanafunzi kutoka jamii za Pokot na Turkana kuhusika kwenye mzozo.

Kulikuwa na madai kuwa baadhi ya wanafunzi kutoka jamii ya Turkana ambao husoma kwenye shule hiyo wanashukiwa kwa kuhusika kwenye ujangili na kumuua mwana bodaboda katika eneo la Sarmach.

Mkazi kutoka eneo la Turkwel, Charles Kedikedi, alidai kuwa baadhi ya wanafunzi kutoka kwa shule hiyo walioonekana na wanashukiwa baada ya kuhusika kwenye mauaji.

“Wanafunzi kutoka eneo la Lorogon na Kainuk wanashukiwa kwa sababu baada ya kupigana na wenzao walirudi kwenye kijiji baada ya maafisa wa kupambana wa ghasia(GSU) kuwasili. Walikuwa wanashirikana na wazazi wao,” alisema Bw Kedikedi.

Uchunguzi unaonyesha kuwa maeneo mengi ya Uganda Kaskazini uaonyesha kuwa watoto wengi kutoka Kenya ambao huhama hadi Uganda kuchunga mifugo hugeuka kuwa majangili.

Ripoti ya National Crime and Research Centre (NCRC)2024, inafichua kuwa watoto huhusika kwenye kuficha na kuhama na mifugo walioibiwa, kuvamia na kuchunguza maeneo ambayo yanayofaa kuvamiwa kwa niabia ya  wakora na wezi wa mifugo wakomavu.

Hii imeathiri masomo huku idadi kubwa ya watoto wakisalia nyumbani kuenda shule katika eneo hilo.

Imetambuliwa kuwa masomo yameathirika kutokana na visa vya wizi wa mifugo ambavyo vimeshamiri katika eneo hilo.

“Tumegundua kuwa maeneo ya mashinani kama Masol, kati ya watoto watano, wawili tu hurusiwa kuenda shuleni na wazazi wao. Wengi huhamia Uganda kuchunga mifugo,” alisema Domtilla Chesang, mratibu wa wakfu wa Irep Foundation ambao kusaidia kwa elimu ya watoto.

Bi Chesang anasema kuwa ujinga na kupuuza mambo ndio inachangia watoto wengi kutoenda shule na kuanza kuhusika kwenye visa vya utovu wa usalama.

Caroline Menach, Mwenyekiti wa Child Protection Network (CPN) katika mahakama ya Kapenguria, kaunti ya Pokot Magharibi aliwataka viongozi wapya waliochaguliwa kusaidia kumaliza maovu hayo kati ua vijana wadogo ambao badala ya kuenda shule wanahusika kwenye wizi wa mifugo na kuchunga mifugo.

“Watoto hawafai kuwa pamoja kwenye mahakama na watu wazima sababu kwa kufanya hivyo wataonekana wanyonge na kutishwa,” alisema.

Afisa wa masuala ya watoto katika kaunti ya Pokot Magharibi Philip Wapopa anasema kuwa vijana katika maeneo ya wafugaji wameharibiwa na suala la bunduki haramu na mila potovu ambavo zilipitwa na wakati kama mashambulizi na wizi wa mifugo pamoja huku ushindani ukiwepo kuhusu nyasi na maji.