WASONGA: Juhudi zifanywe kufunza madaktari zaidi kuhusu kansa
Na CHARLES WASONGA
TATIZO kuu katika mpango mzima wa tiba ya magonjwa sugu nchini huwa ni ukosefu wa wataalamu, vifaa na dawa za kutibu maradhi hayo.
Hii ndio maana kila mwaka Wakenya hutumia zaidi ya Sh10 bilioni kusafari kwenda katika mataifa ya ng’ambo kutafuta tiba ya magonjwa yasiyo ya kuambukizwa kama vile kansa, kisukari na maradhi ya figo.
Chini ya kivuli hiki nakubaliana na wazo la Gavana wa Kisumu Peter Anyang’ Nyong’o kwamba mpango wa serikali wa kuanzisha vituo 10 vya kukabili maradhi ya kansa nchini hautakuwa na maana bila kuwepo kwa wataalamu wa kuhudumu katika vituo hivyo.
Akihutubu katika ibada wa ukumbusho wa marehemu Gavana wa Bomet, Joyce Laboso, Rais Uhuru Kenyatta alitangaza kuwa vituo ya kutibu kansa vitaanzishwa katika kaunti za Kisumu, Kakamega, Garissa, Meru, Mombasa, Machakos, Kisii, Nakuru na Bomet kutoa tiba ya kansa.
Lakini Profesa Nyong’o, ambaye amewahi kuugua kansa, anasema rasilimali zinapasa kuelekezwa katika mpango wa kutoa mafunzo kwa wataalamu wa kutibu maradhi hayo na ununuzi wa mitambo ya matibabu katika vituo vichache vilivyoko nchini.
Wazo hilo lina mashiko kwa sababu hospitali mbili za umma ambazo hutoa tiba ya kansa hazina vifaa na watalaamu wa kukabiliana na jinamizi hilo. Hospitali hizo ni Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) na Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Moi (MTRH), iliyoko Eldoret ambazo hutoa tiba hiyo kwa gharama nafuu ikilinganishwa na hospitali za kibinafsi.
Ahadi ya serikali mwaka jana kwamba ingetenga Sh350 milioni kwa hospitali ya MTRH kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kutibu kansa haikutimizwa kama ilivyothibitishwa na wabunge wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Afya waliozuru hospitali hiyo mapema mwaka huu.
Inasikitisha kuwa mpango uliofadhiliwa na Serikali ya Kitaifa ya kuziwezesha serikali za kaunti kukodisha vifaa vya kisasa vya kutibu maradhi sugu haukujumuisha vifaa vya kutibu saratani licha ya kwamba huua takriban watu 33,000 kila mwaka.
Kando na ukosefu wa mitambo ya kisasa, ukweli mwingine ni kwamba taifa la Kenya linakabiliwa na uhaba mkubwa wa wataalamu wa tiba. Kwa mfano, kulingana na Chama cha Wataalamu wa Kansa Nchini kuna madaktari 45 pekee kansa nchini.
Mwenyekiti wa chama hicho David Makumi amenukuliwa akisema kuwa asilimia 80 ya wataalamu hao wanahudumu katika miji mikubwa ya Nairobi, Mombasa, Eldoret na Kisumu pekee wengi wao wakihudumu katika hospitali za kibinafsi.
Kwa hivyo, kibarua sasa ni kwa serikali kufadhili mipango ya kutoa mafunzo kwa waatalamu wa kansa katika Chuo Kikuu cha Nairobi au kile cha Moi. Wanafunzi wengine wafadhiliwe kujinoa katika mataifa ya ng’ambo kama vile Amerika na Cuba, ambako kuna taasisi bora za kushughulikia maradhi hayo.
Na sio hayo tu, wataalamu watakaoajiriwa walipwe mishahara inayolingana na viwango vilivyoko katika mataifa mengine ili wasihamie mataifa ya nje. Hatua kama hii ni bora kuliko kujenga vituo zaidi vya kutibu kansa ana kutangaza ugonjwa huo kuwa jamba la kitaifa.