WASONGA: Mutyambai akabiliane na maafisa majambazi
Na CHARLES WASONGA
KATIKA siku za hivi karibuni, vyombo vya habari vimejaa ripoti kuhusu visa ambapo baadhi ya maafisa wa polisi wamekuwa wakijuhusisha katika vitendo vya uhalifu badala ya kuwalinda wananchi.
Wengi wetu tunashindwa kuelewa ni kwa nini maafisa walioajiriwa kulinda maisha na mali yetu ndio wanatugeuka kutupora na hata kutudhuru kwa kutumia silaha zilizonunuliwa kwa ushuru tunaolipa.
Mwezi huu mahakama kuu ilielezwa namna maafisa wa AP waliokuwa wakihudumu katika kituo cha Syokimau walivyowateka nyara, wakawazuilia na kisha kuwaua kinyama wakili Willie Kimani, mteja wake Josphat Mwenda na dereva wa teksi Joseph Muiruri mnamo 2016.
Miili yao iliwekwa ndani ya magunia na kutupwa katika mto Oldonyo Sabuk.
Mnamo Septemba 26 afisa mmoja wa Jeshi la Kenya (KDF) na polisi watatu wa utawala walinaswa kuhusiana na wizi wa Sh72 milioni katika mtambo wa ATM katika mtaa wa Nairobi West.
Na wiki jana constable Simon Mwaniki wa Kituo cha Polisi cha Kayole, Nairobi ambaye alihusishwa na wizi wa Sh6 milioni alikamatwa.
Kwa ujumla, takriban maafisa 48 wa polisi wamekamatwa na kushtakiwa kwa makosa mbalimbali. Na inasikitisha kuwa baadhi yao hushirikiana na wahalifu kuwahangaisha wananchi ambao wanapaswa kuwalinda.
Takwimu hizi kutoka kwa Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) zinathibitisha kwamba kuna uozo fulani katika taasisi hii ambayo kauli mbiu yake ni “Huduma kwa Uadilifu”.
Utundu huu miongoni mwa maafisa wa huduma hii bila shaka unaondfoa imani ya umma kwa utendakazi wao ikizingatiwa kuwa maafisa hawa wanahitaji ushirikiano kutoka kwa wananchi ili waweze kufaulu katika utekelezaji wa majukumu yao.
Ili kurekebisha hali, Inspekta Jenerali Hillary Mutyambai anapaswa kuhakikisha kuwa wakuu wa vitengo husika katika NPS wanafuatilia kwa maakini mienendo ya maafisa chini yao.
Kwa mfano kitengo kama, “Internal Affairs Unit”, ambacho hufuatilia ikiwa maafisa wanazingatia kanuni za utendakazi inapasa kupambana vikali na maafisa watundu wanaoharibia wenzao sifa.
Afisi ya Bw Mutyambai inapasa kufanya kazi sako kwa bako na Mamlaka Huru ya Kuchunguza Utendakazi wa Polisi (Independent Policing Oversight Authority-IPOA) kwa kuhakikisha kuwa maafisa watundu wanafutwa kazi kisha kuadhibiwa vikali.
Hii ni kwa sababu kuna maafisa wengi wazuri na wachapa kazi kwa uadilifu ambao sifa zao hazipasi kuharibiwa na wenzao wachache wanaoamua kujiingiza katika vitendo vya uhalifu ili kujitajirisha haraka.
Lakini inaridhisha kuwa wiki jana Bw Mutyambai aliongoza mkutano ulioshirikisha maafisa wake wakuu ambapo maamuzi muhimu yanayolenga kuzima visa vya maafisa kushiriki uhalifu yaliafikiwa.
Mathalan, iliamuliwa kuwa maafisa wote wa polisi wawe wakivalia sare rasmi wakiwa katika shughuli rasmi na wale ambao wamekaa katika kituo kimoja kwa kipindi kirefu wapewe uhamisho.
Sasa mtihani kwa Bw Mutyambai ni kuona kuwa hizi na hatua nyinginezo ambazo amechukua kuzima uozo huu zinazaa matunda.
Haja yetu kubwa kama wananchi ni kuwaona maafisa wa polisi kama walinzi wetu wala sio wahalifu.