Makala

WASONGA: Raia wanataka suluhu kwa matatizo, sio siasa

March 26th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

WAKATI huu maadui wakubwa wa Wakenya wakati huu ni njaa, kiangazi na ufisadi. Ndiyo matatizo makuu yanayoangaziwa zaidi katika vyombo vya habari.

Kikatiba, wajibu wa serikali ni kulinda maisha na mali ya wananchi wote kwa kupambana na matatizo kama haya, na mengineyo.

Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuongoza vita dhidi ya changamoto hizi, ambazo yamkini zina uwezo wa kuyumbisha mipango ya maendeleo iliyoratibiwa na serikali wanayoiongoza.

Kwa kufanya hivyo, bila shaka, mashirika ya kibinafsi, wafadhili na Wakenya kwa jumla wataungana na wawili hawa, pamoja na mawaziri wao, kupambana na matatizo haya.

Lakini kinaya ni kwamba katika hotuba zake katika mikutano ya hadhara maeneo kadhaa nchini, Dkt Ruto amekuwa akionekana kuelekeza nguvu zake katika kumshambulia kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Nimefuatilia kwa makini hotuba zake katika maeneo ya Kisii, Pokot Magharibi, Kericho, Mandera na Nairobi na kubaini kuwa suala kuu limekuwa ni kumlaumu Bw Odinga kwa kile anachodai ni njama ya kiongozi huyo wa upinzani kutumia muafaka kati yake na Rais Kenyatta kusambaratisha chama cha Jubilee.

Wabunge wanaomuunga mkono, vile vile, wamekuwa wakikariri kibwagizo hicho wakidai Bw Odinga anatumia muafaka huo na vita dhidi ya ufisadi kuzima ndoto ya Dkt Ruto kuingia Ikulu 2022.

Badala ya Dkt Ruto kutumia rasilimali za umma kuzunguka kote nchini akimshutumu Bw Odinga, angetumia muda wake mwingi kuongoza kampeni za kuwahamasisha Wakenya kuhusu mbinu za kudumu kukabiliana na njaa, kiangazi na wizi wa mali ya umma.

Wakati huu haja kuu ya zaidi ya Wakenya milioni moja wanaokabiliwa na baa la njaa, sio kujua nani anapanga kusambaratisha chama fulani cha kisiasa. Hawataki kujua malengo ya “handsheki” kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga. Hawataki kujua mwanasiasa ambaye anajuhumu nafasi ya mwenzake kuingia Ikulu mnamo mwaka wa 2022.

Wakati huu raia wanataka chakula kwa dharura ili wasife. Bila shaka habari kwamba takriban watu 17 wamefariki kwa kukosa chakula, licha ya Dkt Ruto kukana, imewatia woga wananchi katika kaunti 17 zinazoathirika na njaa iliyosababishwa na kiangazi.

Dkt Ruto anashilikia kuwa kuna chakula cha kutosha nchini na shida iliyoko ni ya usambazaji. Lakini mbona hajaamuru afisi yake kuelekeza fedha iliyotengewa katika bajeti kugharamia usafiri wa kusambaza chakula kwa waathiriwa wa njaa katika kaunti 17?

Mbona hajamuagiza Waziri wa Fedha Henry Rotich kuwasilisha bajeti ya ziada bungeni itakayotenga pesa za kugharamia usambazaji wa chakula kutoka maeneo ya North Rift hadi maeneo yenye ,mahitaji makuu?

Ni aibu kwamba Dkt Ruto hutumia pesa za umma kuzuru maeneo mbalimbali nchini kumshambulia Bw Odinga, ilhali watu ambao walimwezesha kupata cheo anachoshikilia sasa, kupitia upigaji kura, wanalemewa na njaa.

Bw Odinga hana cheo chochote katika serikali ya Jubilee. Kwa hivyo siamini kwamba ana uwezo wowote wa kusambaratisha chama cha Jubilee alivyobomoa Kanu mnamo 2022.

[email protected]