WASONGA: Rais Kenyatta, naibu wake waonyeshe maafikiano
Na CHARLES WASONGA
SI siri kwamba katika mwaka wa 2019, unaokamilika leo Jumanne, uhusiano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto haujawa mzuri.
Hii ni licha ya madai ya Dkt Ruto kwamba hali ni shwari kati yake na bosi wake na kwamba wale wanaodai kuwa hawaelewani ni “viongozi wa upinzani wanaotaka kusambaratisha Jubilee ili wapate mwanya wa kuingia uongozini mwaka wa 2022”.
Lakini ukweli ni kuwa mara kadhaa, Rais na naibu wake wameonekana wakitofautiana, hata hadharani, kuhusiana na masuala ya sera na maongozi ya serikali wanayoingoza.
Kwa mfano, Rais Kenyatta na Dkt Ruto hawajaafikiana kuhusu vita dhidi ya ufisadi. Huku kiongozi wa taifa akiunga mkono utendakazi wa asasi husika katika vita hivyo, Dkt Ruto hudai kuwa vita hivyo vimeingizwa siasa.
Huwa anasema hadharani katika mikutano ya kisiasa kwamba asasi kama Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) zinatumika kuwaandama watu wanaosawiriwa kuwa wandani wake.
Lengo hapa, kulingana naye, ni kuzima ndoto yake ya kuingia Ikulu mwaka wa 2022 baada ya Rais Kenyatta kustaafu.
Hii ndiyo maana, mapema mwaka huu, alipuuzilia mbali uchunguzi wa DCI kuhusiana na madai ya kupotea kwa Sh21 bilioni katika mradi wa ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwerer, akidai ni Sh7 bilioni pekee zilipotea.
Mwishowe Waziri wa Fedha, aliyesimamishwa kazi, Bw Henry Rotich na aliyekuwa Katibu katika Wizara ya Fedha Kamau Thugge, na maafisa wengine wa serikali, walifikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa sakata hiyo.
Katika mwaka mpya wa 2020 unaoanza kesho, Rais Kenyatta na Dkt Ruto wanapaswa kuweka kando tofauti zao na kuonyesha wananchi kuwa wanalandana kifikra kuhusu ajenda zote za serikali hii.
Tunataka kuona taswira ya viongozi wanaoelewena kuhusu suala kuu la utekelezaji wa ahadi walizowapa wananchi kuelekea uchaguzi mkuu wa 2017.
Ni aibu kumwona Rais akitoa mwongozo kuhusu suala muhimu kama vita dhidi ya ufisadi au haja ya viongozi wa serikali kutangaza asili za mali zao lakini baadaye naibu wake, sawa na wanasiasa wandani wake, anapinga.
Rais Kenyatta aondoe dhana iliyokolea miongoni mwa wafuasi wa Dkt Ruto kwamba kuna mawaziri na maafisa fulani wanaoshikilia vyeo vya juu serikalini ambao wanatumiwa kumhujumu naibu wake.
Afanye hivyo kwa kutoa agizo kali kwa mawaziri na maafisa husika kwamba wanapaswa kumheshimu Dkt Ruto.
Hii ni kwa sababu Naibu Rais ndiye kiongozi wa kipekee nchini ambaye anaruhusiwa kikatiba kushikilia wadhifa wa urais endapo atashindwa kutekeleza majukumu ya afisi hiyo kutokana na sababu ambazo haziwe kuepukika.
Waziri ambaye Rais anapaswa kudhibiti zaidi ni Fred Matiang’i (Usalama wa Ndani) ambaye mara kadhaa ameonekana akimkosea heshima Dkt Ruto.
Mfano ni madai aliyotoa katika Kaunti ya Kirinyaga mnamo Novemba 29 kwamba anawajibika kwa Rais pekee, akiashiria kutomthamini Dkt Ruto. Alisema, “Kila boma linaongozwa na mzee mmoja pekee. Hakuna boma linaloongozwa na wazee wawili”.
Na kwa upande wake, Dkt Ruto anapaswa kumheshimu Rais Kenyatta.
Akome kampeni za mapema kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa 2022 kama ambavyo bosi wake hukariri kila mara. Na aunge mkono vita dhidi ya ufisadi.
Mwaka mpya wa 2020, tunataka kuwaona Rais na naibu wake ambao hawatoi kauli kinzani hasa kuhusu masuala ya uongozi na maadili.