Makala

WASONGA: Viongozi waendeshe kampeni ya kupanda miti

December 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

WANASIASA Ni watu ambao wamepewa kipawa cha kuteka hisia na kushawishi umma, haswa kuhusu masuala ya kisiasa yanayolenga kuwafaidi wao.

Tulishuhudia haya majuzi katika uchaguzi mdogo eneo bunge la Kibra. Na sasa wanaendeleza kampeni kuhusu njia mwafaka ya kufanikisha utekelezaji wa ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI).

Sambamba na kuendeleza mjadala kuhusu suala hili, ingekuwa jambo la busara kwa wanasiasa wetu kutumia majukwaa mbalimbali kuwahamasisha wananchi wapande miti kwa wingi wakati huu ambapo mvua inanyesha kote nchini.

Na mawaziri wa serikali ya kitaifa, wakiongozwa na Waziri wa Usalama Fred Matiang’i wapaswa kuwa mstari wa mbele kuendeleza kampeni ya upanzi wa miti wanapovumisha ripoti ya BBI.

Serikali za kaunti nazo zivalie njuga mpango huu muhimu kwa kuandaa shughuli za upanzi wa miti ya kiasili na ya kisasa.

Nasema hivyo kwa sababu wataalamu wamebaini kuwa maporomoko ya ardhi na mafuriko ambayo yamesababisha maafa katika maeneo mbalimbali nchini yanaweza kuzuiwa kupitia upanzi wa miti kwa wingi.

Kufikia sasa zaidi ya watu 50 wamefariki kutokana na maporomoko ya ardhi sehemu kadha nchini, Kaunti ya Pokot Magharibi ikiathirika zaidi.

Kampeni ya upanzi wa miti iliyoanzishwa na Rais Uhuru Kenyatta mwaka jana inaweza kufana zaidi endapo itakumbatiwa kikamilifu na wanasiasa wetu, haswa wakati huu wanapoendeleza mjadala kuhusu ripoti ya BBI.

Akianzisha kampeni hiyo katika Shule ya Msingi ya Moi Forces Academy, Nairobi mnamo Mei 13, 2018, Rais alisema serikali inalenga kuhakikisha kuwa miti 1.8 bilioni imepandwa kote nchini kufikia 2022.

Kwa hivyo, huu ndio wakati ambapo Kenya kama taifa inaweza kuafikia azma ya kufanya asilimia 10 ya ardhi yake kusetiriwa na misitu sambamba na matakwa ya Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira (UNEP).

Ikiwa nchi hii itafikia azma hii, bila shaka matatizo kama vile kiangazi, mafuriko na maporomoko ya ardhi yatapungua kwa kiasi kikubwa.

Wananchi watafaidi kwa kupata maji ya matumizi katika shughuli za kilimo, nyumbani na uzalishaji bidhaa katika viwanda.

Mito muhimu kwa uzalishaji umeme, kama Tana na Sondu haitakosa maji ya kujaza mabwawa ya kuzalisha kawi. Idadi ya wanyama pori, ambayo ni nguzo kuu katika ustawi wa sekta ya utalii, itaongezeka.