Watafiti watafuta ufumbuzi jinsi ya kukabiliana na madini yasababishayo fluorosis
Na MAGDALENE WANJA
WAKATI Bw Julius Njoroge alipata habari kuwa kuna shughuli ya usajili makurutu wa jeshi, KDF, hakusita kujitokeza.
Alikuwa tayari amepata matokea ya mtihani wake wa kidato cha nne.
Siku ya usajili, alifaulu katika vitengo mbalimbali uwanjani Afraha, lakimi awamu ya mwisho kabisa ikatia mchanga kitumbua afisa aliyekuwa akimfanyia ukaguzi alipomwambia kinywa chake ni kibovu.
Bw Njoroge hakuelewa maana ya matamshi hayo kwani alikuwa amepiga mswaki asubuhi kabla kufika pale.
Afisa huyo alimwambia kuwa hawezi kufanya kazi kama afisa wa KDF.
Njoroge ni mmoja tu wa baadhi ya vijana mjini Nakuru ambao ndoto zao za kujiunga na kikosi zimezimwa kutokana na kuharibika kwa meno.
Kwa miongo sasa, tatizo hili limekuwa likiwakumba wakazi wa maeneo ya Rift Valley.
Hii ni kutokana na unywaji wa maji yenye fluoride kupita kiasi.
Madhara yake ni ugonjwa wa fluorosis ambao hudhuru mifupa na meno ya wanyama na binadamu.
Hatari hata zaidi ni kuwa madini hayo hayaingii kwenye mwili wa binadamu kupitia maji ya kunywa pekee.
Mradi wa kufanya utafiti wa madini hayo ulioanzishwa mwaka 2016 unaojulikana kama Flowered, umewaleta pamoja wanasayansi watakaosaidia katika kupata suluhisho la matatizo yatokanayo na madini hayo.
Wanasayansi ambao wamekuwa wakifanya utafiti katika maeneo ya Rift Valley wamebaini kuwa mimea na wanyama wengi wako na viwango vya juu ya madini hayo.
Binadamu anapoila nyama kutoanana wanyamahao au mimeayenye madini hao anayaongezea kwamwili.
Kulingana na Dkt Enos Wambu kutoka kitengo cha kemia na biolojia katika Chuo Kikuu cha Eldoret, utafiti wa hapo awali umeonyesha kuwa Nakuru ni mojawapo ya sehemu zenye viwango vya juu zaidi vya fluoride.
“Mradi huu unanuia kutafiti jinsi ya kupunguza viwango vya fluorine kwenye maji ya kunywa na ile ya mimea,” akasema Dkt Wambu.
Bi Noel Makete ambaye ni mwanafunzi wa wa uzamifu katika Chuo Kikuu cha Eldoret ni mmojawapo wa watafiti ambao wanatafiti katika maeneo mbalimbali ya Nakuru.
Alisema kuwa mradi huo ulianzia utafiti katika vyakula aina tatu muhimu zaidi nchini ambavyo ni mahindi, viazi na sukunawiki.
“Tunatumai kubaini iwapo ni ukweli kwamba mimea inavuta madini ya flouride kutoka kwa mchanga na kwa kiasi gani,” alisema Bi Makete.