Makala

Watahiniwa mbioni kubadilisha kozi ambazo KUCCPS iliwapa

Na NA MERCY SIMIYU May 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MAELFU ya wanafunzi ambao hawakupewa kozi za digrii walizopendelea na Asasi ya Kuteua Wanafunzi wa Kujiunga na Vyuo Vikuu na Vile vya Kadri (KUCCPS) wanakabiliwa na changamoto nyingi wanapobadilisha kozi hizo.

Wanafunzi hao wamepewa muda wa hadi Jumanne wiki ijayo kutuma maombi ya kozi zingine badala ya zile walizopendelea kupata idadi tosha ya wanafunzi.

Hata hivyo, wale waliozungumza na Taifa Leo walielezea changamoto wanazopitia kuchagua kozi mpya, haswa kuhusiana na gharama ya kozi hizo na jinsi serikali inakavyozifadhili.

KUCCPS haitaweka karo ya kozi kwenye tovuti yake inayotumiwa na wanafunzi kutuma maombi, ilivyokuwa ikifanya miaka miwili iliyopita serikali ilipoanzisha mfumo mpya wa ufadhili wa masomo katika Vyuo Vikuu.

Mwaka jana, Mahakama Kuu iliamua kuwa mfumo huo unakiuka katiba lakini serikali ikakata rufaa dhidi ya uamuzi huo.

Mnamo Machi mwaka jana, Mahakama ya Rufaa ilisitisha utekelezaji wa uamuzi wa Mahakama Kuu, hadi kesi hiyo itakaposikizwa kamili na kuamuliwa.

Serikali pia haijasema lolote kuhusu namna wanafunzi wa vyuo vikuu watapata ufadhili.

Zaidi ya watahimiwa 240,000 waliofanya mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne (KCSE) 2024 walipata alama za kuwawezesha kujiunga na vyuo vikuu.

Kuanzia Jumapili KUCCPS ilitoa nafasi ya wanafunzi kubadilisha kozi wanazotaka kusomea katika vyuo vikuu na vyuo vya kiufundi (TVET).

“Nafasi ya wanafunzi waliotwa kujiunga na vyuo vikuu na vyuo vya TVET katika mwaka wa usajili wa 2025/2026 sasa ipo. Wale ambao hawakupata kozi wanayotaka katika kipindi cha kutuma maombi kilichokamilika Aprili 30, 2025 wanaalikuwa kuingia tena katika mtandano waa KUCCPS na kuteua kozi zilizosalia zilivyoorodheshwa humo,” KUCCPS ikasema kwenye taarifa fupi iliyopakia katika tovuti yake.

Katika kipindi cha kwanza cha wanafunzi kutuma maomba, KUCCPS ilisema kuwa zaidi ya watahiniwa 100,000 wa KCSE 2024 na kupata angalau gredi ya C+ hawakuwa wamewasilisha maombi ya kozi wanazotaka kusomea katika vyuo vikuu.

“Najaribu kutuma maombi  ya kozi ya Shahada ya Digrii katika Ualimu lakini chuo kikuu cha kipekee ninahitimu kujiunga nacho kiko Nyandarua. Vyuo vingine ni vya kibinafsi. Hii inavunja moyo,” akasema Reinson Collins.

Idadi kubwa ya wanafunzi wanasema gharama ya kozi, mahala ambako chuo kikuu kipo na sifa ya taasisi fulani ni miongoni mwa vigezo wanavyozingatia wanapochagua vyuo na kozi.

“Katika ombi langu la kwanza, nilitaka Shahada ya Uanasheria, Shahada ya Sanaa katika Mahusiano ya Kimataifa na Diplomasia na Shahada ya Digrii katika Mawasiliano na Uanahabari lakini kwa bahati mbaya nilikataliwa kwa kozi hizo zote na nikashauriwa kuomba kozi nyingine tofauti. Hata hivyo, kozi zilizosalia ziko katika vyuo vikuu vya kibinafsi ambazo mamangu hawezi kumudu kulipia kwa sababu nilitegemea misaada kutoka kwa wahisani katika shule ya upili. Vile vile, sina uhakika ikiwa Bodi ya Kufadhili Elimu ya Juu (HELB) inatoa ufadhili kwa wanafunzi wanaosomea katika vyuo vikuu vya kibinafsi,” akasema Vanessa Gitonga.