Makala

Watengenezaji wa majeneza wanafaa kufuata maadili na utaratibu upi?

June 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANGI MUIRURI

INGAWA kazi ni kazi, bora riziki, ile ya kuunda majeneza inasemwa kuwa sio kazi vile kwa msingi wa jinsi ambavyo inashirikishwa katika jamii.

Msanii Ng’ang’a Wa Kabari anauliza mbona biashara hii isiwe ya kuzingatia maombi ya watu waishi miaka mingi?

“Mimi nikitazama vile biashara ya kuunda majeneza hufanywa, nahofia kuwazia vile walio katika biashara hiyo huomba Mungu,” anasema Wa Kabari.

Wakati umejihisi kuwa mgonjwa, huwa unaomba Mungu akuponye na unapofungua biashara ya kuuza nguo, chakula, magari, kila aina ya bidhaa, maombi huwa ni Mungu akupe wateja.

Waombolezaji katika mazishi ya mwanahabari John Karume wakiongozwa na mjane Bi Grace Wambui (aliyevalia nguo nyeusi) wabeba jeneza la mabaki yake hadi kupumzishwa katika shamba la babake katika kijiji cha Kanyariri-Endarasha, Kaunti ya Nyeri mnamo Aprili 8, 2016. Picha/ Mwangi Muiruri

Ndipo anauliza hawa nao wa kuunda majeneza huwa wanaomba Mungu afanye nini ndipo wapate pesa? Na je, kazi yao inafaa kuzingatia utaratibu upi?

Anasema kuwa wafanyabiashara hao huwa wanaomba Mungu biashara yao istawi na ustawi huo unaweza tu ukaafikiwa baada ya watu wengi kuaga dunia.

“Biashara hii inafaa kuwekewa sheria kuwa, jeneza liwe likiundwa baada ya mtu kuaga dunia. Sio hali ya sasa ambapo mtu hutafuta mafundi 50, anakodisha jumba kubwa na hatimaye kuunda majeneza ambayo hayana maiti ya kuzika bali yanangojea watu waage dunia,” anasema.

Wahudumu hawa wa bodaboda walichanga pesa kununua jeneza hili ambalo ndani yake ni marehemu Jayne Nduta Murage katika mochari ya Murang’a Februari 14, 2017. Picha/ Mwangi Muiruri

Anasema kuwa wakati majeneza hayo yameundwa, mwenye biashara hiyo na wafanyakazi wake huwa wanaomba watu waage dunia ili kazi ipatikane na pia pato liingie.

“Unafungua duka la majeneza na unayajenga na hakuna mahali umeitishwa majeneza hayo? Si ina maana kuwa unaombea jamii dua mbaya?” anahoji.

Taharuki

Anasema kuwa wafanyabiashara hao ni kiungo thabiti cha kuzua taharuki na kupotea kwa matumaini kwa kuwa “hawa huweka biashara hizo nje ya hospitali na wagonjwa wakipelekwa hospitalini na kuyaona majeneza hayo, huwa wanaanza safari ya kuaga dunia papo hapo.”

Analia kuwa hata majeneza ya watoto huundwa kukiwa hakuna mtoto ameaga dunia kisha yanawekwa nje ya hospitali za wajawazito kujifungua.

Anateta kuwa wafanyabiashara hao wakipata habari za mahali ajali ya barabarani imefanyika, huwa wanapiga simu kuuliza ni wangapi wameaga ili watafute zabuni za kuunda majeneza.

Analia kuwa hata magari ya kubeba maiti yamejaa barabarani yakisaka kazi.

Je, ni maadili gani na utaratibu upi unafaa kuzingatiwa na hawa wanaofanya biashara ya aina hii?