• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 12:56 PM
Waumini wasifunge kwa sababu ni mazoea, wazingatie kumcha Mungu

Waumini wasifunge kwa sababu ni mazoea, wazingatie kumcha Mungu

NA KHAMIS MOHAMED

KWA kweli Ramadhani ni mgeni mwenye siku za kuhesabika. Tayari Kumi la Kwanza limetuaga na la Pili linakwenda kwa kasi sana.

Mfungaji mpendwa, swali kuu tunalofaa tujiulize, ni kwamba hadi sasa kwenye safari hii ya funga umejichukulia akiba ya kutosha? Tukumbuke akiba ilio bora katika safari hii ya funga ni Taqwa (Uchamungu).

“Enyi mlio amini! Mmeandikiwa Saumu, kama waliyoandikiwa walio kuwa kabla yenu ili mpate uchamungu.” (Al-Baqarah, 2:183)

Uchaji Mungu hupatikana kwa kufuata kwa unyenyekevu maamrisho yote ya Mwenyezi Mungu (S.W.T) na kuacha kwa unyenyekevu vile vile makatazo yote ya Mwenyezi Mungu (S.W.T) kwa kutarajia kupata radhi yake na kuepukana na ghadhabu zake.

Tumepata wasaa wa mwezi moja mzima wa kujikakamua katika suala zima la Uchamungu na kutenda matendo mema.

Kwa mfungaji anayefunga na bado anaendelea na maasi sambamba na maamrisho ya Mwenyezi Mungu, basi na ajue anafunga kwa mazoea tu. Lengo halisi la funga halijatimia kwake.

Haina haja ya kufunga na bado hatuwachi kusema uongo, kusengenya na kutenda vitendo viovu kwani itakuwa ni kazi bure tu kama tunavyoashiriwa na hadith iliyopokelewa na Abu Hurayrah (R.A) akisimulia kuwa Mtume (S.A.W) amesema: “Yule ambaye haachi kusema uongo na haachi kufanya vitendo viovu, Allah hana haja na kuona kuwa anaacha chakula chake na kinywaji chake (yaani Mwenyezi Mungu (S.W.T) hana haja na funga yake.” (Al-Bukhaariy.)

Tusifunge tu ilhali tunawacha swala za faradhi zitupite, tusifunge tu na ilhali tunasahau sala za tarawehe na tusifunge tu na Qur’an zetu manyumbani zinajaa vumbi kwa kutokudurusu kitabu kitukufu.

Ni vyema kila mmoja wetu ajitathmini nafsi yake aone kama hadi sasa amekuwa akifunga kwa mazoea ama ni wakati wakubadilika kwani bado kuna muda.

  • Tags

You can share this post!

Mkutano wa Gachagua, wafanyabiashara wadogowadogo wazaa...

Mpeketoni yapona makovu ya mashambulio ya Al-Shabaab

T L