Wauzaji wa mitumba walalama bei wanayochukulia bidhaa zao ni ya juu mno
Na SAMMY WAWERU
LICHA ya wafanyabiashara wa nguo zilizotumika maarufu kama mitumba kupata afueni baada ya serikali kuondoa marufu ya muda kwa nguo hizo kuingia nchini, wauzaji wa mavazi hayo sasa wanalalamikia bei ghali.
Wafanyabiashara tuliozungumza nao, wanasema wanakozitoa ni haba na zinazopatikana zinauzwa bei ghali.
Taifa Leo imetangamana na kufanya mahojiano na wafanyabiashara kadhaa katika Soko la Jubilee, Githurai, kiungani mwa jiji la Nairobi na pia eneo la Kahawa Wendani.
Kibanda cha Simon Wangare, kilichoko katika Soko la Jubilee, anachosema kabla ya Covid-19 kuingia nchini kilikuwa chenye shughuli chungu nzima kuhudumia wateja, anaopokea kwa sasa wanahesabika.
Ni muuzaji wa suruali ndefu za kike, long’i maarufu kama tights na pia kaptura.
“Nguo katika Soko la Gikomba hazipatikani licha ya biashara ya nguo za mitumba kurejelewa mapema wiki hii. Zilizopo tunauziwa mithili ya dhahabu,” Bw Simon akalalamika.
Soko la Gikomba, na lililoko jijini Nairobi ni maarufu katika uuzaji wa nguo kwa bei nafuu, na wauzaji wengi rejareja huziendea humo.
Akitumia mfano wa nguo aliyokuwa akiuziwa Sh30, kisha anauzia wateja rejareja kati ya Sh50- 100, Simon anasema kwa sasa anaipata na zaidi ya Sh70.
“Haya, niinunue Sh100, niuzie mteja zaidi ya Sh150 au hata Sh300, nani atainunua ilhali wanajua bei yake haipiti Sh100?” akashangaa mfanyabiashara huyo.
Simon alisema wafanyabiashara wa nguo za mitumba kipindi hiki wanakadiria hasara, ikizingatiwa kuwa ni sekta iliyobuni nafasi chungu nzima kwa Wakenya.
Malalamishi ya mfanyabiashara huyo si tofauti na ya Zipporah Ndereba ambaye huuza sketi.
“Huuzia wateja sketi moja kati ya Sh100 – 300, bei ambayo imegeuka kuwa ninayozinunua nayo sokoni. Imepanda mara dufu kutokana na athari za corona,” Zipporah akasema, kauli yake ikiwiana na ya Annitah Wairimu, muuzaji wa blauzi za mitumba eneo la Kahawa Wendani, Thika Road.
Ni gharama ya juu na ambayo imelazimisha Simon Wangare kujumuisha nguo mpya. Aidha, mfanyabiashara huyo anasema anafanya mauzo ya mitumba kwa wanaofika au kumudu bei.
“Huenda baada ya mwezi mmoja, kuanzia serikali ilipotangaza kuondoa marufuku ya mitumba, mambo yakarejea shwari. Nguo zilizotumika ni za bei nafuu na zinazonunuliwa upesi,” akasema mjasirimali huyo.
Virusi vya corona vilingia nchini Machi 2020, na ili kuzuia msambao zaidi, serikali ilipiga marufuku kwa muda uagizaji na ununuzi wa mitumba, nguo ambazo hutoka nje ya nchi. Ni hatua iliyoathiri kwa kiwango kikubwa wafanyabiashara wa mavazi hayo.
Kabla ya serikali kuondoa marufuku hiyo, migomo ya wauzaji wa nguo za mitumba Nairobi na Nakuru ilishuhudiwa, wakilalamikia biashara zao kuathirika pakubwa kwa sababu ya ukosefu wa nguo hizo sokoni.
Waziri wa Biashara Bi Betty Maina, hata hivyo alichapisha katika Gazeti Rasmi la Serikali, mikakati itakayofuatwa katika uagizaji na ununuzi wa mitumba kutoka nje, jambo ambalo limeonekana kuleta matumaini kwa wafanyabiashara wa nguo hizo za bei nafuu.