• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
Waziri ajiuzulu kufuatia upungufu wa pombe

Waziri ajiuzulu kufuatia upungufu wa pombe

CHARLES WASONGA Na MASHIRIKA

CHAMA tawala nchini Tanzania, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimemdadisi aliyekuwa Waziri wa Utalii Zanzibar, wiki kadha baada yake kujiuzulu kutokana na uhaba wa pombe katika kisiwa hicho.

Samia Mohamed Said alifika mbele ya kamati ya maadili ya chama hicho Jumanne jioni lakini hakufichua sababu ya kuagizwa kufanya hivyo.

“Ni jambo la kawaida kufika katika ofisi za chama. Na mimi si msemaji wa mikutano kama hiyo, mwaweza kumsaka mwenyekiti au katibu wa kamati hiyo aseme nanyi,” akasema Said akizungumza na wanahabari punde baada ya mkutano huo, ilivyoripotiwa na Shirika la Habari Nchini Uingereza (BBC).

Alijiuzulu wadhifa wa Waziri wa Utalii majuma mawili yaliyopita kutokana na kile alichokitaja kama “mazingira yasiyo mazuri na yenye usumbufu”.

Hata hivyo, kujiuzulu kwake kumehusishwa na uhaba wa pombe unaokumba Zanzibar, hali ambayo imeathiri pakubwa sekta ya utalii. Kisiwa hicho ni kimojawapo cha vituo vya kitalii Afrika ambavyo hutembelewa na idadi kubwa ya watalii.

Kutokana na uhaba huo, bei ya pombe imepanda kwa kiwango cha asilimia 100 baada ya mfumo wa usambazaji bidhaa hiyo kuvurugwa na kubadilishwa ghafla kwa waagizaji.

Kabla ya kujiuzulu kwake, Bw Said aliilaumu waziwazi Bodi ya Kudhibiti Pombe Zanzibari (ZLCB) kwa usimamizi mbaya wa sekta ya vileo.

Lakini Rais wa Zanzibar Hussein Mwinyi alimtuhumu kwa kuendeleza mgongano wa kimasilahi alipokuwa akihudumu kama waziri.

Baadhi ya ripoti zimehusisha mmoja wa jamaa za Bw Said na kampuni moja ya kuagiza pombe kutoka nje, ambayo muda wa matumizi ya leseni yake haukoungezwa.

Uhaba wa pombe katika  kisiwa cha Zanzibar unajiri wakati ambapo idadi ya watalii wanaozuru Zanzibar imeongezeka.

Hapa Kenya ni nadra kwa waziri wa serikali kujiuzulu kutokana na kasoro zozote katika wizara anayosimamia.

Wiki moja, iliyopita watu sita waliuawa na wengine zaidi ya 300 kupata majeraha mabaya kufuatia mlipuko wa gesi ya kupikia katika kiwanda kimoja katika kitongoji cha Mradi, eneo bunge la Embakasi Mashariki kaunti ya Nairobi.

Lakini Waziri wa Kawi Davis Chirchir ambayo wizara inasimamia mamlaka inayotoa leseni kwa biashara zozote za gesi alihiari kutoa taarifa kuhusu chanzo cha mkasa hao na kuendelea kusalia afisini.

Nayo Mamlaka ya Kusimamia Sekta ya Kawi na Mafuta (Epra) ambayo ndio hutoa leseni kwa biashara hiyo, ilijiondolea lawama ikisema iliinyima kampuni hiyo lesene ya kujaza mitungi ya gesi mara tatu.

“Leseni ambayo EPRA imetoa kwa kampuni hiyo ni ile ya kusafirisha mitungi ya gesi wala sio kuijaza. Kampuni hii imetuma maombi mara tatu ikitaka leseni ya kujaza mitungi ya gesi lakini tuliinyima kwa kutotimiza masharti yaliyowekwa ya usalama,” Afisa Mkuu Mtendaji wa Epra Daniel Kiptoo akasema Ijumaa wiki jana kwenye mahojiano katika runinga ya NTV.

Mnamo Mei 25, 2008, aliyekuwa Waziri wa Fedha katika Utawala wa Rais Mwai Kibaki, Amos Kimunya alisema kuwa heri afe kuliko kujiuzulu baada ya kutajwa katika sakata ya uuzaji wa mkahawa wa Grand Regency, sasa Laico Regency.

Hoja ya kumtaka ajiuzulu iliwasilishwa na aliyekuwa Mbunge wa Ikolomani wakati huo Dkt Boni Khalwale aliyemhusisha Kimunya na uuzaji kinyume cha sheria cha mkahawa uliokuwa wa kifahari jijini Nairobi nyakati hizo.

Kwa sasa Dkt Khalwale ni Seneta wa Kaunti ya Kakamega.

Hoja hiyo iliwasilishwa mnamo Mei 21, 2008.

Lakini akiongea katika eneo bunge lake la Kipipiri baadaye mnamo Mei 25, 2008, Kimunya aliapa kwamba katu hangejiuzulu.

“Heri nife badala ya kujiuzulu wadhifa wangu wa waziri wa Fedha kutokana na madai ambayo hayana msingi wowote. Waliowasilisha hoja hiyo wamechochewa kisiasa kuniharibia jina,” akafoka.

Mwishoni mwa mwaka 2023, Waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen alipuuzilia mbali shinikizo za kumtaka ajiulu kufuatia visa vitatu vya kupotea kwa umeme kote nchini, ikiwemo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), Nairobi.

  • Tags

You can share this post!

Mwalimu ajiua kwa kukataliwa na ex, aacha mke mjamzito

Wanafunzi Moi wakubaliana na sheria ya kuzima vimini

T L