Waziri Kuria ‘mwanasiasa’ Ruto hana budi kumvumilia na sarakasi zake
NA MWANGI MUIRURI
KATIKA siku za hivi karibuni, Waziri wa Utendakazi wa umma Bw Moses Kuria amejipa nembo ya mwanasiasa ambaye humkanganya Rais William Ruto na serikali kwa jumla.
Mara kwa mara, amejitokeza wazi kwamba kisiasa ni mwanasiasa ambaye kumkabili na kumdhibiti ni sayansi ya kipekee.
Rais Ruto alikuwa amempa Kuria Uwaziri wa Biashara lakini mabalozi walisemwa kuanza kumsusia kutokana na ulimi wake telezi hadi akahamishiwa wizara yake ya sasa.
Nukuu za Bw Kuria huzua utata kiasi kwamba mwishoni mwa mwaka jana, 2023, Naibu wa Rais Rigathi Gachagua alisema alikuwa amejipa wajibu wa kumsaidia Waziri Kuria kuhepa maongezi hasi.
Wadadisi sasa wanasema kwamba Bw Kuria ni mwanasiasa mjanja sana na ambaye anaelewa kwamba ana umuhimu wa kipekee na ambao humwezesha kujipa uhuru wa kufanya na kusema atakavyo kutokana na hali tete ya siasa nchini na pia Mlima Kenya.
“Bw Kuria ni mweledi wa kisiasa na ana tajiriba si haba. Alianza siasa wakati wa Rais Mwai Kibaki (ambaye ni mstaafu na marehemu) na amekuwa katika uundaji wa mikakati ya kuingiza Rais Uhuru Kenyatta na Rais Ruto ikulu. Yeye sio kurutu kisiasa,” asema aliyekuwa afisa wa kiutawala Bw Joseph Kaguthi.
Bw Kaguthi anasema kwamba “Waziri Kuria kisiasa ni sawa na mtoto ambaye mzazi hajui amfanyie nini, mapenzi ya mwana yakidumu”.
Anafafanua kwamba “ikiwa kuna mwanasiasa aliyesimama na Rais Ruto katika kampeni za 2022, ni Kuria ambaye alikuwa mbunge wa eneobunge la Rais Kenyatta la Gatundu Kusini”.
Bw Kaguthi anaonya kwamba “Rais Ruto kwa kuwa hupenda kudumisha urafiki na wale waliomfanikishia ndoto yake ya kuwa rais, huwa anasitasita kumchukulia Bw Kuria hatua hata wakati kila mdadisi anaonelea hatima yake ingekuwa tu kufutwa kazi”.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Jamii ya Agikuyu, Bw Wachira Kiago, baadhi ya maongezi hudunisha hata mila za kijamii.
Bw Kiago alisema kwamba “ni hivi majuzi ambapo tuliskia wanasiasa wakitishia kufika katika lango kuu la Mama Ngina Kenyatta na watoe uume wao waende haja ndogo kama njia ya kumwonyesha dharau”.
Bw Kiago alisema “matamshi na matendo ya aina hiyo kwa wakati mwingine huzua wasiwasi mkuu”.
Aliyekuwa Waziri Msaidizi (CAS) katika Wizara ya Spoti na Elimu Zack Kinuthia anasema kwamba Bw Kuria ni kizungumkuti.
“Bw Kuria anapendwa na kuchukiwa kwa viwango sawa. Inategemea unamchambua ukiwa umesimama upande gani wa utiifu wa siasa. Maisha yake yana utata mwingi, lakini wapiga kura Mlima Kenya kwa wakati mwingine humwona kama mtetezi sugu wa maslahi yao,” Zack asema.
Anasema kwamba “Bw Kuria ataendelea kuwatatiza Rais Ruto na Naibu wake Bw Gachagua, kwa kiwango kikuu na wasijue jinsi ya kukabiliana naye”.
Bw Kinuthia anadadisi kwamba kwa sasa iwapo Rais Ruto atamfuta kazi Waziri Kuria, atatatiza serikali Mlima Kenya na kitaifa.
“Ukimfuta Kuria kazi saa hii ataingia mtaani na azindue chama chake na aanze kampeni za 2027. Kwa sasa Mlima Kenya siasa si tamu sana kwa serikali ya Kenya Kwanza na kujiunda kwa upinzani kunaweza kuwa rahisi,” asema.
Aliyekuwa mbunge wa Gatanga Bw Nduati Ngugi anasema kwamba Bw Kuria amekuwa na nia ya kuwa kinara wa siasa za Mlima Kenya.
“Kumfuta kazi kutampa kisingizio cha kuzindua siasa hizo Mlima Kenya na jinsi nimjuavyo Bw Kuria, anaweza akavutia idadi ya umati kutikisa serikali,” asema.
Anaongeza kwamba tajiriba ya Bw Kuria kisiasa inaweza ikamtuma kuunga mkono wanasiasa kama Ndindi Nyoro ama Mwangi Kiunjuri kuwa vinara wa siasa za Mlima Kenya au hata akimbie kwa Bw Kenyatta ambaye amekuwa donda sugu kwa utawala wa Rais Ruto.
“Yule ambaye kwa sasa hawezi akafurahia harakati za kuundwa kwa mrengo mwingine wa kisiasa Mlima Kenya ni Bw Gachagua ambaye anatatizika si haba kuwa msemaji wa Mlima Kenya,” akasema Bw Ngugi.
Katika hali hizo, wanasema kwamba Rais Ruto na naibu wake Gachagua hawana budi ila tu kuendelea kumvumilia Bw Kuria na sarakasi zake tele.
“Siasa ni kuhusu maslahi na njama za kudumisha uthabiti wa kukupa uwezo wa kuibuka mshindi. Kwa sasa, kumfuta Kuria kutatikisa uwezo huo na kuzidishe mitafaruku katika siasa za Mlima na kitaifa. Ningekuwa Ruto ningekaa tu nikimpa macho Bw Kuria,” ashauri Bw Kinuthia.