• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Wenyeji Lamu wakataa mitaa ya kwao kuitwa majina ya kigeni

Wenyeji Lamu wakataa mitaa ya kwao kuitwa majina ya kigeni

NA KALUME KAZUNGU

KUWEPO kwa miji na mitaa ya kisiwa cha Lamu ambayo majina yake ni ya kigeni sasa kunapingwa vikali na wenyeji.

Unapofika kwenye kisiwa cha Lamu, utapata kuna mitaa, miji, vijiji na vitongoji vyenye majina kama Kashmir, Kandahar, Bombay, India, Pakistani, Spotlight na mengineyo, ambayo yote hayana uhusiano wowote na uhalisia wa Lamu.

Jamii ya kisiwa cha Lamu ni ile ya Waswahili wa asili ya Kibajuni ambao mara nyingi wamesifika kwa kujikakamua kuenzi, kuhifadhi na kuendeleza mila na tamaduni zao.

Baraza la Wazee wa Jamii ya Wabajuni, kaunti ya Lamu sasa limeanzisha mchakato wa kutaka majina yote ya kigeni na ambayo hayana uhusiano na Mbajuni, yafutiliwe mbali ili kupisha kuanzishwa kwa majina yenye nasaba na jamii hiyo.

Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Jamii ya Wabajuni, kaunti ya Lamu, Bw Feiswal Miji, alieleza masikitiko yake jinsi majina ya kigeni yanavyochangia pakubwa mmomonyoko wa tamaduni, itikadi, mila, desturi na uhalisia wao wa tangu jadi.

Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Jamii ya Wabajuni katika Kaunti ya Lamu, Feiswal Miji. Anasema wameanza harakati za kuondoa majina ya kigeni kwenye mitaa, miji na vitongoji na badala yake kuweka majina ya asili ili kuhifadhi tamaduni zao. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bw Miji alisema Wabajuni wako imara kutetea uhalisia wao na kwamba baraza hilo litaendeleza shinikizo zao hadi pale mitaa, miji, vijiji na vitongoji vyao vitakapobadilishwa majina kutoka ya kigeni hadi yale ya asili ya Lamu kama vile Mkunazini, Mwembeni nakadhalika.

“Inasikitisha kwamba kutawaliwa kwetu na wakoloni na tabia za kimagharibi kumechanganya hata fikra zetu kutawaliwa hadi kupotoka pia. Tumebebwa na mila na desturi za watu wengine kiasi kwamba tumekuja kusahau asili yetu. Mpaka miji yetu tukaafikia kuibandika majina ambayo si yetu wala hayana uhusiano na sisi kama jamii ya Wabajuni. Hilo ni jambo limetukera na tutajaribu kukomesha,” akasema Bw Miji.

Alishikilia kuwa miji kama Kashmir, Kandahar, Bombay na mingineyo haina nasaba na Mbajuni na kwamba wakati umewadia kuhakikisha yamebadilishwa na majina yenye uhusiano na Mbajuni yaibuliwe.

“Majina kama Mwembeni, Mkunazini na mengineyo kiasili ni yetu. Ikumbukwe kuwa miji ndiyo inayoashiria pakubwa utamaduni na uhalisia wetu wa tangu jadi kama jamii. Hatutaki kizazi cha miaka ijayo kipotoke kwa kuambiwa eti kuna Kandahar, Kashmir au Bombay, ambapo mtu atashindwa kuelewa miji hii ya nchi za kigeni ikapatikanaje Lamu au ina uhusiano gani na jamii ya Wabajuni? Tutahakikisha tunakomesha hilo kwa kubadilisha na kuweka majina ambayo yana nasaba na sisi kama Wabajuni wa Lamu,” akasema Bw Miji.

Mzee Abubakar Kuchi, ambaye pia ni mwanachama wa Baraza la Wazee wa Jamii ya Wabajuni, Kaunti ya Lamu alishikilia kuwa Lamu, ambayo inatambulika kama kaunti ya utamaduni na historia, inapaswa kudhihirisha kikweli kwamba inaenzi uhalisia wake wa tangu jadi.

Bw Kuchi alisema hilo litadhihirika zaidi endapo mitaa, miji, vijiji au vitongoji vitapewa majina ya asili na ambayo yanaashiria waziwazi historia ya eneo hilo.

“Tunafaa kudhihirisha kuwa kweli tunaenzi mila na tamaduni zetu kupitia majina tunayowapa watoto wetu, yale ya mitaa, miji, vijiji, vitongoji na mengineyo mengi. Tukianza kupenyeza usasa kwenye masuala muhimu kama mitaa yetu kuipa majina yasiyo ya asili yetu basi tutakuwa tunafanya kinyume,” akasema Bw Kuchi.

Bi Fatma Ali anaamini kuendelezwa kwa mila na desturi za Wabajuni kupitia matumizi ama upeanaji wa majina ni jambo la kuzingatiwa kwani litasaidia kupitisha tamaduni za jamii yao kutoka kizazi kimoja hadi kingine, hivyo kuzuia zisiangamie.

Matumizi ya majina asilia pia ni hatua muhimu itakayohakikisha hadhi ya Lamu inaheshimiwa na kudhibitiwa.

Mnamo 2001, Shirika la Umoja wa Mataifa Kuhusu Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) liliorodhesha mji wa kale wa Lamu kuwa miongoni mwa maeneo yanayotambuliwa zaidi ulimwenguni kwa kufaulu kutunza, kuenzi na kuhifadhi mila na tamaduni zake, yaani Unesco World Heritage Site.

  • Tags

You can share this post!

Rais Ruto apiga makofi badala ya kutikisa mguu

Didmus Barasa amtaka Uhuru kumpigia debe Raila uenyekiti AUC

T L