Makala

Wenyeji mjini Kenol kuchanga Sh200,000 kuburudisha polisi

January 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MWANGI MUIRURI

RAIA katika eneobunge la Maragua wanaolalamika kulemewa na gharama ya maisha kiasi cha kuhangaika kupata chakula na karo, sasa watatakiwa kuchanga Sh200,000 za kugharimia hafla ya mlo wa polisi wao.

Ingawa hivyo, kutoa ni moyo kwa sababu hakuna anayelazimishwa.

Bajeti hiyo itakuwa ya kununua bidhaa nyingi ikiwemo minofu na vinywaji vya kuburudisha maafisa hao mnamo Januari 26, 2024, kama njia moja ya kuwapa motisha wa kuwahudumia mwaka huu mpya wa 2024.

“Mimi niko katika kamati ya maandalizi na tutakuwa na muziki, mlo wa chapati, nyama, mchele, maji ya chupa na pia juisi. Sio eti ni polisi peke yao watakula, bali tutawaalika hata raia tule na tunengue viungo pamoja,” akasema mdokezi wetu.

Ili kuupa mchango huo sura ya kiserikali, kituo cha polisi cha Kenol kimeunda kadi za mwaliko zikiwa na nembo zote za idara ya polisi na pia kutiwa sahihi huku kikitangaza kwamba mgeni wa heshima katika hafla hiyo atakuwa mbunge Mary wa Maua.

Sherehe hiyo itaandaliwa katika kituo cha polisi cha kenol na ambapo nambari ya simu ya kutuma pesa imepeanwa kuwa ya karani wa kituo hicho.

Bi Wanjiku Mwangi ambaye ndiye ambaye nambari yake ya simu imepeanwa, aliambia Taifa Leo kwamba ndiye amepewa jukumu hilo la kukusanya michango.

“Ni kwa hiari, sio kwa kulazimishwa… Ni katika hali ya kusaka umoja na ushirikiano,” akasema Bi Mwangi.

Hata hivyo, baadhi ya wamiliki wa baa walilalama kwamba wameagizwa wachange aina mbalimbali za mvinyo na pombe.

“Badala ya waende wakamate waandalizi wa chang’aa ili wapate kinywaji cha kujiburudisha, wanakuja kwa baa zetu ambazo tunalipia ushuru, mishahara ya wafanyakazi wetu, upangaji na pia leseni za kuhudumu na kututaka tuwachangie pombe na sigara,” akadai mhudumu mmoja wa baa.

Aliteta kwamba “hawa ndio tea wale polisi ambao wamekuwa wakitutia mbaroni mtaani na kutuachilia baada ya kutudai pesa kisha tena wanatualika harambee ya kuwaburudisha”.

Aidha, baadhi ya wauzaji maziwa, juisi, maji, soda, nyama na pia mboga wameteta kulazimishwa kuchangia mlo huo wa afande.

Kamanda wa polisi wa Murang’a kusini Bi Jane Nyakeruma alikataa kujadili mpango huo.

[email protected]