Wezi watumia machozi kutekeleza uporaji mazishini
NA WANDERI KAMAU
KUMEZUKA mtindo mpya miongoni mwa waporaji, ambapo sasa wamekuwa wakitumia hafla za mazishi kuwapora watu.
Ijapokuwa kwa kawaida mazishi huwa hafla ya kuwafariji jamaa waliofiwa, uchunguzi wa Taifa Leo umebaini kuwa waporaji wamekuwa wakitumia njia za kijanja kujifanya waombolezaji.
Uporaji huo umekuwa ukifanyika hasa katika maeneo ya vijijini.
Kulingana na waathiriwa wawili wa uporaji huo waliozungumza nasi, waporaji hao huwa wanajifanya jamaa za waathiriwa kwa kuangua vilio, hasa marehemu anapoteremshwa kwenye kaburi.
“Wanapoangua vilio na kujiangusha, bila shaka kuna watu ambao huwa wanawabeba na kuwapeleka mbali na eneo la kumzikia marehemu. Waporaji hao huwa wamejipanga. Ingawa bado huwa wanatiririkwa na machozi, huwa wanawaelekeza watu wanaowasaidia kwenda katika eneo fulani, karibu na waporaji wale wengine. Wanapofikishwa hapo, waporaji hao huungana pamoja na kuwageuka watu waliojitolea kuwasaidia,” asema Bw James Chege, ambaye ni mwathiriwa wa uporaji huo mpya.
Kulingana na Bw Chege, ambaye ni mkazi wa kijiji cha Githunguchu, eneobunge la Ndaragwa, Kaunti ya Nyandarua, waporaji hao hufanya hivyo wakati mazishi yanapokaribia kumalizika na watu wengi wanapoelekea kwenye kaburi.
“Nyakati hizo, karibu kila mwombolezaji huwa ameelekea kwenye kaburi, huku wengine wakiondoka. Hivyo, si wengi huwa wanajishughulisha sana na yale yanayoendelea,” akasema Bw Chege.
Wiki iliyopita, Bw Chege alipoteza simu yake baada ya kujitolea ‘kumsaidia’ mwanamume alijejifanya kuzimia kwenye hafla moja ya mazishi katika eneo hilo.
“Tulipofika karibu na kaburi, alipiga kamsa na kuanguka. Ili kumwokoa, tulimchukua pamoja na watu wengine wanne—wanawake watatu na wanaume wawili. Alituelekeza mahali ambapo angependa tumlaze, akisema alikuwa amezidiwa na hisia. Tulipigwa na butwaa tulipovamiwa na watu waliotoka vichakani na kutuzunguka. Walitupora simu na pesa. Ni tukio lililofanyika kwa haraka sana,” akasema Bw Chege.
Simulizi ni kama hiyo kwa Bi Margaret Wachuka, aliyepoteza Sh1,000 baada ya kujitolea kumsaidia ‘jamaa wa marehemu’ aliyejifanya kuzidiwa na hisia.
“Mazishi hayo yalikuwa yakifanyika katika eneo la Mawingu, Nyandarua, Desemba. Wakati wa kuelekea kwa kaburi ulipokaribia, mwanamke mmoja aliangua kilio na kuanguka. Tulidhani alizimia. Tulimbeba na akatuelekeza tumpeleke karibu na eneo la vichaka, lenye kivuli. Kumbe kulikuwa na wanaume waliokuwa wamejificha hapo! Mara tu tulipofika hapo, alitugeuka huku tukizungukwa. Walikuwa wamejihami kwa visu. Walituamuru tuwape pesa. Bahati nzuri sikuwa na simu yangu,” akasema.
Kulingana na mzee wa nyumba kumi katika eneo la Mawingu, Bw Muthiora Gathungu, wameanza uchunguzi kuhusu visa hivyo na watawaarifu maafisa wa usalama kuhakikisha kuwa wale wanaonaswa wakijihusisha kwenye vitendo kama hivyo wamenaswa.
“Nimepata malalamishi kadhaa kuhusu visa hivyo. Tumeanza ushirikiano na vitengo vya usalama katika eneo hili ili kuhakikisha wale wanaonaswa wamekabilwa vikali,” akasema.