Makala

Wimbo mpya wa Rose Muhando kwa Uhuru, Wakenya waibua hisia mitandaoni

September 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MARY WANGARI

MWIMBAJI nyota wa Injili ambaye ni raia wa Tanzania, Rose Muhando ameyeyusha nyoyo za Wakenya na kuwaacha watumiaji wa mitandao ya kijamii wakishindwa kujizuia kutiririkwa na machozi baada ya kutunga wimbo akiwashukuru Wakenya kwa upendo na msaada wao alipokutwa na mengi ya kuhuzunisha.

Mwanamziki huyo mwenye kipaji alijitosa kwenye mtandao wa kijamii wa mnamo Jumanne, Septemba 24, ambapo alifungua moyo uliofurika shukran kwa Rais Uhuru Kenyatta na taifa la Kenya kwa kusimama naye.

“Ahsante Rais Uhuru Kenyatta na Wakenya wote kwa upendo mlionionyesha nilipokuwa mgonjwa Kenya. Sasa niko salama na tayari kumfanyia Mungu kazi,” aliandika katika kipande kimojawapo cha wimbo wake.

Kupitia kibao cha kuibua hisia kilichochapishwa na mwanamuziki mwenzake wa injili, Steven Kasolo, Muhando alimimina sifa sufufu kwa Kiongozi wa Taifa la Kenya, viongozi na Wakenya.

Kisha kwenye pambio, mwimbaji huyo anamwomba Mungu kumpanulia mipaka Rais na kuwalinda Wakenya.

“Shukran zangu kwa taifa la Kenya, viongozi na Wakenya kwa kuokoa maisha yangu. Uhuru, yabarikiwe malango yako. Uhuru, yafanikiwe malango yako. Taifa lako libarikiwe. Kenya ulindwe milele ifanikiwe mipaka yako. Kenya uinuliwe,” akatiririsha mistari.

Mali

Aidha katika wimbo huo, mwimbaji huyo wa kibao kilichovuma cha ‘Nibebe‘, anasema hana mali wala nguvu za kuwapa Wakenya kwa ukarimu wao kwake lakini anaiamrisha mbingu kuitangazia baraka Kenya, raia wake na vizazi vyao.

“Mlinifungulia milango yenu, mkanipokea mikononi mwenu. Mkanionea huruma, malango yenu na yafanikiwe. Mlinisaidia, sina chochote cha kuwapa, sina mali wala nguvu. Mbingu nazinene vyema kuwahusu Wakenya na watoto wenu.

Mungu ikumbuke Kenya na vizazi vyake. Mungu awe adui wa maadui zenu. Mungu awe mtesi wa watesi wenu na apigane kinyume na wanaopigana nanyi,” anaendelea.

Mnamo Novemba 2018 Muhando aligonga vichwa vya habari baada ya video kuenezwa mitandaoniambapo alionekana akiombewa na mhubiri anayezingirwa na utata, James Ng’ang’a, ambapo alidaiwa kupungwa pepo.

Mwimbaji huyo wa jadi alipata makao Kenya ambapo amekuwa akiishi na mwanamuziki mwenzake wa injili Anastacia Mukabwa alipokuwa akiugua.

Kibao hicho ambacho bila shaka kitakuwa kikichezwa mno katika hafla nhcini Kenya, ndio wimbo wa pili baada ya wimbo kwa jina ‘Walionicheka’ alichomshirikisha mwanamuziki wa injili mwenye utata Ringtone Apoko.