Winnie Odinga asifiwa kusimama ‘kiume’ kutoka babake akiwa mgonjwa mpaka mauko
WINNIE Odinga, bintiye Kinara wa ODM Raila Odinga, amesema kuwa yupo tayari kwa majukumu ya kisiasa nchini.
“Mheshimiwa Rais niko tayari kwa majukumu ya nyumbani,” akasema Winnie wakati ambapo alikuwa akitoa rambirambi zake mbele ya hadhira iliyokuwa imefurika uwanja wa Chuo Kikuu cha Jaramogi Oginga Odinga.
Kwa sasa, Winnie ni mbunge katika Bunge la Jumuiya ya Afrika (EALA) baada ya kupewa nafasi hiyo kupitia tiketi ya ODM.
Winnie aliyekuwa na babake alipoaga dunia India Jumatano iliyopita amekuwa akisifiwa mtandani kama ambaye yupo pazuri zaidi kurithi siasa za Raila.
Seneta wa Siaya Dkt Oburu Oginga pia alimsifu Winnie kutokana na jinsi alivyosimama na babake hadi dakika ya mwisho.
Wakati huo huo, hata wakati ambapo huzuni ilitanda katika hafla ya kumzika marehemu Waziri Mkuu Raila Odinga kulikuwa na nyakati za ucheshi ambazo zilitanda na kuwaacha waombolezaji wakivunjika mbavu.
Seneta wa Siaya Dkt Oburu Oginga, aliwaacha wengi wakicheka na kudondokwa na machozi ya furaha alipokuwa akimshukuru Mjane Mama Ida Odinga kwa kusimama na ndugu yake kwa zaidi ya miaka 52 wakiwa kwenye ndoa.
Ndoa ya Raila na Mama Ida imedumu kwa muda huo. Dkt Oburu alirejelea tukio la 1984 wakati ambapo Raila alikamatwa baada ya mapinduzi ya kijeshi 1982 na akaishia kusalia gerezani kwa muda wa miaka tisa.
Wakati huo Mama Ida alikuwa na umri wa miaka 37 pekee na Dkt Oginga alisema kuwa ingekuwa wanawake wengine wangemtoroka Raila kwa sababu ya masaibu yasiyoishia kisiasa.
“Kuna wale wenye damu moto na wangetoroka katika umri wake,” akasema Dkt Odinga na kuzua kicheko kabla ya kuendelea kuwatambua wake zake wawili ambao alikuwa amekosa kuwatambua hapo awali.
Mwenyekiti wa Baraza la Jamii ya Waluo Odungi Randa naye alizua kicheko kwa kusimulia kuwa idadi ya jamii ya Waluo ilikuwa milioni nne pekee na lazima wazaane ili kuongeza idadi yao.
“Wajaluo kutoka DR Congo wamekuja hapa na kuniuliza idadi ya Wajuluo Kenya nzima na nimesema kuwa ni milioni nne pekee. Hiyo idadi ni chini sana na kila mtu akitoka hapa, aende ahakikishe kuwa anampa mke mimba ili kuwapata watoto wanaoitwa Raila,” akasema Randa ambaye pia ni mfungwa wa kisiasa jinsi alivyokuwa Raila.
Gavana Wanga ambaye alikuwa mfawidhi wa sherehe aliwaambia wanaume kuwa kibarua hicho hakingekuwa rahisi na lazima wajitahidi.
Kulingana na sensa iliyofanyika mnamo 2019, idadi ya jamii ya waluo ni 5,066,966.